Thursday, January 9, 2014

Halmashauri ya Manispaa ya Singida kukusanya shilingi 31.7 bilioni 2014/2015.

Mstahiki meya wa manispaa ya Singida, Sheikh Salum Mahami,akifungua kikao maalum cha madiwani cha kupitisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha.Kushoto ni naibu meya Hassan Mkata na kulia ni kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Singida na Afisa mipango,Deus Lusiga.
Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Singida, Deus Lusiga, akitoa ufafanuzi kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani lililokuwa linapitisha mapendekezo ya bajeti 2014/2015.
Baadhi ya madiwani wa manispaa ya Singida,wakifuatilia kwa makini mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/2015.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Singida inatarajia kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi 31.7 bilioni kutoka vyanzo vyake mbalimbali vya mapato katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida,Deus Luziga wakati akitoa mapendekezo ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha mbele ya kikao maalum cha madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo.

Luziga ambaye ni Afisa Mipango wa Manispaa ya Singida amesema wanatarajia kukusanya zaidi ya shilingi 2.9 biloni kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.

Amesema wanatarajia serikali kuu itawapatia ruzuku ya shilingi 181,219,050 kwa ajili ya kufidia ushuru na kodi iliyofutwa.

“Serikali kuu pia tunatarajia itatupa zaidi ya shilingi 15.2 bilioni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma,itatupatia pia ruzuku ya zaidi ya shilingi 1.8 bilioni ya matumzi yasiyo ya mishahara na ruzuku ya miradi ya maendeleo ya zaidi ya shilingi 11.6 bilioni’,amesema.

Kaimu Mkurugenzi huyo amesema bajeti ya Manispaa ya Singida imeongezeka kwa shilingi 13,630,476,230 ambayo ni sawa na asilimia 43 ya lengo la kukusanya zaidi ya shilingi 18.1 bilioni katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/2014.

“Ongezeko hili limechangiwa pamoja na kuongezeka kwa ajira mpya na nyongeza za mishahara na kuongezeka kwa

miradi ya maji ambayo mwelekeo wake ni kutekeleza miradi katika vijiji 20″,alifafanua.

Luziga amesema kuwa manispaa ya Singida imeandaa bajeti yake kwa kuzingatia mwongozo wa bajeti wa taifa na sera ya taifa ya kuondoa umaskini.

“Pia imezingatia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, ahadi mbalimbali za rais na miongozo mingine inayolenga kuwanufaisha wananchi”,amesema.

No comments:

Post a Comment