Monday, March 18, 2013

TANROADS Singida yaagizwa kusimamia wakandarasi wa barabara kwa ukaribu ili kuepuka ujenzi chini ya kiwango.

 Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Vicent Kone akifungua kikao cha 34 cha bodi ya barabara mkoa wa Singida leo. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya  mkuu wa mkoa mjini Singida.

 Baadhi ya wajumbe wa kikao cha 34 cha bodi ya barabara mkoa wa Singida, wakifuatilia kwa makini kikao hicho kilichokuwa chini ya mwenyekiti ambaye ni  mkuu wa mkoa wa  mkoa wa Singida Dk.Parseko Vicent Kone (hayupo kwenye picha).

Mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Parseko Vicent Kone ameuagiza wakala wa barabara (TANROADS), kusimamia kwa karibu na kuhakikisha wakandarasi wanaopewa kazi ya kujenga barabara, wanajenga kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mikataba yao.
Dk. Kone amesema kwa njia hiyo kutasaidia mno kupunguza mianya ya kupoteza fedha za umma na  pia, kuondoa malalamiko kutoka kwa viongozi na wananchi, kwamba ujenzi husika haufanani na fedha zilizotumika.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo leo wakati akifungua
kikao cha 34 cha bodi ya barabara cha mkoa wa Singida, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini Singida.
Amesema kumekuwa na malalamiko mengi ambayo yanaelekezwa kwa wajenzi wa madaraja, makalvati na barabara, kuwa miundo mbinu hiyo inajengwa kwa ubora usioridhisha kabisa.
Dk. Kone amefafanua kuwa inawezekana mimi kama kiongozi au mwananchi yeyote asiwe na elimu ya uhandisi, lakini akawa na ufahamu unaomuwezesha kubaini kuwa barabara au daraja fulani, limejengwa chini ya kiwango, hivyo tuheshimu maelekezo ya viongozi na kuwasikiliza wananchi, ili kazi zetu ziwe na ubora unaotakiwa.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewataka wakurugenzi wa halmashauri na mstahiki meya wa manispaa ya Singida kupitia mabaraza ya madiwani, wasimamie kwa karibu ujenzi wa barabara zao, ili kutumia fedha kwa thamani inayokusudiwa (value for money) na kuondokana na malalamiko kutoka kwa wananchi ambao ndio walipa kodi.
Aidha, Dk.Kone amewataka wakurugenzi hao na mstahiki meya, kutumia maabara za TANROADS kwa ajili ya kupima ubora wa kazi zinazofanywa na wakandarasi.
Amesema upimaji huo ujumuishe pia na kupima ubora wa udongo uliotumika, uimara wa madaraja na makalvati yanayojengwa.
“Vile vile ameomba sana, tusikimbilie kuwalipa wakandarasi kabla hatujajiridhisha na kazi zao”amesema mkuu huyo wa mkoa.
Wakati huo huo Dk.Kone ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali kwa kumuamuru mkandarasi CHICCO na mhandisi mshauri BCOM kutoka Ufaransa, kukijenga upya kwa kiwango cha lami kipande cha barabara kati ya Sekenke na Shelui chenye urefu wakilomita 33.3 kwa gharama zao.
Hii ni baada ya kubainika kuwa kipande hicho kilijengwa chini ya kiwango.

No comments:

Post a Comment