Thursday, November 15, 2012

UHABA WA NYUMBA NA UPUNGUFU WA WALIMU WA SAYANSI KIKWAZO KIKUBWA KWA ELIMU KATA IPEMBE MKOANI SINGIDA

Kata ya Ipembe jimbo la Singida mjini inakabiliwa na uhaba mkubwa wa nyumba za kuishi walimu zipatazo 72 katika shule zake tatu ikiwemo moja ya sekondari.
Akitoa taarifa yake ya utekelezaji mbele ya  kikao cha baraza la madiwani wa manispaa ya Singida, diwani wa kata hiyo Twalib Kihara amesema shule ya msingi Ipembe inakabiliwa na upungufu wa nyumba za kuishi walimu 23, wakati shule ya  msingi Sumaye, pia ina upungufu wa nyumba 20.
Kihara amesema shule pekee ya sekondari ya kata hiyo, inahitaji nyumba za kuishi walimu 30, kwa sasa ina nyumba moja tu, na hivyo inakabiliwa na upungufu wa nyumba 29.
Katika hatua nyingine, Kihara ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi katika shule ya sekondari Ipembe.
Diwani huyo mkongwe,alitaja changamoto zingine kuwa ni uhaba wa vitendea kazi na mwitikio mdogo wa jamii katika uchangiaji wa maendeleo.
Kwa mujibu wa diwani Kihara Kata ya Ipembe ni miongoni mwa kata 16 za manispaa na ina wakazi wapatao 2,833 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002.

1 comment:

  1. Ndugu nashukuru kwa habari zako nzuri tunazopata katika blog yako hii nzuri, lakini ninachoomba kwako picha za SGD mjini ili hata mtu akipitia blog hii aione SGD yetu na sisi wa ughaibuni tuione tufurahi kidogo.

    ReplyDelete