Friday, April 4, 2014

Soko la Nyuki ni mkombozi wa kiuchumi kwa Wafugaji – Dk. Kone.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, (wa nne kulia) akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa utundikaji wa mizinga ya Nyuki mkoani Singida.Wa pili kushoto ni mkuu wa wilaya ya Mkalama Edward Ole Lenga.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida, Edward Ole Lenga, akizungumza kwenye hafla ya utundikaji mizinga ya nyuki kimkoa zilizofanyika katika kijiji cha Nkungi wilayani Mkalama.Wa pili kulia walioketi,ni mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone na (wa kwanza kulia) ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama,James.Kushoto (aliyekaa), ni Katibu tawala mkoa wa Singida Liana Hassan.
Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone, akiweka nta kwenye mzinga wa Nyuki kama njia moja wapo ya kuwavutia Nyuki ili waweze kupanga kwenye mzinga huo.

MKUU wa Mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone ameziagiza Halmashauri na Manispaa ya Singida, kuanzisha au kuunda ushirika utakaosaidia wafugaji kupata soko zuri la mazao ya nyuki ili waweze kuharakisha kujikomboa kiuchumi.

 Dk.Kone ametoa agizo hilo hivi karibuni wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya taifa ya utundukaji mizinga ngazi ya mkoa yaliyofanyika kimkoa wilayani Mkalama.

Amesema utundikaji huo wa ushirika wa wafuga nyuki ni agizo lililotolewa na Waziri Mkuu kuwa kila mkoa uwe na ushirika huo.

Akifafanua zaidi,Dk.Kone amesema ushirika wa wafugaji nyuki,una faida nyingi ikiwemo wafugaji kupata soko zuri na la uhakika.

Kuhusu siku ya utundikaji mizinga,amesema lengo lake ni kuhamasisha ufugaji nyuki ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki kwa kuzingatia ubora na teknolojia sahihi.

 “Kwa kutumia teknolojia sahihi,wananchi watazalisha
mazao mengi na yenye ubora unaokidhi viwango vya soko la kitaifa na kimataifa”,alifafanua Dk.Kone.


 Katika hatua nyingine,mkuu huyo wa mkoa,alisema mkoa umeweka mikakati kadhaa,ili kuhakikisha kuwa ufugaji wa nyuki unashamiri na kuwapatia wananchi kipato kizuri cha kujikimu katika mahitaji yao,ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara,kwa njia ya uchavushaji maua.

No comments:

Post a Comment