Tuesday, April 9, 2013

MVUA KUBWA YASABABISHA KIFO CHA KIKONGWE NA WATU ZAIDI YA 7 KUKOSA MAKAZI SINGIDA.

 Mkuu wa wilaya ya Singida, mwalimu Queen Mlozi akizungumza na mwandishi wa habari wa Singida Yetu Blog ofisini kwake juu ya madhara makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha wilayani humo.
 Nguzo ya umeme iliyoangushwa katika mtaa wa Utemini stesheni  baada ya kunyesha kwa mvua kubwa iliyoambatana na upepe mkali.
 Mabati ya banda la maonyesho lililopo Mandewa nje kidogo ya Singida mjini, yakiwa juu ya mti baada ya kutupwa na upepo mkali wakati mvua kubwa ilionyesha siku ya Ijumaa.

Banda pekee la maonyesho lililopo Mandewa nje kidogo ya Singida mjini likiwa limeezuliwa mabati kwa upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa zilizonyesha Ijumaa jioni mjini Singida.

Picha juu na chini ni Nyumba iliyokuwa ikimilikiwa na kikongwe Isima Kituku @Nyamwantandu (86) iliyopo maeneo ya uwanja wa ndege wa jimbo la Singida mjini, baada ya kubomolewa na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa. Kikongwe huyo alifariki dunia kwa kupigwa na radi wakati akikimbilia kwa jirani yake kujihifadhi.

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani Singida, zimesababisha madhara makubwa ikiwemo kikongwe mmoja mwenye umri wa miaka 86 kupigwa na radi, na kufariki dunia na pia wakazi wa nyumba saba kukosa makazi.
Mkuu wa wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi amesema kuwa mvua hiyo kubwa mbaya ya hatari na yenye maji mengi, ilinyesha Ijumaa jioni kuanzia saa 2.15 hadi saa 3.45 usiku.
Amesema mvua hiyo iliambatana na upepo mkali, na  matukio ya mara kwa mara  ya radi kali ambayo yaliogofya sana wakazi wengi wilayani humo.
Amesema jumla ya
nyumba saba, kanisa moja na kibanda cha maonyesho cha mkoa kilichopo Mandewa nje kidogo ya mji wa Singida, zimeezuliwa mabati na zingine zimeangushwa.
Mlozi amesema katika matukio hayo, bibi kikongwe Isima Kitiku Nyamwantandu (86) mkazi wa maeneo ya uwanja wa ndege mjini Singida, amefariki dunia baada ya kupigwa na radi wakati anakimbilia kwa jirani yake kwenda kujihifadhi, baada ya kuta za nyumba yake kubomolewa na upepo ulioambatana na mvua hiyo.
“Nimefika kwenye msiba wa bibi huyo na kutoa ubani kidogo.Lakini nilipoikagua nyumba yake iliyobomolewa,niligundua kuwa haikuwa bora na ilijaa nyufa kitendo ambacho kwa vyo vyote,kimechangia kuta za nyumba hiyo kubomoka”amesema Mlozi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kwa ujumla nyumba zote zilizoathirika na mvua hiyo,karibu zote zilikuwa na mapungufu mengi kitendo kilichosababisha mapaa yaezuliwe na kuta kuangushwa kirahisi.
“Nitumie fursa hii kuwataka wakazi wa wilaya yangu kujenga utamaduni wa kukagua nyumba zao na hasa zile za Tembe.Wahakikishe kama zipo imara kukabiliana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hivi sasa. Hofu yangu kubwa ipo kwenye nyumba za matembe, hizi nyumba kuna wakati unafika miti iliyotumika kujengea, huoza na hivyo inakuwa rahisi kuangushwa”amesema mkuu huyo wa wilaya.

No comments:

Post a Comment