Saturday, March 30, 2013

Mwalimu wa walemavu amtaka Rais ateue walemavu kushika nafasi za Ukuu wa Wilaya, Mkoa na Uwaziri.

 Mwalimu mkuu msaidizi wa walemavu katika shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Donard Bilali akitoa wito wake kwa rais Kikwete kuangalia uwezekano wa kuteua walemavu kushika nafasi za ukuu wa wilaya,mkoa na uwaziri kama anavyofanya kwa kundi la wanawake.
Mwalimu wa walemavu katika shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilayani Ikungi,Manase Ligula akitoa wapendekezo yake kuwa katiba ijayo,iagize wamiliki wa vyombo vya usafiri,watoe huduma bure kwa walemavu.

Rais wa jamhuri ya muungano Tanzania,Dk.Jakaya Mrisho Kikwete ameshauriwa kuangalia uwezekano wa kuteua walemavu kushika nafasi za ukuu wa wilaya,mkoa na uwaziri kwa wale wenye uwezo na sifa za kuongoza katika nafasi hizo kwa ufanisi.
Wito huo umetolewa na mwalimu mkuu msaidizi wa walemavu katika shule ya msingi mchanganyiko ya Ikungi wilaya ya Ikungi , Donard Bilali wakati akizungumza na Singida Yetu Blog juu ya zoezi la uundwaji wa mabaraza ya katiba.
Amesema serikali ya awamu ya nne iliyoko chini ya rais Kikwete,imefanya
mambo mengi mazuri ikiwemo kushirikisha kikamilifu makundi mbalimbali ya watu katika utendaji wa serikali.
“Kwa moyo wa dhati kabisa,nampongeza sana rais Kikwete kwa hili la ushirikishwaji,amefanya vizuri sana kwa kundi la wanawake.Sasa nadhani wakati umefika na sisi walemavu atuangalie katika nafas za ukuu wa wilaya,mkoa na hata uwaziri”,amesema mwalimu Bilali kwa kujiamini.
Mwalimu Bilali ambaye pia ni katibu mkuu wa chama cha walemavu wilaya ya Ikungi,alisema hata hivyo asiteue tu mtu mradi mlemavu, aangalie sifa, uadilifu na uwezo wa kumudu nafasi husika.
Aidha ameiomba serikali iwape haki sawa na watu wasio walemavu katika kunufaika na mifuko mbalimbali ya umma ikiwemo fedha za JK,i li kundi hilo liweze kupiga hatua katika kuboresha hali zao za kiuchumi.
Mwalimu huyo ambaye ana ulemavu wa kutokuona, alipendekeza katiba ijayo ibainishe wazi kuwa walemavu wasome bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu,kama njia mojawapo ya kuwavutia walemavu kujiendeleza kielimu.
Kwa upande wake mwalimu Manase Ligula,amesema upo umuhimu mkubwa kwa walemavu  wakajumuishwa kwenye mabara ya katiba, kwa madai kuwa wao ndio wanaoyafahamu kwa kina mahitaji yao.
Mwalimu Ligula ambaye ni mlemavu wa macho,alisema pia katiba ijayo iweke wazi kuwa walemavu waruhusiwe na wamiliki wa vyombo vya usafiri kusafiri bure popote aendapo.
Alisema hilo linawezekana kwa madai kuwa kundi la walemavu ni dogo sana kwa hali hiyo, litakuwa halina madhara yo yote kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri.

No comments:

Post a Comment