Thursday, March 14, 2013

Asilimia 12 tu ya kaya katika halmashauri ya Singida ndio wamejiunga na mfuko wa afya ya jamii.

 Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi (wa pili kulia) akifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa za mfuko wa taifa wa bima ya afya na mfuko wa afya ya jamii, kwenye bwalo la shule ya sekondari ya Mwenge mjini Singida.Wa kwanza mbele kulia ni afisa elimu sekondari manispaa ya Singida Mafita. Wa kwanza kushoto ni afisa wa mfuko wa taifa bima ya afya mkoa wa Singida Agnes Chaki na anayefuatia na kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Singida.
 Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi akifungua semina ya siku moja iliyohudhuriwa na wadau wa mfuko wa taifa wa bima ya afya na mfuko wa afya ya jamii (CHF) iliyofanyika kwenye bwalo la shule ya sekondari ya Mwenge mjini Singida. Kushoto ni kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Singida na kulia ni afisa elimu sekondari katika manispaa ya Singida.
Afisa wa mfuko wa taifa wa bima ya afya mkoa wa Singida Agnes Chaki, akitoa taarifa yake kwenye semina ya wadau wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) na mfuko wa afya ya jamii (CHF)  iliyofanyika kwenye bwalo la shule ya sekondari ya Mwenge mjini Singida.
 

Kati ya kaya 23,860 za halmashauri ya manispaa ya Singida ni kaya 2,845 ambayo ni sawa na aslimia 12 tu ndizo zilizojiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) imeelezwa.
Mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Qeen Mlozi, amesema hayo wakati akifungua zoezi la utoaji elimu kwa wadau wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) na mfuko wa afya ya jamii (CHF) wa halmashauri ya manispaa ya Singida.
Amesema kutokana na hali hiyo mbaya, upo umuhimu mkubwa kwa viongozi na watendaji kuongeza juhudi katika
kuelimisha na kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo.
Kuhusu mfuko huo, Mlozi ametaja baadhi ya sababu za kuanzishwa kwa mfuko huo kuwa ni pamoja na kuiwezesha jamii kumiliki huduma za afya zinazowahusu katika maeneo wanayoishi na kushirikisha jamii kutoaq mawazo yao, ili kuboresha huduma za afya kupitia mikutano na kamati mbalimbali watakazozichangua wao wenyewe.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya, ametaja baadhi ya faida za mfuko huo kuwa ni huduma ya wagonjwa wa kutwa na kulazwa, vipimo vya maabara, wanachama kupata huduma bora ya afya kwa mwaka mzima na huduma ya upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na halmashauri husika.
Kuhusu wadau waliohudhuria zoezi la utoaji elimu juu ya mifuko hiyo, Mlozi amewataka wawe wajumbe wazuri wa kuwaelimisha wengine ambao hawakupata bahati ya kuhudhuria zoezi hilo.
“Kuja kwenye zoezi hili leo, iwe ni dhamana ambayo utekelezaji wake ni wewe uliyekuja hapa, kurudi sehemu yako ya kazi, ili uwaeleze/uwaelimishe wenzako nini kimejadiliwa hapa”alifafanua Mlozi.
Zoezi hilo la utoaji elimu juu ya mifuko hiyo miwili, liliandaliwa na ofisi ya mfuko wa taifa wa bima ya afya mkoa wa Singida na lilifanyika katika bwalo la shule ya sekondari ya Mwange mjini Singida na kuhudhuriwa na baadhi ya walimu wa shule za sekondari na msingi, watendaji wa manispaa ya Singida na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mwenge. 

No comments:

Post a Comment