Sunday, December 16, 2012

TFDA yakamata bidhaa zilizomaliza muda wake Mkoani Singida.

 Maafisa TFDA kanda ya kati, Florent Kyombo (kushoto) akishuhudia mmiliki wa duka la Temba, Singida mjini Bw. Temba akisaini fomu yakutekeza bidhaa zilizoisha muda wake na akazitoa dukani, TFDA walimsifu sana.
Kaimu meneja TFDA kanda kati, Florent Kyombo na Joseph Mwasambili wakikagua vinywaji vikali kwenye moja ya duka mjini Singida, katika oparesheni maalumu kusaka bidhaa zilizomaliza muda kwa matumizi ya binadamu.

 Mamlaka ya chakula na dawa nchini (TFDA), imekamata bidhaa mbalimbali ikiwemo vipodozi vilivyopigwa marufuku na vilivyomaliza muda vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. Milioni
2.6, mjini Singida.
Kukamatwa kwa bidhaa hizo, kumefuatia zoezi maalumu la oparesheni iliyofanyika katika maduka mbalimbali yanayouza bidhaa hizo, katika manispaa ya Singida.
Akizungumza na Singida Yetu Blog kaimu meneja wa TFDA kanda ya kati, Florent Kyombo amesema  bidhaa hizo zilikamatwa na maafisa wa mamlaka hiyo, kanda ya kati, kwa kushirikiana na wenzao wa manispaa Singida.
Kyombo amesema, katika operesheni hiyo jumla ya kilo 112.2 za vipodozi na vyakula visivyoruhusiwa kwa matumizi ya binadamu vilikamatwa.
Hata hivyo Kyombo akieleza kuridhishwa na mwamko wa wananchi na wamiliki wa biashara hizo katika mji wa Singida, kwa madai kuwa hivi sasa wanajitahidi kufuata sheria, kanuni na taratibu za TFDA.
“Wamiliki wa maduka hivi sasa wanajitahidi kufuata sheria za TFDA, bidhaa ikimaliza muda utakuta imeondolewa sehemu ya kuuzia, hadi chumba maalumu, tayari kwa ajili ya maafisa wa TFDA kukagua na kuteketezwa,”amesema.
Aliongeza operesheni hiyo iliyoanza desemba 10, 2012 mjini Singida, imeendelea hadi jana Desemba 15 mwaka huu, kabla ya kuendelea Singida vijijini na baadaye kumalizia katika wilayani Iramba.
Kyombo amesema hadi kufikia juzi jumatano ya tarehe 12, tayari maduka 64 yanayojihusisha na uuzaji vipodozi, dawa na vyakula yalikwishafanyiwa ukaguzi.
“Nashukuru wamiliki wa maduka ya vipodi, dawa na chakula wanatuelewa… sheria inafuatwa sana na ukiukwaji umepungua kwa asilimia kubwa sana ikilinganishwa na hapo mwanzo,”alifafanua.
Aidha Kyombo ametumia fursa hiyo kuwataka wamiliki na watumiaji kuchukua tahadhari kwa kusoma muda wa bidhaa kutengenezwa na muda wa kuharibika, kila wanaponunua bidhaa katika maduka mbalimbali.
“Jamii iwe makini na bidhaa wanazonunua…vipodozi vilivyopigwa marufuku vina madhara makubwa sana, vinasababisha kansa ya figo na ngozi, kwa kweli zinaharibu ngozi, naomba wananchi wawe makini sana,”amesema Kyombo.

No comments:

Post a Comment