Friday, October 28, 2011

Matonya ndani ya Singida leo katika BLACK & WHITE PARTY.

Msanii kutokea Tanga Matonya,leo atawatumbuiza wakazi wa Singida Mjini hasa wanafunzi wa Uhasibu{T.I.A} katika show ya BLACK & WHITE PARTY itakayofanyika pande za Singida Motel kuanzia mida ya saa mbili usiku hadi majogoo.Shoe pia itapambwa na wakali tokea pande za Uhasibu{T.I.A}
Tukutane Singida Motel wakazi wote wa Singida mjini.

Mwenge Waanza Mbio Za Siku Mbili Tabora kutokea Singida

Mwalimu mkuu shule ya Msingi Uwanza, wilaya Iramba Maria Ntoga akisoma taarifa fupi ya msitu wa asili unaomilikiwa na vijiji viwili vya Gumanga na Msingi, kabla ya kuziduliwa rasmi na kiongozi wa mbio za Mwenge Fatuma Rashid Khalfan.

Wakimbiza mwenge wakiwa picha ya pamoja leo asubuhi katika kijiji cha Shelui,Iramba, kabla ya kuanza safari kuelekea mpakani mwa mikoa ya Singida na Tabora.

Mkuu wa wilaya Igunga hajati Fatuma Kimario akiwa na mkuu wa mkoa wa Tabora Fatuma Mwasa, wakisubiri mpakani kukabidhiwa Mwenge wa Uhuru kutoka kwa uongozi wa mkoa Singida

Mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone(kushoto),akimkabidhi Mwenge wa Uhuru mkuu wa mkoa Tabora Fatuma Mwasa, leo asubuhi mpakani mwa mikoa hiyo.

Kiongozi wa mbio za Mwenge akiwa amewakabidhi chandarua, sare za shule na viatu watoto wanao ishi katika maingira hatarishi wanaosoma shule ya Uwanza, tarafa ya Kinampanda.vifaa hivyo vimegharamiwa na halmashauri ya wilaya ya Iramba

Jamii ya kabila la Kitaturu wanaoishi wilayani Igunga, wakiendelea na shamra shamra baada ya uongozi wa wilaya hiyo kukabidhiwa Mwenge wa uhuru kuendelea na mbio zake.

Mwenge wa uhuru umemaliza mbio zake za siku mbili mkoani Singida jana jioni, na leo jumatano asubuhi umekabidhiwa kwa uongozi wa mkoa wa Tabora, Ukiwa Singida umekimbizwa kilomita 348.7 na kuzindua,kufungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 18,ya thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 448.7.

Miradi 10 Yazinduliwa Na Mwenge Wa Uhuru Singida

Mkuu wa mkoa Dodoma Rehema Nchimbi akimkabidhi Mwenge wa Uhuru mwenzake wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone, katika kijiji cha Lusilile,wilayani Manyoni

Katibu tawala wa mkoa wa Singida Liana Hassan(Kulia), akiteta jambo na wasaidizi wake, kabla ya kuupokea Mwenge wa Uhuru ulioanza mbio zake mkoani Singida leo jumatatu.

Kiongozi wa mbio za Mwenge mwaka huu Mtumwa Rashid Khalfani,kutoka mkoa wa Kaskazini Unguja, akiweka jiwe la msingi, jengo la utawala shule ya sekondari Ikungi, wilayani Singida jana lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh.Milioni 38.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma akiauaga Mwenge kwa kuselelebuka, katika kijiji cha Lusilile kilichopo mpakani mwa Singida na Dodoma

Oktoba 24,2011:JUMLA ya miradi kumi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 129.2, imezinduliwa, kufunguliwa na kuwekewa mawe ya msingi, na Mwenge wa Uhuru mwaka huu, mkoani Dodoma.
Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa mkoa huo, Rehema Nchimbi, kwenye makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru, kwa uongozi wa mkoa wa Singida,yaliyofanyika katika kijiji cha Lusilile,wilayani Manyoni

Msafara Wa Punda!


Na mbwa wamo ingawa hawaonekani. Pichani msafara wa punda waliobeba magunia ya mkawa ukielekea Singida Mjini kutoka vijiji vya kando ya mji. Picha hii nimeipiga leo alfajiri kabla ya kupambazuka

Sunday, October 23, 2011

Manchester United 1-6 Manchester City

Vita CCM yamgusa mtoto wa JK, Ikulu;MAKUNDI MAWILI YATUNISHIANA MISULI URAIS 2015


MINYUKANO inayohusisha makundi mawili ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), sasa imeanza kugusa taasisi ya Urais baada ya jina la Rais Jakaya Kikwete, mwanawe, Ridhwan na Ikulu kuanza kuhusishwa katika malumbano yanayoendelea.Jina la Rais na Ikulu limeanza kutajwa hivi karibuni katika mgogoro ulioanza baada ya moja ya kundi la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa chama hicho, (UVCCM), likiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wake wa taifa, Benno
Malisa na baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa umoja huo, kuzuiwa na Jeshi la Polisi kufugua matawi mkoani Arusha, kwa kile kilichodaiwa maelekezo ya mtoto wa kigogo.

Ingawa Malisa na wenzake hawakutaja jina la mtoto huyo wa kigogo
walipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Hospitali ya St. Thomas mjini Arusha, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Ole Millya alimtaja,Ridhwani Kikwete kuhusika na njama za kuzuia shughuli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Lash Garden, walikofikia viongozi hao.

“Ingawa polisi wanadai kutunyima kibali cha maandamano ya kufungua mashina ya Umoja wa Vijana na mkutano wa hadhara kwa kile wanachodai taarifa za kiintelijensia kugundua kutatokea uvunjifu wa amani, tumepata habari kuwa Ridhwan ndiye kapiga simu kuelekeza tunyimwe.Sisi tutaendelea na shughuli yetu liwalo na liwe, wacha watupige mabomu kama Chadema,” alisema Millya.

Millya pia alimshambulia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye na kumtaja kama ugonjwa wa saratani kwa chama hicho na kuonya kwamba kama hatadhibitiwa, atasababisha anguko la chama.

Millya alizungumzia pia tamko la Baraza la UVCCM Mkoa wa Pwani lilotolewa mapema mwaka huu na kuzua mtafaruku miongoni mwa wanaCCM kuwa rais ajaye hawezi kutoka Kanda ya Kaskazini na kwamba ni Rais Kikwete pekee ndiye anayemjua mrithi wake.

Mwenyekiti huyo alisema kauli hiyo ni tata, kandamizi na yenye kuonyesha dharau kwa watu wa Kanda ya Kaskazini na demokrasia nchini na kuongeza kuwa Ikulu na Rais Kikwete, ilipaswa kutolea kauli ya kuthibitisha au kukanusha maneno hayo ya vijana wa Mkoa wa Pwani yaliyotamkwa mbele ya Ridhwan lakini hadi sasa hakuna ufafanuzi uliotolewa, hivyo kuzua hofu kuwa pengine vijana hao walielekezwa kutoa ujumbe huo na mamlaka za juu za nchi (Rais na Ikulu).


Kiongozi mwingine wa CCM ambaye wiki hii alimrushia kombora Nape, ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole aliyedai kuwa Katibu huyo kwa sasa hafanyi kazi ya kueneza na kujenga chama badala yake anakibomoa kwa kung’ang’ania hoja ya kujivua gamba, akilenga watu binafsi hivyo kupotosha nia njema ya Rais Kikwete iliyeanisha falsafa hiyo, akilenga marekebisho ya mfumo mzima wa uongozi, uanachama na chaguzi ndani ya chama.

Ole Nangole ambaye pia alizungumza na waandishi mjini Arusha, alienda mbali zaidi kwa kumuita Nape kuwa ‘muasi namba moja’ ndani ya CCM baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa waasisi wa Chama Cha Jamii (CCJ), kilichokwama kupata usajili baada ya kushindwa kutimiza masharti.

Mtu mwingine aliyemshambulia hadharani Nape ni Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM taifa, Malisa aliyedai Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, anapotosha nia na kauli ya Rais Kikwete kuhusu dhana ya kujivua gamba kwa kung’ang’ania kutaja majina ya viongozi wachache ndani ya chama kuwa ndio walengwa wa falsafa hiyo.

Akijibu tuhuma hizo Nape, alisema kuna kundi dogo la watu ndani ya chama hicho wenye nguvu ya pesa, wanaotaka kufanya njama za kumng'oa mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete, kwa kigezo cha kutenganisha kofia mbili, urais na uenyekiti.

Matukio makubwa yaliyotokea wiki hii ya Makamu Mwenyekiti wa UVCCM taifa, Malisa kutoa matamshi mazito ya kumshutumu Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi na Uchumi ya Umoja huo Ridhwan hadharani, yameibua sura mpya ya mvutano huo.

Malisa ambaye awali alikuwa swahiba mkubwa wa Ridhiwan ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa taifa wa CCM Rais Kikwete, wakati wa kampeni za kuwania Uenyekiti wa Umoja huo mjini Dodoma, walikuwa kambi moja wakipigana kushawishi wajumbe, sasa hawako pamoja tena.

Nguvu za makundi ikoje?
Kundi la watuhumiwa wa ufisadi
Nguvu kubwa ya kundi hili linalodaiwa kuongozwa na makada wanaohumiwa kwa ufisadi ndani ya chama hicho ni;
1. Kuwa na mtandao mkubwa ndani ya chama ambao ulitumika kumwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
2. Jumuia zote za chama ukiwemo Umoja wa Vijana (UVCCM), Umoja wa Wanawake (UWT) na Jumuiya ya Wazazi ambazo zina wanachama hadi ngazi ya shina.

3. Kundi hili linaungwa mkono pia na wenyeviti wa mikoa
19 wa CCM kutoka bara na visiwani

4. Lina nusu ya wajumbe wa Halmashuari Kuu ya Taifa
(NEC) wanaoweza kushinikiza maamuzi magumu
yakapitishwa na chama.
5. Kundi hili pia lina nguvu kubwa ndani ya bunge likiwa
na wabunge wengi wa CCM wanaoliunga mkono.
6. Lina nguvu kubwa ya fedha inayolifanya kutumia
kuwashawishi wana CCM wengi kuliunga mkono.

Nguvu ya kundi la Mwenyekiti Kikwete

Kundi hili ni lile la wana CCM wanaounga mkono maamuzi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete ya chama kujivua gamba.

1. Kundi hili linaungwa mkono na viongozi ndani ya CCM ambao wanapambana na ufisadi wakiwamo baadhi ya wabunge, mawaziri, makada na wanachama wa kawaida wa chama hicho.

2. Nguvu nyingine ya kundi hili, ni kwamba linaongozwa na Mwenyekiti ambaye ana dola, ana uwezo wa kuteua viongozi mbalimbali hususan makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya.

3. Mwenyekiti ana nguvu kwenye vikao, anaweza kunishikiza jambo ambalo analitaka na likafanyika kama anataka.

4. Mwenyekiti anaungwa mkono na wanachama wa kawaida wa CCM ambao wengi wao wapo katika ngazi ya matawi.

5. Raslimali zote za chama zipo chini ya Mwenyekiti.

6. Nguvu ya kundi hili pia inatokana na kuungwa mkono na kundi la viongozi wastaafu wa chama wakiwamo baadhi ya mawaziri wakuu.

Kauli za makada wa CCM

Kada wa CCM Mwanza

KADA wa CCM na Diwani wa Kata ya Lugata Kome wilayani Sengerema, Adrian Tizeba amesema falsafa ya chama chake ya kujivua gamba haina lolote kwani haina nia ya kukinusuru bali kuongeza minyukano ya makundi ambayo alisema yatasababisha kifo cha chama hicho.

Aliiambia Mwananchi Jumapili kuwa kutokana na hali ilivyo na jinsi anavyoona mambo ndani ya CCM, chama hicho hivi sasa kimegawanyika katika sura mbili kwa wakati mmoja, hivyo kinaweza kufa.

“Ninachoweza kutabiri juu ya chama changu ni jambo ambalo liko wazi, kutokana na kuwa na makundi mawili moja linalomtii na kuamini misingi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, na lingine linaloamini katika kujilimbikizia mali basi, kutaibua fujo kubwa ndani ya chama na kitavunjika,” alieleza.

Alisema kwa upande mwingine wananchi wameanza kuonekana kukichoka kutokana na kutupa misingi ya Baba wa Taifa, hatua ambayo imesababisha chama kutekwa na kundi la wafanyabiashara wanaotaka kujinufaisha.

Mwenyekiti CCM Shinyanga
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, alisema wana CCM wanapaswa kurudi kwenye kanuni na kutoa matatizo yao kwa njia za vikao na kubainisha kuwa kuyasema majukwaani ama hadharani kunakifanya chama kuonekana kama kina matatizo makubwa.

Mgeja alisema hali inavyoonekana sasa siyo nzuri, hii inatokana na baadhi ya wanachama kukiuka utaratibu wa vikao na kuwa wazungumzaji nje ya vikao.Alionya kwamba iwapo jambo hilo litaendelea basi upo uwezekano wa CCM kupoteza mwelekeo.

“Ninavyoona mwelekeo wa sasa siyo mzuri, chama kinaoutaratibu wa kutumia vikao, lakini kama watu wanazungumza nje ya vikao ni tatizo, cha muhimu ni kuwaomba wanaCCM kurejea kwenye utaribu wa vikao. Tukiendelea kuzungumza nje ya vikao, chama kitaonekana kina matatizo makubwa sana,” alieleza Mgeja.


Ole Millya
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Millya anasema kimsingi mgongano wa kimawazo unaoibuka sasa haulengi kukidhoofisha chama hicho bali ni kuboresha.

"Hiki ni kipindi cha mpito isionekane watu kutoa mawazo kuwa, wanatumiwa au wana njaa, hali kama hii iliwahi kuvikuta vyama vya Labour nchini Uingereza na Democrat nchini Marekani na walikaa na kufikia maamuzi ambayo yamewafanya kuendelea kushika dola,"alisema Millya.

Alisema suala la kusikilizwa maoni ya vijana linapaswa kupewa uzito kwani wao ndio wapigakura wengi kwa sasa na wanaweza kuwa na mawazo chanya ya kukiboresha chama kuelekea uchaguzi mkuu.

"Haya ambayo yanatokea isionekane kuna mpasuko, hapana sote tunataka kujenga chama chetu hivyo maoni na ushauri ufanyiwe kazi na sio kundi moja kudharau lingine,"alisema Millya.

Akizungumzia kauli yake ya mtoto mmoja wa kigogo kuyumbisha chama hicho mkoani Arusha, alisisitiza ni jambo lililowazi na ana ushahidi nalo kama atahitajika kusema.

"Sisi sio vichaa kuibuka majukwaani na kulalamikia hili, tuna ushahidi na nia yetu sio kulumbana ni kutaka mambo yaende vizuri na CCM iendelee kushika dola,"alisema Millya.

Kanda mwingine wa CCM, Julius Mollel alisema katika kila chama ni busara kuzingatia maoni ya pande zote na kufikia maamuzi sahihi badala ya kudharauliana.

"Mimi ninachoona hali ndani ya CCM ni nzuri tu kwani watu wanasema na kuna marekebisho yanafanyika,"alisema Mollel.

Hata hivyo, wanaCCM wengine, Jeremiah Nkya na Solomon Singu, kwa nyakati tofauti walisema kuumbuana hadharani kwa vigogo wa CCM ni mwelekeo wa chama hicho kopoteza heshima na nguvu ya kushika dola.

Nkya alisema ni aibu chama chenye dola, viongozi wake waanze kulaumiana hadharani na kushutumiana kuwa wanataka kuuana halafu waseme ni uhuru wa mawazo.

"Kuna matatizo ndani ya CCM, la muhimu ni kumaliza malalamiko kupitia vikao sahihi," alisema Nkya.

Kwa upande wake, Singu alifafanua zaidi na kusema makundi ndani ya chama hicho, yamekifikisha pabaya na sasa viongozi wake wameshindwa kuheshimiana.

"Leo Nape (Katibu wa Itikadi na Uenezi) anasema hivi, kesho anaibuka Mwenyekiti wa UVCCM anasema vile, hivyo hivyo hata kwa mawaziri hapa hakuna chama tena kila mtu anafanyakazi kivyake"alisema Singu.

Kauli ya Nape
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape alipotafutwa na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu jana, alijibu kwa kifupi kuwa masuala yote hayo yatazungumzwa kwenye vikao vya chama.
“Masuala yote haya yatajadiliwa kwenye vikao vya chama vitakavyokuja,” alisema Nape bila kutaja ni kikao gani ambacho kitajadili mvutano huo.
“Uamuzi wa kikao gani tutazungumza ni wetu sio wenu, kikao kitakachokuwa na hadhi ya kujadili jambo hili basi litajadiliwa,” aliongeza Nape.

Ridhiwan Kikwete
Ridhwan alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia hali hiyo hakupatikana na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi wa simu, hakujibu.

Katika kuonyesha kuongezeka kwa fukuto la kisiasa ndani ya chama hicho, kada wa maarufu wa chama hicho, aliyekuwa pia Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Juni mwaka huu alitangaza kujivua nyadhifa zote ndani ya chama, huku akiweka wazi kwamba amechoshwa na siasa uchwara zinazoendeshwa na baadhi ya wanasiasa ndani ya chama hicho.


Edward Lowassa
Wiki hii Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa naye alivunja ukimya kwa kuzungumzia tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake, huku akisisitiza kuwa amechoka kukashifiwa na sasa kamwe hatawavumilia wanaomzulia mambo.

Alisema kuanzia sasa hatakubali kuchafuliwa jina na mtu yeyote au chombo chochote cha habari na atakayefanya hivyo, ajiandae kukabiliana na mkono wa sheria.

Alisisitiza kuwa ni jambo lisiloingia akilini kumhusisha yeye na kile kinachodaiwa mkakati wa kumhujumu Rais Kikwete au CCM, wakati yeye ni mbunge anayetokana na chama hicho na kiongozi wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya nje, Ulinzi na Usalama .

Gaddafi ana utajiri wa Sh 140 trilioni:NI SAWA NA BAJETI YA TANZANIA KWA MIAKA 12


KIONGOZI wa Libya aliyeuawa juzi na wapiganaji wa Serikali ya Mpito (NTC), anadaiwa kuacha utajiri wa Sh 139 trioni kiasi ambacho ni sawa na bajeti ya Tanzania kwa miaka 12. Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa fedha hizo ni zile zinazofahamika, alizoweka kwenye benki za nchi kadhaa duniani, huenda alikuwa na hazina zaidi mbali na hiyo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Gaddafi alikuwa anamiliki Pauni 29 bilioni nchini Uingereza (Sh78 trilioni), Dola 32 bilioni nchini Marekani (Sh54 trilioni) , Dola 2.4 bilioni nchini Canada( Sh4 trilioni) na Dola 1.7 bilioni nchini Australia (Sh3 trilioni). Kwa fedha ya Tanzania. Pauni moja ya Uingereza ni sawa na Sh 2,720, Dola moja ya Marekani Sh 1,704, Dola moja ya Canada, Sh 1,692 na Dola ya Australia ni Sh 1,769.

Fedha hiyo kwa ujumla wake ni sawa na bajeti ya Tanzania kwa miaka 12. Juni mwaka huu, Bunge lilipitisha jumla ya Sh11 trilioni kwa matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 .Kiasi hicho kikizidishwa mara miaka 12 zitakuwa Sh132 trilioni, hivyo ukichukulia kiwango hicho, inamaana kuwa fedha za Gaddafi zinatosha kuendesha Tanzania kwa miaka 12 na bado zitabaki Sh trilioni saba.

Alikuwa na nywele, sura bandia
Vipimo vya DNA vilivyofanywa kwenye mwili wa Gaddafi, vimebaini kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Libya, alikuwa na nywele bandia, Jarida la Washington Post limeripoti.Waziri Mkuu wa muda wa Libya, Mahmoud Jibril aliliambia jarida hilo kuwa wachunguzi walifanya vipimo vya damu, mate na nywele na kugundua kuwa nywele hizo si halisi.

Mwili wa kiongozi huyo kwa sasa umehifadhiwa ndani ya msikiti mmoja nje ya mji wa Sirte alikokamatwa na kuuawa ukisubiri kuzikwa baada ya uchunguzi unaotarajiwa kufanywa na Umoja wa Mataifa.

Mwaka 1995, Gaddafi aliwahi kufanyiwa upasuaji wa uso kwa kile alichodai kuwa hataki kuonekana mzee.
“Aliniambia kuwa amekaa madarakani kwa miaka 25 wakati huo na kwamba hataki vijana wa taifa lake wamwone mzee,” alisema Dk Liacyr Ribeiro kutoka Brazil aliyemfanyia upasuaji huo.
Kwa mujibu wa Washington Post, Gaddafi aliwekewa nywele bandia pia aliwekewa mafuta kwenye uso wake yaliyotolewa tumboni, ili kupunguza uwezekano wa uso wake kuonekana wa kizee.

Familia yaomba mwili wa Gaddafi
Mke wa Kanali Gaddafi, Safia, ameibuka na kutaka apewe mwili wa mumewe ili ukazikwe na familia kisha Umoja wa Mataifa ufanye uchunguzi wa kina juu ya kifo chake.Akizungumza kupitia Televisheni ya Rai Tre ya Italia, akiwa uhamishoni nchini Algeria, Safia alisema ni muhimu uchunguzi wa kifo hicho ufanyike ili kujua kama haki ilitendeka ama la.

"Hayo ni makubaliano na familia yangu kwamba tunaomba ufanyike uchunguzi wa kina na baada ya kumalizika kwa uchunguzi tuletewe mwili wake, tutazika wenyewe,"alisema Safia.

Mazishi ya Gaddafi yanayoelezwa kutaka kufanywa kwa siri, yamesitishwa kutokana na tofauti zilizoibuka miongoni mwa maofisa wa Libya baada ya baadhi kutaka ahifadhiwe na wengine atupwe baharini.

Safia alisema; "Kwa utamaduni wa Kiislamu, maziko ya Gaddafi yanapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo na sio kuhifadhiwa kwa siku kadhaa. Naomba uchunguzi ufanyike tena wa kimataifa ili ibainike chanzo cha kifo cha Gaddafi," alisema Safia ambaye alieleza kuwa wanawe, walipiga simu ya baba yao mara baada ya kusikia amefariki dunia, lakini mara zote simu hiyo ilipokelewa na waasi.

Kwa mujibu wa vituo vya televisheni vya Dubai na Jordan juzi, mtoto wa kike wa Gaddafi Ayesha, akizungumza kutoka Algeria, alilalamika kwamba waasi wamemuua baba yake na kumfanyia ukatili mkubwa.

"Niliposikia baba yangu ameuawa sikuamini nikampigia simu lakini, ikapokelewa na mapanya hao (waasi) wa Mediteranian," alisema. Ayesha aliungana na mama yake Safia kutaka wapewe mwili wa baba yao ili wakamzike wenyewe, badala ya kuzikwa na waasi hao alioeleza kuwa hawana haki tena dhidi yake, baada ya kumwua.

Ameutaka Umoja wa Mataifa (UN) usaidie urejeshwaji wa mwili wa Gaddafi kwa familia yake ili ndugu na jamaa wamwage na kumzika kwa heshima zote.Hata hivyo, Kamishna wa Kutetea Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, alisema ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike dhidi ya kifo hicho.

Kaimu Waziri Mkuu wa Libya, Jibril alisema kwamba Kanali Gaddafi alipigwa risasi kichwani wakati alipojaribu kurushiana risasi na waasi.

Serikali mpya kutangazwa leo
Baada ya kifo cha Gaddafi, Serikali mpya ya nchi hiyo inatarajiwa kutangazwa leo. Msemaji wa Jeshi la Libya Abdel-Rahman Busin, alisema kwamba watatangaza kuzaliwa upya kwa Serikali yao katika mji wa Benghazi.

Alisema Serikali hiyo mpya inaiomba familia ya Gaddafi kuhudhuria sherehe hizo za utambulisho Serikali mpya bila wasiwasi wowote kwani baada ya mapinduzi hayo, Libya sasa ni nchi ya kidemokrasia.

“Leo (jana) watu wana furaha na furaha hiyo itaongezeka zaidi kesho (leo) baada ya kutangazwa kwa Serikali yetu mpya ambayo itakuwa ya wananchi wote bila ya ubaguzi,”alisema. Msemaji huyo wa jeshi alieleza kuwa mazishi ya Gaddafi bado hayajajulikana yatafanyika lini lakini kwa vyovyote vile yatasubiri uchunguzi unaotarajiwa kufanywa na Umoja wa Mataifa (UN) wakati wowote kuanzia sasa.

Mabomu, risasi yarindima

VURUGU, milio ya risasi za moto na mabomu ya machozi jana ziligubika mji wa Dodoma kufuatia wakazi wa Mtaa wa Njedengwa, Kata ya Dodoma Makulu kupambana na polisi kupinga hatua ya Manispaa ya Dodoma kuvunja nyumba zao.

Vurugu hizo zilizoanza saa 11.30 alfajiri zilisababisha watu 12 kujeruhiwa vibaya baada ya polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kukabiliana na wakazi wa mtaa huo maarufu mjini Dodoma, wanaodaiwa kuvamia na kujenga katika eneo la mwekezaji.

Risasi za moto zilianza kusikika eneo la tukio huku kundi la polisi pamoja na vijana wenye nguvu (mabaunsa) wakiwa wametanda eneo hilo na kufanya ligeuke uwanja wa mapambano.Mabaunsa hao ambao walikuwa wamefunika nyuso na kuacha sehemu ya macho, waliingia kila nyumba na kuwashambulia waliokuwa ndani huku huku wakiwalazimisha kutoka nje.

Hata hivyo, licha ya polisi kuwa na silaha za moto, wenyeji hao hawakukubali kutii amri, walitoka na silaha za jadi mishale, mapanga na mawe ili kupambana kuzuia bomoa bomoa hiyo.

Baadhi yao walirusha mishale na wengine kutumia mapanga kujihami kila walipovamiwa na vijana hao wenye miraba minne . Hata hivyo wenyeji hao kutokana na silaha dhaifu, walizidiwa nguvu na kujikuta wengi wao wakiwekwa chini ya ulinzi.

Wakati wanaume wakipambana na askari hao, vilio vya akina mama na watoto vilisikika kutoka kila upande huku mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa mfululizo yakizidi kuwachaganya.

Hatua ya kubomoa nyumba hizo ilitokana na hukumu ya Mahakama iliyompa haki mtu anayefahamika kwa jina la Maimu (Sinana Enterprises ) kuwa ni mmiliki halali wa eneo hilo ambalo amepewa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa ajili ya kujenga shule.

Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa wenyeji wa eneo hilo, mwekezaji huyo wakati anapewa sehemu hiyo, tayari kulikuwa na nyumba za watu waliokuwa wakiishi hapo kwa muda mrefu.

“Kwa mfano mimi hapa, nilikuta kuna msitu mwaka 1987 nikaanza kulima na mwaka uliofuata nilijenga hii nyumba yangu, lakini huyo mwekezaji yeye alikuja mwaka 2004 sasa jamani kuna haki hapo?’’Alisema mama mmoja ambaye jina lake halikupatikana baada ya kutishiwa kukamatwa na askari aliyekuwa jirani na kumtaka aondoke ili tingatinga libomoe nyumba yake.

Eneo la tukio
Kwa kiasi kikubwa mabaunsa hao wa kampuni iliyopewa kazi na mwekezaji kusimamia ubomoaji huo, ndio walioonekana kuchochea moto huo zaidi, kwani kila wakati walisikika wakitoa lugha za vitisho kwa wenyeji huku wakiwa wamevalia kofia za kufunika uso.“Habaki bweha hapa, lazima mfundishwe adabu zenu maana sisi tumekuja kikazi zaidi na hamtatusahau kabisa maishani mwenu,’’ alisika mmoja wao akisema.

Mali zaharibiwa
Nyumba nyingi zilizobomolewa zilikuwa na vitu mbalimbali vya thamani, isipokuwa wale waliowahi kutoa vyombo vyao nje ambapo tingatinga hilo la CDA halikuweza kuvigusa.

Baadhi ya maduka yalivunjwa na bidhaa zikiwa ndani huku vijana waliokuwepo aneo hilo, wakisomba bia na kugawana baadhi ya vitu hali iliyolazimisha polisi kuanza kuwazuia.

CDA wakataa kubebeshwa lawama
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Martin Kitila alikanusha vikali kuhusika kwa mamlaka yake kwenye bomoa bomoa hiyo kwa maelezo kwamba anayevunja, ni mwenye eneo hilo.
“Sisi hatuhusiki kabisa katika uvunjaji huo maana tulishamlikisha mhusika, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kufanya atakavyo,’’ alisema Kitila.

Alipotakiwa kueleza ni kwa nini vyombo vyake vimehusika Mkurugenzi huyo alisema, “Hilo sio tatizo kwani mtu yeyote anaweza kuja kuazima vifaa kwetu na tukifikia makubaliano, sisi tunampa’’.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alipinga suala na wananchi kupewa namba na CDA kuwa ni kigezo cha kuhalalishwa na badala yake alisema namba zinazobandikwa huwa ni kwa ajili ya kuwatambua tu wakazi hao, lakini si uhalali wa kuishi au kupimiwa viwanja.

Vyombo vya habari
Vurugu hizo pia zilizua balaa kwa waandishi wa habari waliokuwa kazini eneo ambao walijikuta wakishambuliwa na polisi waliokuwa wakiwakataza kufanya kazi.

Waandishi wa Mwananchi, walijikuta pikipiki yao ikivunjwa kioo na polisi aliyewalalamikia kuwa gazeti lao ni wambeya huku akiwataka wakaandike chochote watakacho. Polisi pia walikuwa wakizuia waandishi kupiga picha.
Licha ya kuonyesha vitambulisho vyao, mwandishi Masoud Masasi na mfanyakazi mwenzake wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Ali Jumanne waliofika eneo la tukio kwa pikipiki, walipigwa na kuzuiliwa kwa muda hadi mmoja wa waandishi alipofika na kuwasaidia ingawa baadaye askari hao waliomba radhi.

Katika vurugu hizo Jumanne alijeruhiwa mguu wa kushoto.
Kwa upande wao Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), gari yao ilivunjwa vioo na wananchi kwa madai kuwa hawataki kuwaona kwani ni watu wa Serikali, kabla ya mtangazaji wa Radio Mwangaza, Jane Charles kushambuliwa kwa mawe na wananchi hao na kujeruhiwa.

Kamanda wa Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen hakuweza kuzungumzia tukio hilo kwani muda wote simu yake ilikuwa ikipokelewa na mtu aliyejitaja kwa jina la Yohana na kujitambulisha kuwa ni msaidizi wake.“Mimi ni msaidizi wa Kamanda naitwa Yohana, muda huu Kamanda hawezi kuzungumza na ninyi, yuko kwenye mapokezi ya Mwenge mtafute baadaye,’’alisema mtu huyo na kukata simu.

Mwenye Kampuni
Msemaji wa Kampuni la Sinana ambaye alijitambulisha kwa jina la Mujibu Ali, alisema kuwa kampuni hiyo ilipewa hati ya kumiliki eneo hilo tangu mwaka 2004 na kwamba hapakuwa na nyumba katika eneo lote.

“Hapa tunamiliki ekari 21 ambazo tunataka kujenga shule na tulianza kumiliki tangu mwaka 2004, lakini hawa jamaa walikataa kuondoka na kesi tulishinda mahakamani tangu Julai 25 mwaka huu na kuwapa notisi, lakini bado hawakuondoka,’’alisisitiza Ali.Majeruhi.Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Nassoro Mzee alisema walipokea majeruhi 12 na kukanusha kutokea kwa kifo kwenye tukio hilo.

“Ni kweli tumepokea majeruhi 12 hapa, lakini waliolazwa hadi sasa ni tisa, kati yao wanawake wawili na wanaume ni saba." Wagonjwa hao wanaonekana wamejeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya miili yao hata hivyo siwezi kuthibitisha kama ni risasi maana hadi tuzitoe mwilini,’’alisema Mzee.

Akizungumza kwa tabu katika wodi namba moja mmoja wa majeruhi hao aliyejitambulisha kwa jina la Mukoro Maro, alisema alikatwa mapanga na mabaunsa wakati akijaribu kukoa familia yake.

“Polisi walinikamata na kunipeleka kwa vijana waliovaa kofia za kuficha nyuso ambao walinishambulia kwa mapanga na kunipora simu yangu, alisema Maro huku akiwa amelowa damu kutokana na majeraha makubwa kichwani.
Kwa upande wake Yohana Charles, alisema kuwa yeye alistukia kitu cha moto katika paja la mguu wake wa kushoto wakati akienda kumsaidia mzee aliyekuwa anapigwa na polisi ghafla alianguka chini na kupoteza fahamu baadaye alijikuta hospitalini na kugundua kuwa amepigwa risasi.

Ulinzi hospitalini
Eneo la Hospitali ya Mkoa wa Dodoma lilikuwa na ulinzi mkali, polisi wakiwa wametanda kila kona na silaha za moto hali iliyowatisha watu wengi waliokuwa wakienda hapo kusalimia wagonjwa wao.

Saturday, October 22, 2011

Ujenzi Wa Barabara Ya Singida-Katesh(Manyara), Wakamilika

Mkuu wa mkoa Dk.Kone, (kushoto) ba mhandisi Kkangolle(kulia),na wakandarasi wa wa ujenzi wa barabara hiyo iliyoigharimu serikali zaidi ya Sh.Bilioni 51.6, ambao umekamilika na magari yataruhusiwa kuanza kupita katika kipindi cha siku saba kuanzia leo.

Mkuu wa mkoa Dk.Kone, akipewa maelekezo na mhandisi Kangole, juu ya mawe mawili katika barabara hiyo, ambayo ni lango la kuingia na kutoka katika mji wa Singida

Mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone(katikati), meneja wa wakala wa barabara Singida,mhandisi Yustak Kangole, wakiwa kwenye picha ya pamoja na wataalamu wa kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd ya China, baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Singida-Kateshi(Manyara) kilomita 65.1

Mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone baada ya kukagua mradi wa barabara ya Manyoni-Chaya, jana aliendelea na kazi hiyo, kwa kufanya ukaguzi barabara ya Singida-Kateshi(Manyara) inayojengwa na kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd, kwa zaidi ya Sh.Bilioni 51.6.

Mkuu Wa Mkoa Wa Singida Akagua Ujenzi Wa Barabara Manyoni-Ch​aya(Tabora​)

Barabara hii ya Manyoni-Chaya(Tabora), ikijengwa kwa kasi,moja ya lori likionekana likimwaga mchanga kwenye barabara hiyo inayoigharimu serikali zaidi ya Sh.Bilioni 109.6, mradi huu unajengwa na kampuni ya Sinohydro,kutoka nchini China, wakati mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone alipotembelea kujionea maendeleo yake

:Mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone mwenye kofia ya bluu, akitaka ufafanuzi kwa mhandisi mshauri wa mradi wa barabara hiyo, kampuni ya Nicolous Odoya ya nchini Island,Bw. Patrick Gayer.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone akionyeshwa moja ya karo yanayotumika kuhifadhia maji kabla ya kutumiwa kwenye shughuli za ujenzi wa barabara hiyo yenye umbali wa kilomita 89.3, kutoka Manyoni(Singida) hadi Chaya(Tabora)

MKUU wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone ameyataka makampuni yanayojishughulisha na kandarasi za ujenzi wa barabara, kukamilisha mapema miradi yao, ili kuendana sawa na mikataba wanayoingia na serikali.Dk.Kone ameyasema hayo leo, wakati akikagua mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya Manyoni(Singida) hadi Chaya mkoani Tabora, kilomita 89.3, unaotekelezwa na kampuni ya SINOHYDRO,kutoka nchini China, kwa gharama ya zaidi ya Sh.Bilioni 109.6.
Hata hivyo aliipongeza kampuni hiyo kwa msingi wa barabara ambao mradi huo upo mbele kwa siku 53, lakini ameitaka kuchukua tahadhari wakati wa masika ambapo mvua huadhiri maendeleo ya ujenzi

Singida Kuzalisha Umeme Wa Upepo


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Power Pool East Africa, Machwa Kagoswe akitoa maelezo kwa Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu juu ya eneo la kuzalishia umeme wa upepo mkoani Singida . Serikali imeingia Ubia kupitia Shiriaka la Maendeleo la Taifa (NDC) na kampuni binafsi ya Power Pool East Aftrica ili kuzalisha umeme huo kuanzia mwakani.

Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) limeingia ubia na kampuni ya Power Pool East Africa wa kuzalisha umeme wa upepo mkoani Singida utakaogharimu takribani ya Sh Bilioni 180.

Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu alisema tayari makubaliano yamesainiwa na shirika la NDC kwa niaba ya serikali itakuwa ikimiliki asilimia 51 za hisa na nyingine zitakuwa za mwekezaji binafsi.

Nyalandu alisema kwa mradi huo ambao utakuwa wa gharama nafuu katika uzalishaji utaingizwa katika gridi ya taifa na kwa kuanzia zitazalishwa megawati 50 na baadae zitaongezwa kulingana na uwezo wa wabia hao.

“Tokea kuanza kufungwa kwa mitambo itachukua takribani miezi 15 ili umeme uingie katika gridi na hii itakuwa ufumbuzi wa matatizo ya umeme kwa sasa” alisema Nyalandu.

Mkurugenzi wa Viwanda vikubwa wa NDC, Alley Mwakibolwa alieleza kuwa kwa ujenzi wa mitambo hiyo ya kutumia upepo kutasaidia kuzalisha umeme ampema kwani mitambo ya aina hiyo huchukua muda mfupi kuwekwa ikilinganishwa na ya maji ama ya gesi.

Tutajitahidi mradi huu uende kwa kasi kubwa kwani kwa kuanzia tutazalisha megawati 50 na baadae tutaongeza 50 ili kuoingia katika gridi ya taifa" alisema.

Aidha katikaeneo hilo ambalo liko ukingoni kwa bonde la ufa, upepo ni mkakli kiasi cha kufanya miti karibu yote kulalia upande mmoja na upeo huende kwa kasi ya hadi mita 21 kwa sekunde.

Friday, October 21, 2011

MWISHO WA KANALI GADAFFI


ALIYEKUWA kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi ameripotiwa kuuawa na wapiganaji wanaoongozwa na Baraza la Mpito nchini humo (NTC), baada ya mji wa nyumbani kwake, Sirte kunyakuliwa na vikosi hivyo jana.

Kifo cha Kanali Gaddafi (69) kilitangazwa rasmi na Waziri Mkuu wa Serikali ya mpito nchini humo, Mahmoud Jibril, muda mfupi baada kiongozi huyo aliyeitawala Libya kwa miaka 42 kuuawa.

Awali, msemaji wa NTC nchini Libya, Kanali Ahmed Bani alisema Kanali Gaddafi aliuawa na mwili wake ulipelekwa katika mji wa Misratah, bila kutoa ufafanuzi kamili kuhusu mazingira ya kifo hicho.

Taarifa za kuuawa kwake zilitolewa huku zikiambatanishwa na picha zinazoonyesha sura inayoonekana kuwa ni ya kiongozi huyo, katika muonekano wa nywele zake laini na ndefu wastani na uso uliotapakaa damu na majeraha.

Kanali Gaddafi anakuwa kiongozi wa kwanza kuuawa tangu kuanza vuguvugu la mageuzi katika mataifa ya kiarabu mwanzoni mwa mwaka huu, yaliyowaondoa madarakani Rais Ben Ali wa Tunisia na Hosni Mubarak wa Misri.

Kifo hicho kimetangazwa ikiwa ni miezi tisa tangu kuanza kwa upinzani mkali dhidi ya Serikali yake Februari mwaka huu, ambapo aliapa kwamba asingeondoka nchini Libya na kwamba yeye na wafuasi wake wangepambana hadi tone la mwisho la damu.

Kanali Gaddafi ambaye wakati wa utawala wake aliwahi kujipa wadhifa wa “mfalme wa wafalme wa Afrika” alikuwa akisifika kwa ukali wa sauti yake na maneno makali ya kuhamasisha na kueleza misimamo yake katika hotuba zake.

Mapambano hayo yameishia katika mji wa nyumbani kwake, Sirte ambao umekuwa na upinzani mkali kwa vikosi vya wapiganaji wa NTC ambavyo vililazimika kupambana kwa miezi kadhaa hadi waasi walipofanikiwa kuuteka jana.

Kanali Bani alisema mtoto wa Kanali Gaddafi, Mutassim ambaye walikuwa pamoja katika mji wa Sirte aliuawa na wapiganaji hao wa NTC.

Msemaji huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa kiongozi huyo alifariki dunia baada ya kujeruhiwa vibaya katika miguu yake yote na kichwani.

“Aliuawa katika mapambano na wapiganaji wetu. Kuna picha zinazoonyesha hayo,”alisema.

Alijificha kwenye karavati

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, Kanali Gaddafi alidhibitiwa baada ya kukutwa amejificha katika karavati la barabarani, yeye pamoja na baadhi ya walinzi wake.

Kwa upande wake, kamanda wa wapiganaji wa baraza hilo, Abdul Hakim Belhaj pia alithibitisha kuwa Kanali Gaddafi alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kukamatwa.

Makamu Mwenyekiti wa NTC, Abdul Hafiz Ghoga alithibitisha mbele ya waandishi wa habari kuwa Gaddafi aliuawa katika mji wa Sirte.

“Tunatangaza kwa dunia kuwa Muammar Gaddafi aliuawa katika mikono ya wanamapinduzi,” alisema Ghoga.

Katika mtiririko wa matukio yaliyokuwa yakirushwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, kituo cha televisheni cha al-Jazeera kilionyesha picha za mwili wa Kanali Gaddafi ukiburuzwa katika eneo alilouawa.

Filamu za video zilizochukuliwa kwa simu za mkono zilionyesha kile kilichoonekana kuwa maiti ya Gaddafi iliyolowa damu. Mwili wake baadaye uliburuzwa na wapiganaji na kupakiwa nyuma ya gari aina ya pick-up.


Nato na Marekani zilieleza kuwa haziwezi kuthibitisha taarifa za kuuwawa kwa kiongozi huyo ambaye hajaonekana tangu NTC ilipoikamata Tripoli.

Watu washangilia mitaani

Wakati huohuo, katika mji wa Benghazi na miji mingine nchini humo, watu walionekana kukusanyika mitaani na kushangilia taarifa hizo za kuuawa kwa Gaddafi.

Viongozi mbalimbali duniani pia wamezungumzia kuhusu taarifa hizo za kuuawa kwa Kanali Gaddafi ambaye amewahi kuwa mpinzani mkubwa wa mataifa ya Ulaya na Marekani kutokana na misimamo yake dhidi ya mataifa hayo.

Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon ambaye alisema ni siku maalum ya kukumbuka maovu yote yaliyofanywa na Gaddafi.

Alisema watu wa Libya wako katika nafasi nzuri ya kujenga nchi imara na yenye demokrasia.

“Ninafurahi kazi ambayo Uingereza imesaidia katika kuuondoa utawala wa Gaddafi,”alisema.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain Juppe amepongeza kufikiwa mwisho kwa utawala wa miaka 42 ya Gaddafi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon pia alisema kwamba kifo cha Kanali Gaddafi kinatoa mwanya wa “historia mpya kwa Libya”.

“Watu wanatakiwa watambue kuwa huu ni mwisho wa mwanzo. Sasa ni wakati wa Walibya wote kushikamana na kuwa kitu kimoja. Ni wakati wa kuponya majeraha na kujenga upya taifa. Si wakati wa visasi,” alisema Ki-Moon.

Balozi wa Libya nchini Uingereza, Mahmud Nacua alisema kuwa kuawa kwa Gaddafi kunamaanisha Libya inaelekea kwenye mustakhabali bora wa baadaye.

Wasifu wa Kanali Muammar Gaddafi

Alikuwa mtoto wa wafugaji wa Kibedui, mwenye maisha ya utata, lakini ambaye alitukuzwa sana, huku mataifa ya Magharibi yakimuona mtu wa hatari wakati wote.

Muammar Muhammad Gaddafi aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 40. Hadi mwanzoni mwa Machi 2011, alikuwa akiamini ndani ya moyo wake kwamba watu wake walikuwa wakimpenda na kwamba walikuwa tayari kumlinda hadi kufa kwa ajili yake.

Lakini wakati huo, tayari Gaddafi alikuwa ameshatumia njia za kikatili kuyazima maandamano dhidi yake, maandamano ambayo baadaye yaligeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mujibu wa taarifa, watu zaidi ya 30,000 waliuawa kwenye vita hivyo. Mara nyingi sana, Gaddafi alitoa matamko makali wakati wa vita hivyo, ila linalojuilikana zaidi ni lile la kuwaita wapinzani wake kuwa ni panya.

Kwa kila hali, yaliyotokea ni mambo ambayo Gaddafi hakuyatarajia asilani. Mtoto huyu wa wafugaji wa Kibedui aliyezaliwa mwaka 1942, alikuja kuibuka kama mkombozi wa Walibya, alipompindua Mfalme Idriss hapo mwaka 1969.

Kuanzia hapo akaanza kujenga kile alichokiona mwenyewe kuwa ni mfumo wa kidemokrasia wa moja kwa moja. Alianzisha kamati za umma zilizoamua juu ya mustakabali wa umma na wa Serikali. Aliuita mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi kuwa ni wa kisoshalisti, alioufafanua kwenye kijitabu chake cha Kijani.

Historia yake kiufupi

Alizaliwa mwaka 1942 katika eneo la Jangwa, kwenye mji wa Sirte, katika familia ya baba Mohamed Abdulsalama Abuminiar na mama Aisha Ben Niran. Alijiunga na Jeshi la Libya mwaka 1965.
Alifanya mapinduzi ya Serikali yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa mfalme Idris katika utawala wake mwaka 1969 na kuwa mtawala wa Libya akiwa na umri wa miaka 27.

Alikuwa maarufu kwa nguo anazopenda kuvaa na walinzi wa kike wenye kubeba silaha, kiongozi huyo wa Libya pia anadhaniwa kuwa na mbinu nzuri za kisiasa kwa kuweza kuirejesha Libya kutokana na kutengwa kidiplomasia duniani.

Baada ya miongo miwili ya kutengwa katika jamii ya kimataifa, mwaka 2003, Tripoli ilikiri kuwa walifanya shambulio la Lockerbie kwa kuiangamiza kwa mabomu ndege ya Pam Am. Umoja wa Mataifa (UN) ulikubali kuondoa vikwazo dhidi ya Libya.



Baada ya miezi kadhaa, Serikali ya Kanali Gaddafi ilisitisha mipango yake ya kuunda silaha za maangamizi na hii ikarejesha ushirikiano na nchi za Magharibi.

Gaddafi ni mtu wa kipekee katika kauli zake, mienendo yake, tabia zake na mikakati yake, kwa mujibu wa Saas Djebbar, mtaalam wa siasa za Libya.
Alipokuwa kijana alivutiwa na kiongozi mzalendo wa Misri, Gamal Abdel Nasser, alipokuwa akishiriki katika maandamano dhidi ya Israel wakati wa mtafaruku wa Suez mwaka 1956.

Alipanga njama ya kupindua utawala wa kifalme alipokuwa mwanafunzi wa kijeshi alipokuwa mafunzoni Uingereza kabla ya kurejea nyumbani Libya. Alipanga mapinduzi ya Septemba 1, 1969 akiwa katika mji wa Benghazi.

Alianza kujenga itikadi zake za kisiasa mwaka 1970 na kuziandika katika kitabu chake cha kijani kibichi.
Alikitumia kitabu chake kuanzisha mfumo wa kisiasa uliojumuisha kanuni za Kiislamu na mfumo ulio tofauti na siasa za ujamaa au ubepari.

Mwaka1977 aliasisi mfumo ujulikanao kama 'Jamahiriya' au 'Taifa la Umma' ambapo raia ndio wanaoendesha uongozi wa nchi yao kupitia 'kamati za umma'.

Mfumo huo wa Gaddafi umevuka mipaka na hauhusishi mambo ya siasa tu, bali pia mambo mengine.
Akiwa safarini ng'ambo, alikuwa akitumia makazi maalum kwenye kambi iliyojengwa na hema yake ya kifahari ya Kibeduwi akiwa amefuatana na walinzi wanawake ambao, inasemekana, huwa hawapotezi umakini kazini kama walinzi wanaume.Hema hiyo pia ilitumiwa kuwalaki wageni wa Libya na Kanali Gaddafi huendesha mikutano na mahojiano yake humo humo akipepea usinga au tawi la mitende.

Rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alimwita Gaddafi 'mad dog' yaani 'mbwa kichaa' na Marekani ililipiza kisasi dhidi ya Libya kwa madai ya kuhusika na mashambulio ya anga barani Ulaya kwa kuvamia miji ya Tripoli na Benghazi mwaka 1986.Aliposhindwa katika jitihada zake za kuzipatanisha nchi za Uarabuni katika miaka ya 90, Kanali Gaddafi alielekeza nguvu zake barani Afrika na kupendekeza 'Muungano wa Nchi' za bara la Afrika.

Alianza kuvaa mavazi yake binafsi, sare za michezo zilizo na ngao za Bara la Afrika au picha za viongozi kutoka bara hilo.Aliwahi kuvunja na kufuta Wizara za nchi hiyo pamoja na bajeti zao, isipokuwa Wizara chache ikiwemo ya Ulinzi, Fedha na Mambo ya Nje.Licha ya uchumi wa Libya kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje, mabadiliko bado yanakwenda taratibu.

Vuguvugu la mageuzi dhidi yake lilipoanza mwanzoni mwa mwaka huu, aliapa kuwafuata wanaompinga nyumba hadi nyumba, mlango kwa mlango, hatua iliyoibua hasira na kuchochea harakati za kijeshi dhidi yake.

Baada ya baadhi ya askari kutangaza kujitoa katika jeshi lake na kuanzisha uasi, aliapa kwamba atapambana hadi tone la mwisho la damu litakapomwagika. Alisisitiza kwamba kamwe hatakimbia kutoka katika ardhi ya Libya, atafia katika ardhi ya mababu zake.

Taarifa zilieleza jana kwamba aliuawa baada ya kukutwa akiwa amejificha katika daraja dogo kwa ajili ya kupitisha maji barabarani (karavati).

Mara baada ya kuuawa, wapiganaji wa Baraza la Mpito waliokuwa katika mapambano dhidi yake walibaini kwamba alikuwa na bastola iliyotengenezwa kwa dhahabu tupu.

JK aahidi kukiboresha UDSM


SERIKALI imeahidi kukiboresha Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na makazi ya wafanyakazi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.Uboreshwaji huo utakuwa ni pamoja na ujenzi wa hosteli katika kampasi kuu itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 4,500 na nyumba 450 za watumishi wa chuo hicho.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyokwenda sambamba na sherehe za mahafali ya 41 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, Rais Jakaya Kikwete alisema uamuzi huo ni moja ya mipango ya Serikali kuboresha vyuo vikuu nchini.

Rais Kikwete ambaye aliambatana na Rais Yoweri Museveni ambaye aliwahi kusoma chuoni hapo miaka ya nyuma, alisema "nimeambiwa hali ya makazi ni mbaya inayohitaji hatua za haraka. Tutaliangalia hilo".

Kwa mujibu wa Rais, "Serikali pia itakisaidia chuo kutekeleza mpango wake wa ujenzi wa nyumba 450 kwa ajili ya watumishi wake".

Alisema serikali pia inakaribisha na itasaidia ujenzi wa kituo cha wanafunzi kwa ajili ya kujisomea na kuongeza, " Kama nyote mnavyojua, mimi na kaka yangu Rais Museveni tumeshiriki katika juhudi mbalimbali kufanikisha fedha za mradi huo".


Mpango wa elimu ya juu
Akizungumzia Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Juu (HEDP), Rais Kikwete alisema umeandaliwa kwa kipindi cha miaka mitano kutoka 2010 hadi 2015 na kila mwaka utakuwa ukigharimu Serikali Sh52bilioni.

Alisema HEDP una malengo makuu matano ambayo ni pamoja na kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi, kujenga miundo mbinu iliyopo na kujenga mipya, kutoa vifaa vya kufundishia na kujisomea ambavyo ni pamoja na vitabu na kompyuta.

Lengo jingine alilotaja Rais, ni pamoja na matumizi ya teknoloji ya kisasa ya Mawasiliano kwa Kompyuta (ICT) na kufanya tafiti na uwezeshaji wake.

Alisema ni dhamira ya Serikali kuona sekta binafsi inashiriki vema katika kujenga vyuo vikuu zaidi katika nchi na kuongeza kwamba, "tutaendelea kupanua wigo wa upatikanaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu".

Kwa mujibu wa Rais, mwaka 2005/06 mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni Sh56.1 bilioni lakini hadi kufikia mwaka huu mikopo hiyo imeongezeka na kufikia kiasi cha Sh317.9 bilioni na kusisitiza, "hii inatuwezesha kuongeza namba ya wanafunzi wanaopata udhamini wa Serikali kupata mikopo kutoka 16,345 kati ya mwaka 2005/06 hadi kufikia 93,105 mwaka huu".

Rais alizidi kujivunia mafanikio akisema, idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakaopata mikopo kwa mwaka huu ambayo ni 24,625 ni kubwa ya idadi jumla ya wanafunzi wote wa vyuo vikuu kwa mwaka 2005

Alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka 42,948 mwaka 2004 hadi 95,525 mwaka 2009.

Museveni
Katika hatua nyingine Rais wa Uganda, Yoweri Mseveni aliwapongeza waanzilishi wa chuo hicho na kusema,
“Tanzania inastahili pongezi nyingi sana, kwani Mwanasheria Mkuu wa nchi yangu hajasoma Uingereza wala India bali ni matunda ya Chuo hiki,”.

Alisema yeye pia ni matunda ya chuo hicho na bado kinaendelea kuisaidia Uganda kwa kupokea wanafunzi wake.

“Sisi na watanzani wote tunapaswa kujivunia UDSM na tuhakikishe kinaendelea kwani katika miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania kimekuwa ni msaada kwa maendeleo ya nchi mbalimbali” alisema Rais huyo mwenye kupenda kuvaa kofia pana.

MADUKA MANNE YAUNGUA MOTO MJINI SINGIDA



Dogo akiwa kwenye hekaheka


Picha zote tatu zikionyesha jinsi maduka yalivyokua yakiteketea kwa moto
Watu wakiwa katika harakati za kuokoa vitu vyoa

Gari la zima moto likifanya kazi yake

Hali hilivyokua baada ya moto kuzimwa nusu na kikosi cha zima moto.
Hakuna mtu aliyepoteza maisha au kujeruhiwa

EPIC NATION NDANI YA SINGIDA

GARI LA MADEE NA DOGO JANJA LIKIINGIA NAMFUA HUKU LIKISINDIKIZWA NA WASHABIKI WAO

WANA WENGINE WAKISINDIKIZA SHANGWE ZA EPIC NATION NDANI YA SINGIDA

MADEE NA DOGO JANJA WALIPO PANDA STAGENI




WAKAZI MBALIMBALI WA SINGIDA WAKISHUHUDIA SHAGWE ZA EPIC NATION


MADEE NA DOGO JANJA WALIVYO ZONGWA BAADA YA KUSHUKA STAGENI
KWA MBALI NI GARI LA MADEE NA DOGO JANJA LIKIKIMBIZWA NA MASHABIKI WAO LILIPOKUWA LIKIONDIKA