Friday, April 4, 2014

China kuwekeza kwenye kilimo mkoani Singida.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone (wa kwanza kulia) akimwonyesha Balozi wa Jamhuri ya watu wa China,Dk.Lu Youqing (katikati) eneo lililopo katika kijiji cha Kisasida manispaa ya Singida mahali umeme wa nishati ya upepo utazalishwa  na kampuni kutoka nchini China. Kushoto ni mwakilishi mkuu wa uwakilishi wa kiuchumi na kibiashara wa Jamhuri ya watu wa China nchini, Lin Zhiyong.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone (mwenye suti nyeusi) akibadilishana mawazo na Balozi wa Jamhuri ya watu wa China (katikati) wakati Balozi huyo alipotembelea eneo la kijiji cha Kisasida manispaa ya Singida mahali kampuni ya Kichina, inatarajiwa kuanza kuzalisha umeme wa nishati ya upepo.
Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone (kulia) akizungumza ofisini kwake na baadhi ya viongozi waliokuwa wameambatana na Balozi wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini, Dk.Lu Youqing katika ziara ya balozi huyo mkoani Singida.

BALOZI wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini, Dk.Lu Youqing amesema nchi yake inatarajia kuwekeza kwenye sekta mbalimbali mkoani Singida ikiwemo sekta ya kilimo na ufugaji, ili kuharakisha kukuza uchumi wa mkoa huo.

Balozi Youqing aliyasema hayo wakati akizungumza ofisini kwa mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo.

Amesema uwekezaji huo utawanufaisha wakazi wengi wa mkoa wa Singida ambao ni wakulima na wafugaji.

Balozi Youqing alifafanua zaidi kwa kusema kuwa kwa kuanzia,China kupitia kampuni yake moja imeonyesha nia ya kuwekeza katika kufua umeme wa kutumia nishati ya upepo.


“Tanzania ina hitaji kubwa la umeme wa upepo ambao utakuwa wa gharama ndogo na hauchafui mazingira”,amesema.

Akisisitiza zaidi, amesema kuwa kutokana na historia ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China, sekretarieti za mikoa na serikali za mitaa, zina fursa ya kushirikiana na mamlaka za serikali za mikoa nchini China ili kujifunza teknolijia mbalimbali.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, Balozi Youqing amesema
sekretariati za mikoa na serikali za mitaa kupitia ushirikiano huo, zitafute kampuni za uwekezaji na pia zitabadilishana uzoefu katika maeneo mengi ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Kone, alimshukuru Balozi Youqing kwa kuonyesha ni ya kushirikiana na mkoa wa Singida katika mradi wa umeme wa nishati ya upepo.


Dk.Kone amesema mradi wa umeme wa upepo hautaunufaisha tu mkoa wa Singida,bali taifa kwa ujumla kwa kutoa fursa nyingi za ajira, ongezeko la viwanda na  umeme wa uhakika.

No comments:

Post a Comment