Friday, November 23, 2012

ALIYEMUIBIA HAKIMU SINGIDA AHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA MITATU.


                               Jengo la mahakama ya mwanzo Utemini mjini Singida.

Mlinzi wa kibanda cha biashara cha hakimu wa mahakama ya mwanzo Ipembe mjini Singida Jumanne Juma (47), amehukumiwa kutumikia jela jumla ya miaka minne na miezi sita, baada ya kukiri kutenda makosa matatu likiwemo la kuvunja kibanda cha mwajiri wake kwa lengo la kufanya uhalifu.
Mlinzi Jumanne anatuhumiwa kutenda makosa hayo,Novemba 3 mwaka huu saa tano usiku eneo la Utemini mjini Singida.
Mshitakiwa Jumanne ambaye
ni mlemavu wa jicho moja la kushoto (chogo), aliajiriwa na hakimu Hossea Selema Mkude (58) wa mahakama ya mwanzo Ipembe.
Katika shitaka la kwanza, mshitakiwa alisomewa kuwa mnamo Novemba 23 mwaka huu saa tano usiku huko Utemini, mshitakiwa bila halali, alivunja kibanda cha mwajiri wake kwa nia la kutenda kosa la jinai.
Shitaka la pili, mshitakiwa Jumanne alisomewa kuwa katika siku ile ile na wakati huo huo ,aliiba mizani ya kupimia uzito na vocha mbalimbali za simu za viganjani, vyote thamani yake ni shilingi laki tano (500,000).
Aidha, ilidaiwa kuwa mshitakiwa akiwa mwajiriwa wa hakimu Mkude, alipuuza na hivyo akishindwa kuzuia kosa la wizi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Mshitakiwa baada ya kusomewa mashitaka yake hayo, bila kuuma uma mdomo, alikiri kutenda makosa hayo.
“Kwa hiyo, naiomba mahakama yako tukufu, inionee huruma kwa vile sijasumbua kabisa nimenyoosha maelezo yangu moja kwa moja, pia nipo tayari kumlipa Mheshimiwa wangu Mkude sh.500,000 anazodai kuibiwa”, alisema mshitakiwa Jumanne huku akiinamisha kichwa chake chini.
Kwa upande wake hakimu wa mahakama ya Utemini Ferdnard Njau, alisema pamoja na maombi ya mshitakiwa, mahakama ipo pamoja na mambo mengine, kurekebisha tabia mbaya zinazofanywa na baadhi ya watu.
”Kwa kosa la kwanza, utatumikia jela miaka mitatu, kosa la pili, miezi 12 na kosa la tatu, miezi sita. Adhabu zote zitakwenda pamoja na hivyo utatumikia jela miaka mitatu tu”,alisema hakimu Njau.

No comments:

Post a Comment