Wednesday, November 21, 2012

ANUSURIKA KUFA BAADA YA TFDA KUKAMATA BIDHAA ZISIZO SALAMA DUKANI KWAKE.

 Kaimu meneja wa mamlaka ya chakula na dawa kanda ya kati(TFDA), Aberl Deule akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya zoezi la kukagua bidhaa katika maduka ya wilaya ya Manyoni.
 Moto ukiwa umewaka kuteketeza bidhaa zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tano ambazo ni sumu na zile ambazo muda wake wa kutumika umekwisha.Bidhaa hizo zilikamatwa na TFDA katika baadhi ya maduka ya wilaya ya Manyoni.
 Bidhaa ambazo zina sumu na zilizokwisha muda wake zilizokamatwa na TFDA kabla hazijateketezwa kwa moto.
Kaimu meneja wa TFDA kanda ya kati, Aberl Deule (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo kwa muuza duka wa Manyoni mjini.


Mamlaka ya Chakula na Dawa Kanda ya Kati (TFDA) imeteketeza bidhaa mbali mbali zenye thamnai ya zaidi ya shilingi milioni tano zikiwemo zile ambazo muda wake wa kutumika umeisha.
Bidhaa hizo ni pamoja na soda, juice, biskuti (muda wake wa kutumika uliishapita) na maziwa ya unga ya watoto wadogo aina ya Lactogen (18 na 2) ambayo ni bandia.
Bidhaa zingie zilizoteketezwa ni tani moja ya vipodozi hatari kwa matumizi ya binadamu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tatu.
Vipodozi hivyo vyenye kemikali za hydroquinone na zebaki, hutumiwa kubadilisha rangi ya ngozi (kujichubua).
Akizungumza muda mfupi baada ya kuteketeza bidhaa hizo, Kaimu Meneja TFDA Kanda ya Kati Aberl Deule, amesema msako wa ukaguzi wa kuangalia ubora na usalama wa chakula, dawa na vipodozi, ulianza Novemba 13 hadi 17 wilayani Manyoni.
Amesema msako huo ambao ni endelevu, ulifanyika katika maeneo 52 ya Manyoni mjini na Itigi, ambayo ni pamoja na viwanda vya kutengeneza vyakula, kuuzia vyakula, maduka ya vipodozi, maduka ya dawa za binadamu na yale ya dawa za mifugo.
Katika hatua nyingine, Kaimu Meneja huyo amewataka wananchi kuhakikisha wanatumia bidhaa ambao hazijaisha muda wake na zile ambazo  hazina sumu.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Deule amewataka muda wote wahakikishe wanampatia mteja bidhaa zenye ubora, zisizokuwa na sumu na zile ambazo muda wake wa kutumika, haujaisha.
Amesema “Wafanyabiashara mnaojishughulisha na biashara za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, hakikisheni majengo yenu yanasajiliwa na TFDA.  Hakikisheni pia  bidhaa, mnazozalisha au kuuza ni salama kwa afya ya binadamu na bora”.
Deule amewataka wajenge utamaduni wa  kukagua bidhaa zao ili kubaini kama kuna bidhaa zilizopitwa muda wa matumizi na wajiepushe kuuza vipodozi vyenye viambato vya sumu.
Imedaiwa kuwa mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina moja la Anord wa Manyoni mjini,  amelazwa katika hospitali  ya wilaya, muda mfupi baada ya shehena ya biadhaa zisizokuwa salama kwa matumizi ya binadamu, kuamatwa dukani kwake.

No comments:

Post a Comment