Saturday, December 8, 2012

Kampuni ya Tan Discovery yakanusha kutowasaidia wachimbaji wadogo wa madini mkoani Singida.

Afisa msimamizi wa kampuni ya Tan Discovery Akida Sungura akiwa Internet Cafe akitekeleza majukumu yake.


Kampuni ya Tan Discovery inayojishughulisha na kuuza na kukodisha vifaa vya uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo mkoani Singida, imekanusha taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba haijawasaidia wachimbaji kufikia
malengo yao.
Msimamizi wa kituo cha Tan Discovery mkoani Singida Akida Sungura, amesema taarifa hizo hazina ukweli wo wote kwani kampuni toka imefungua kituo katika kijiji cha London wilaya ya Manyoni, imeuza kwa bei nafuu vifaa vingi kwa lengo la kuwaendeleza wachimbaji wadogo.
Amesema pia kituo hicho kimekodisha na kinaendelea kukodisha vifaa mbalimbali kwa wachimbaji wadogo kwa gharama ndogo kadri ya mahitaji yao.
Amesema Kampuni hiyo pamoja na kuuza na kukodisha vifaa kwa wachimbaji wadogo, pia imeweza kuleta wataalam wa madini kutoka Dodoma na wakatoa mafunzo ya kina kwa wachimbaji, lengo likiwa ni kupanua uwezo wao kuhusu uchimbaji na kubaini miamba yenye dhahabu.
Aidha, msimamizi huyo amesema gharama za kuuza na kukodisha vifaa walivyonavyo, sio kubwa kama inavyodaiwa na wachimbaji wadogo wa mkoa wa Singida.
“Mimi nitoe wito tu kwa ndugu zangu wachimbaji wadogo, kwamba kazi ya uchimbaji madini, ni kazi nzito na ni ya gharama kubwa.Si rahisi kwa mchimbaji mmoja mmoja kuimudu”alifafanua Sungura.
Amesema dawa pekee ya wachimbaji wadogo kumudu kazi ya uchimbaji ni kujiunga kwenye vikundi ili kuwa na nguvu ya kutosha na wakati huo huo, kujijengea mazingira mazuri ya kuweza kukopesheka na taasisi za kifedha.
Katika hatua nyingine, Sungura pia amekanusha taarifa kwamba kampuni yao imekopeshwa na serikali zaidi ya shilingi bilioni nane.
Msimamizi huyo amesisitiza kuwa Serikali haijatupa shilingi bilioni nane, imetupa shilingi milioni 180 tu hadi sasa. Baadaye inatarajia kutuongeza shilingi milioni 20. Kwa ujumla shilingi milioni 200 ni fedha chache mno kwenye shughuli ya madin.
Sungura amesema serikali itakapoongeza kiwango kizuri zaidi cha fedha kwa maana ya kutosheleza mahitaji, kampuni ya Tan Discovery, nayo itajitahidi kukidhi mahitaji ya wachimbaji wote wadogo wa mkoa wa Singida.
Katika risala ya hivi karibuni ya chama cha watafiti na wachimbaji madini mkoa wa Singida (SIREMA), imedai kwamba kampuni ya Tan Discovery, gharama zake za kukodisha na kuuza vifaa ni kubwa mno na wachimbaji wadogo hawawezi kuimudu.

No comments:

Post a Comment