Wednesday, November 20, 2013

SEMA yagharamia ujenzi wa Vyoo kwa Tsh 155m shule tano za Manispaa ya Singida.

Meneja wa shrika la SEMA, Ivo Manyanku,(wa kwanza kulia) akitoa taarifa yake ya ujenzi wa vyoo bora katika shule tano za msingi manispaa ya Singida kwa Naibu Waziri TAMISEMI (Elimu), Mh. Kassim Majaliwa (mwenye miwani).Vyoo hivyo vimegharimu zaidi ya shilingi 155 milioni.
Naibu Waziri TAMISEMI (Elimu) Mh. Kassim Majaliwa (aliyeipa kisongo kamera) akizindua rasmi ujenzi wa vyoo bora katika shule ya msingi Unyankindi.Vyoo hivyo bora vimejengwa kwa gharama ya shilingi 155 milioni na shirika la SEMA.Kushoto ni meneja wa SEMA. Ivo Manyanku.
Naibu Waziri wa TAMISEMI (Elimu),Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria ufunguzi wa matumizi ya vyoo bora vya shule ya msingi Unyankindi mjini Singida.Vyoo hivyo vimejengwa na shirika la SEMA kwa gharama ya shilingi 155 milioni.
Moja ya vyoo bora vya shule ya msingi Unyankindi manispaa ya Singida vilivyojengwa na shirika la SEMA la mkoa wa Singida.

Shirika lisilo la kiserikali la Sustainable Environment Management Action (SEMA) la mkoani Singida limetumia zaidi ya shilingi 155 milioni kugharamia ujenzi wa vyoo bora katika shule tano za manispaa ya Singida.

 Shule zilizonufaika na mradi huo ni,Unyankindi,Singidani,Manguamitogho,Mtamaa na Mtisi.

 Hayo yamesemwa juzi na Meneja wa SEMA, Ivo Manyanku wakati akizungumza kwenye hafla iliyofana ya uzinduzi wa vyoo hivyo uliofanyika katika shule ya msingi Unyankindi Singida mjini.

 Amesema fedha hizo zilizotumika katika ujenzi huo zimetolewa ufadhili na shirika la WaterAid Tanzania kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji na usafi shuleni katika halmashauri ya manispaa ya Singida.

 “Vyoo hivi vina matundu 48 ambayo yana uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,903 kati yao wavulana ni 1,446 na wasichana ni 1,457.Idadi hiyo inajumuisha na walemavu 38 ambao 25 ni wavulana na 13 ni wasichana”,amesema Meneja huyo.

 Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi huo,naibu waziri TAMISEMI (elimu),Kassimu Majaliwa,alitumia fursa hiyo kulipongeza shirika la SEMA kwa ujezi bora wa vyoo hivyo ambavyo vimekidhi vigezo vyote vinavyohitajika.

 Amesema serikali na wadau wengine wa maendeleo hawana budi kuliunga mkono shirika la SEMA kwa madai linatelekeza miradi yake kulingana na thamani ya fedha zilizotumika.

 “SEMA binafsi nawapongezeni sana ujenzi huu mtakuwa mmeisaidia serikali katika kupunguza
kero mbalimbali zinazoikabili sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu.Vyoo hivi ni bora mno na vitakuwa vimepunguza kwa kiwango kikubwa uhaba wa vyoo katika shule zetu za msingi”,amesema Majaliwa.

 Wakati huo huo, Naibu Waziri huyo ameuomba uongozi wa halmashauri ya manispaa ya Singida kusimamia matumizi ya vyoo hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu zaidi.

No comments:

Post a Comment