Thursday, March 7, 2013

Polisi mkoani Singida yamnasa mtuhumiwa akiwa na bunduki aina ya SMG na risasi 30.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida Linus Sinzumwa (kushoto) akishikilia silaha ya kijeshi  bunduki aina ya SMG aliyodai kukamatwa ikiwa imehifadhiwa  ndani ya sanduku la nguo na kufichwa kwenye shamba la mahindi katika kijiji cha Itigi jimbo la Manyoni Magharibi. Bunduki hiyo inadhaniwa kuwa ilikuwa ikitumika kwenye matukio ya uhalifu ikiwemo ujambazi. Juu ya meza ni risasi 30 za SMG hiyo. Kulia ni afisa upelelezi (RCO) wa makosa ya jinai mkoa wa Singida Thobias Sedoyeka.

Jeshi la polisi mkoani Singida limefanikiwa kukamata silaha ya kijeshi bunduki aina ya SMG na risasi zake 30, ambayo inadhaniwa  kuwa ilikuwa ikitumika katika matukio ya uhalifu mbalimbali ukiwemo wa ujambazi wa kutumia silaha.
 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Linus Sinzumwa, amesema kuwa bunduki aina ya SMG waliyoikamata ina namba za usajili UA 39621992 na imekamatwa Machi tano mwaka huu, kwenye msako mkali unaoendelea mkoani Singida kusaka wahalifu mbalimbali.
 Amesema kuwa mtu mmoja amekamatwa kwa
tuhuma ya kumiliki bunduki hiyo ya kijeshi kinyume cha sheria na kwamba kwa sasa, jina la mtuhumiwa haliwezi kutangazwa kwa vile vinaweza kuharibu upelelezi unaoendelea.
 Sinzumwa amesema kuwa silaha hiyo, ilikamatwa ikiwa imehifadhiwa ndani ya sanduku la nguo ambalo lilifunikwa na majani na kuwekwa katikati ya shamba la mahindi.
Amesema mafanikio hayo makubwa yametokana na ushirikiano mkubwa uliotolewa na raia wema ambao walitoa taarifa sahihi zilizoweza kusaidia mtuhumiwa kukamatwa pamoja na silaha hii ya kijeshi na kuwaomba wananchi waendelee na moyo huo huo wa kutoa ushirikiano ili kusaidia vita hivi vya kukomesha vitendo vya uhalifu mkoani Singida.
 Aidha amesema uchunguzi/upelelezi ukikamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.
 Katika tukio jingine, Kamanda Sinzumwa amesema huko katika mtaa wa Karakana mjini Singida, Tatu Idd (25) alikamatwa akimiliki lita tano za pombe haramu ya gongo pamoja na mtambo wake.
“Pia siku hiyo hiyo, Abbakari Mohammed (30) tumemkamata akiwa na misokoto ya bangi 15 ndani ya mifuko yake ya suruali ambayo alikuwa akiitembeza kuiuza. Vijana  wanane ambao tunahisi kuwa ni vibaka sugu nao tumewakamata tunaendelea kuwahoji. Muuza gongo sugu Tatu, muuza bangi Abbakari na vibaka nane, tukimaliza upelelezi, tunatarajia kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili”, amesema.

No comments:

Post a Comment