Tuesday, December 18, 2012

Kesi ya Vigogo wa CHADEMA wanaodaiwa kumtukana Mbunge wa Iramba yaendelea kupigwa danadana yaahirishwa hadi leo.

 Vigogo wa CHADEMA Dkt. Kitila Mkumbo mshauri wa CHADEMA na mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar-es-salaam (kulia) katibu wa sera na utafiti wa CHADEMA makao makuu Mwita Waitara (katikati) na Pela Ngunangwa aliyejitambulisha kuwa ni dereva kiongozi ofisi za CHADEMA makao makuu, wakiwa wanaelekea kuingia kwenye mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida.
Wakili wa vigogo wa CHADEMA Raymond Kimu (wa kwanza kushoto aliyenyoosha kidole) akiteta na wateja wake Mwita Waitara (katikati) na wa pili kulia mwenye miwani Dk.Kitila Mkumbo.

 Kesi inayowakabili vigogo wa CHADEMA ya kumtolea lugha ya matusi mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi  (CCM) Mwigulu Lameck Nchemba, iliyoanza kusikilizwa jana kwenye mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida imeahirishwa hadi leo.  
Kesi hiyo imeahirishwa baada ya kukosekana kwa hati za
maelezo ya awali yalioandikwa polisi na mashahidi wa upande wa mashitaka.
Vigogo wanaokabiliwa na kesi hiyo ni katibu wa Sera na Utafiti wa CHADEMA Makao Makuu Mwita Waitara  na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na Mshauri wa CHADEMA Dkt. Kitila Mkumbo.
Baada ya shahidi wa pili Lyanga Elikana kuanza kutoa ushahidi wake huku akiongozwa na mwendesha mashitaka mkaguzi msaidizi wa polisi Shukrani Magafu, wakili wa upande wa washitakiwa Tundu Lissu, alisimama na kuomba maelezo ya shahidi aliyoyaandika polisi awali.
Mwendesha mashitaka Magafu, alisema kuwa kwa wakati huo hana hayo maelezo na kuiomba mahakama iliyokuwa chini ya hakimu  Ruth  Massamu, kuahirisha kesi hiyo hadi leo atakapoleta  maelezo ya shahidi Lyanga pamoja na mashahidi wengine wanne waliobakia.
Mahakama ilikubaliana na ombi hilo ambalo pia upande wa utetezi ulikubaliana.
Awali  shahidi Lyanga alihojiwa na Tundu Lissu kama ilifuatavyo; shahidi,je ni kweli mshitakiwa wa kwanza Waitara, aliuliza wananchi waliokuwa wamehudhuria mkutano wa hadhara kama wanamfahamu ‘the comedy’ wa jimbo la Iramba magharibi?
Shahidi Lyanga alijibu “ni kweli  Waitara aliuliza swali hilo ambalo lilijibiwa na wananchi kuwa ‘ndio’ wanamfahamu.
Tundu, hebu mweleze mheshimiwa hakimu na wasikilizaji wa kesi hii, wananchi walijibu kuwa ni nani huyo ‘the comedy’.
Shahidi Lyanga alijibu kuwa wananchi  walimjibu Waitara kuwa ‘the comedy’huyo ni Mwigullu Nchemba.
Tundu aliuliza tena kuwa watu wanaofanya vichekesho yaani the comedy kama akina Masaja, je sanaa hiyo inakashifu au inatukana watu.
Shahidi Lyanga, sio kashifa ila ikitumiwa vibaya, inakuwa kashifa na matusi.
Aidha shahidi Lyanga aliiambia mahakama hiyo kuwa matusi yaliyotolewa na mshitakiwa Waitara kuwa mbunge wa jimbo la Iramba magharibi Mwigulu, ni mzizi, Malaya, mpumbavu na fisadi, yalirudiwa kutamkwa na mshitakiwa wa pili ambaye ni Dk.Kitila Mkumbo.
Washitakiwa hao wadaiwa kutenda kosa hilo Julai 14 mwaka huu katika kijiji cha Nguvumali kata ya Ndago jimbo la Iramba magharibi.
Washitakiwa hao wanatetewa na wakili Tundu Lissu, Onesmo Kyaule (mkazi wa jijini Dar-es-salaam ) na Raymond Kimu wa Singida mjini.

No comments:

Post a Comment