Monday, April 14, 2014

Wananchi waomba serikali kurudisha oparesheni tokomeza ujangili.

Mkuu wa wilaya ya Manyoni, Fatuma Toufiq (wa kwanza kushoto) na anayefuata ni Dc wa wilaya ya Iramba,Yahaya Nawanda na mkuu wa wilaya mpya ya Ikungi, Manju Masambya (wa tatu kushoto).

SERIKALI wilaya ya Manyoni mkoani Singida imeiomba serikali kuu kuangalia uwezekano wa kurejesha mapema zoezi la oparesheni ‘tokomeza ujangili’, ili kudhibiti kasi kubwa iliyopo ya majangili kuua wanyama pori hasa tembo.

Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni,Fatuma Toufiq wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya wimbi kubwa la majangili kuua wanyama pori na zaidi tembo katika hifadhi za wilaya hiyo.

Amesema kuwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita,majangili katika hifadhi ya Rungwa,Kizigo na Kihesi wilayani humo yameuawa tembo 35.

Aidha,Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi wameweza kukamata meno ya tembo mara mbili kati ya Januari na sasa katika kizuizi cha kijiji cha Kayui kata ya Mgandu.

“Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni tena tumemkamata Afisa Mtendaji wa kijiji cha Kayui Philemon Kanyonga na watu wengine wanne kwa tuhuma ya kumiliki meno ya tembo kilo160 na bunduki ya kivita SMG moja pamoja na risasi zake 195″, amesema.

Toufiq amesema kutokana na kasi hiyo ya uwindaji haramu unaotishia ustawi wa wanyamapori wakiwemo tembo,upo umuhimu mkubwa wa
oparesheni tokomeza ujangili ikarejeshwa mapema iwezekanavyo.

Naye Juma Kidimanda mkazi wa Singida mjini,ameiomba serikali iache kujivunia vitendo vya kutangaza tu kukamata nyara za serikali ikiwemo meno ya tembo bali ijikite zaidi katika kuongeza juhudi za kudhibiti vitendo vya uwindaji haramu wa wanyamapori.


“Hizi adhabu wanazopewa majangili wanaotumia silaha za kivita kuulia wanyamapori,nina wasi wasi nazo.Inaelekea sio kali kulingana na makosa wanayoyafanya.Napendekeza serikali ianzishe adhabu kali zaidi ikiwezekana ya kifo ili kuwaogofya majangili waweze kuachana na uwindaji haramu na kutafuta njia nyingine ya kujiingizia mapato”,amesema Juma.

No comments:

Post a Comment