Friday, January 4, 2013

Mamia wakwama, wawili wafariki Singida Kutokana na Mvua Kubwa Zinazoedelea Kunyesha

Wananchi wakivuka kwa miguu katika Daraja la Manung’una, lililopo katika Kijiji cha Msisi, Singida ambalo limekatika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
 
MVUA zinazoendelea kunyesha mkoani Singida, zimesababisha maafa
makubwa baada ya watu wawili, mmoja akiwa raia ya China, kufariki dunia
kwa kusombwa na maji,huku mamia ya abiria wakikwama njiani baada ya
daraja linalounganisha mkoa huo na mingine kukatika.Kukatika kwa Daraja la Munung’una kwa siku mbili
sasa,kumesababisha msongamano mkubwa wa magari yanayokadiriwa kuwa
zaidi ya 300.
Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa
waliofariki dunia kutokana na mvua hizo ni Xue Hui (36),maarufu kwa
jina la Kevin na Mariamu Samweli(18), mkazi wa Kijiji cha Maluga ambao
walifariki dunia kwa nyakati tofauti baada ya kusombwa na maji.



Vifo vyao vimeongeza idadi ya watu waliofariki
dunia kutokana na mvua mkoani Singida kufikia sita katika siku tatu
zilizopita. Mvua za juzi, zilisababisha watu wanne wa familia moja
katika Wilaya ya Mkalama kupoteza maisha baada ya kuangukiwa na nyumba
ya tembe.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Ole Lenga alisema raia
huyo wa China, alifariki dunia juzi jioni katika Kijiji cha Gumanga
Wilaya ya Mkalama baada ya gari alilokuwa anasafiria kusombwa na maji...
“Mchina huo alikuwa na mtoto wake ambaye alinusurika kifo.”

Alisema
Mariamu alifariki dunia baada ya kusombwa na maji katika Mto Kiula
uliopo katika Kijiji cha Igonia. “Miili ya marehemu hao imehifadhiwa
kwenye chumba cha maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida.”



Abiria wakwama
Mvua hizo kubwa
zilizonyesha tangu mwishoni mwa Desemba mwaka jana, zilisababisha
daraja hilo la Munung’una lililopo katika Kijiji cha Msisi wilayani
Singida kuvunjika.

Kutokana na athari hiyo, kumekuwa na msongamano
mkubwa wa magari baada ya mawasiliano kati ya Singida na mikoa ya kanda
ya ziwa na nchi jirani kukatika.
Baadhi ya wananchi walilalamikia uharibifu huo
wakisema umetokana na ujenzi wa daraja hilo kuwa wa kiwango cha chini.
Dereva, George Medadi akitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam, alisema
daraja hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kujengwa chini ya kiwango.

1 comment: