Friday, April 4, 2014

Mamlaka ya maji Singida yadai zaidi shilingi milioni 210.

Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone, akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya maji manispaa ya Singida.Wa kwanza kulia (walioketi) ni Kaimu Mkurugenzi wa SUWASA ,Eng.Kombe Mushi, anayefuatia ni Meya Mstahiki manispaa ya Singida na Sheikh mkoa wa Singida, Salum Mahami na Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya Masi safi na mazingira safi (SUWASA) Singida mjini, Eng.Kombe Mushi,akitoa taarifa yake ya utendaji wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji.
Mkurugenzi wa manispaa ya Singida, Joseph Mchina, akitoa nasaha zake kwenye maadhimisho ya wiki ya maji katika manispaa hiyo yaliyofanyika Mandewa mjini Singida.
Mwenyekiti wa bodi ya SUWASA, Kisenge akitoa nasaha zake kwenye uzinduzi wa wiki ya maji manispaa ya Singida.
Tanki la maji la SUWASA lililopo Mandewa mjini Singida.

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (SUWASA) Singida mjini, inadai wateja wake mbalimbali zaidi ya shilingi 210.9 milioni, kitendo kinachochangia kudhoofisha utendaji wa mamlaka hiyo.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji SUWASA, Eng. Kombe Mushi wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji uliofanyika Mandewa nje kidogo ya mji wa Singida.

Amesema kati ya madeni hayo, wateja binafsi wanadaiwa zaidi ya shilingi 123.7 milioni, wakati wafanyabiashara mbali mbali, wanadaiwa zaidi ya shilingi 12.9 milioni.

“Taasisi mbali mbali za serikali, tunazidai shilingi 70,750,185 na madhehebu ya dini tunayadai zaidi ya shilingi 3.6 milioni.  Fedha hizi nyingi, endapo tutalipwa zote, zitatusaidia mno kuboresha utoaji wa huduma zetu”,amesema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Aidha, Eng.Kombe amesema mbaya zaidi ni kwamba badhi ya wadaiwa hao, hushindwa kurejesha huduma ya maji na badala yake, kununua maji kutoka kwa majirani au kujiunganishia maji na kuchepusha dira za maji.

“Changamoto zingine tunayokabiliana nayo ni, upotevu wa maji kupitia mifimo chakavu ya maji.  Kwa wastani upotevu huo ni asilimia 43.  Hata hivyo tumejipanga vizuri kwa ajili ya kulimaliza tatizo hilo”,alifafanua.

Katika hatua nyingine, Eng. Mushi amewataka wananchi kuwafichua watu wanaojiunganishia maji kiholela na wanaochepusha dira ya maji.  Bingo ya shilingi
50,000/= itatolewa kwa atakayetoa taarifa sahihi kuhusiana na wateja hao wenye lengo la kuhujumu mamlaka.

Maudhui ya wiki ya maji mwaka huu, ni “maji na nishati ambayo inatokana na kauli mbiu ya siku  ya maji duniani.


No comments:

Post a Comment