Monday, September 16, 2013

Watahiniwa wa darasa la saba wamebambwa wakiwa hawajui kusoma na kuandika

JUMLA ya wanafunzi 22 wa shule tatu za msingi wilaya ya Ikungi mkoani Singida,’wamebambwa’ wakiwa kwenye vyumba vya kufanyia mtihani wa taifa darasa la saba,huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.

 Wanafunzi hao na idadi yao kwenye mabano walikuwa kwenye shule ya msingi Muhintiri (2),Iglansoni (16) na Kinyampee (4) tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi.

 Wakati kwenye shule ya msingi Mnyange tarafa hiyo hiyo ya Ihanja mwanafunzi mmoja wa kike hakufika kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi hakuhudhuria kufanya mtihani huo kwa kile kilichodaiwa tayari ameishaozwa.

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi Protace Magayane,aliyekuwa akikagua maendeleo ya zoezi la kufanya mtihani huo katika siku yake ya mwisho juzi, aliagiza wazazi wa mwanafunzi huyo wa kike ambaye hakufanya mtihani,wachukuliwe hatua stahiki za kisheria haraka iwezekanavyo.

 Baadhi ya wasimamizi akiwemo Ernest Mahendeka wa shule ya Kinyampembee, Rebeca Julius wa Muhintiri na Salum Jafari wa Iglanson wamesema ilibidi wajaze fomu maalumu kulingana na maelekezo kabla ya kuwaacha waendelee na mtihani kulingana na jinsi wanavyoelewa.

 Kwa upande wao  wahitimu akiwemo Perpetua Msengi na John Martin, wamesema wana matumaini makubwa ya kufaulu mtihihani huo, ingawa somo la hisabati lilionekana kuwa gumu kwa upande wao.

 Katika hatua nyingine,Mkurugenzi Magayane amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha mwakani
ufaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi katika wilaya hiyo mpya, unafikia aslimia 70.

 “Hili linawezekana kwa sababu hivi sasa ufaulu wetu ni aslimia 51 wakati kitaifa unatakiwa uwe 31.

Kwa hali hiyo nina imani kubwa kuwa lengo letu tutalifikia na ikiwezekana tuvuke hilo lengo,ili mwaka 2015 tuweze kufikisha aslimia 80”, amesema Magayane  kwa kujiamini.

No comments:

Post a Comment