Thursday, July 17, 2014

HAPA Singida kutumia mil 485 kuboresha afya vijiji 62.

Meneja wa shirika la HAPA la mkoa wa Singida, David Mkanje akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 7.4 milioni kwa kijiji cha Mlandala kata Urughu wilaya ya Iramba.Vifaa hivyo vimetolewa msaada na shirika la HAPA. Kulia ni mwenyekiti wa kijiji cha Mlandala,Mahona Mahela na kushoto ni kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Iramba, Dk.Antony Mburu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mlandala kata Urughu wlaya ya Iramba,Mahona Mahela, akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba vya zanahati ya kijiji hicho vilivyotolewa msaada na shirika la HAPA la mjini Singida. Kulia ni meneja wa shirika la HAPA, David Mkanje.
Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Iramba, Dk.Antony Mburu, akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 7.4 milioni vilivyotolewa msaada na shirika la HAPA.
Meneja wa shirika la HAPA, David Mkanje (kushoto) akimkabidhi kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Iramba, Dk.Antony Mburu,mizani ya kupimia watoto wachanga,ambayo ni sehemu ya msaada tiba wenye thamani ya zaidi ya shilingi 7.4 milioni uliotolewa na HAPA.
Baadhi ya wageni waliohudhuria hafla ya makabidhiano wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 7.4 milioni vilivyotolewa msaada kwa kijiji cha Mlandala kata Urughu wilaya ya Iramba.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Health Actions Promotion Association (HAPA) la mkoa wa Singida,linatarajia kutumia zaidi ya shilingi 485 milioni kugharamia utekelezaji wa mradi wa ‘Pamoja Tunaweza’ katika vijiji 62 vilivyopo kwenye kata 13, za wilaya ya Iramba na wilaya ya Mkalama.

Mradi huo wa miaka mitano ambao unatarajiwa kumalizika mwakani,lengo lake ni kuinua hali za afya za uzazi kwa akina mama na watoto.

Meneja wa shirika la HAPA, David Mkanje, alisema hayo wakati akizungumza kwenye hafla iliyofana ya makabidhiano ya vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 7.4 milioni vilivyotolewa na shirika hilo la HAPA,kwa kijiji cha Mlandala kata ya Urughu wilaya ya Iramba.

Alisema fedha hizo zilizotolewa na shirika la nchini Uholanzi la SIMAVI, zinatumika katika
kuhamasisha jamii kuhusu uzazi salama ambapo baba na mama wanatakiwa kuhudhuria klinki pindi mama anapokuwa mjamzito.


“Pamoja na ununuzi wa vifaa tiba na ujenzi wa majengo la kutolea huduma za afya,pia tunatoa elimu kwa jamii kuhusu unyanyasaji wa akina mama pindi wanapokuwa wajawazito na kuwapunguzia kazi,ili kulinda usalama wa mama na mtoto”,alifafanua Mkanje.

Kuhusu vifaa vilivyotolewa kwa zahanati ya Mlandala, Meneja huyo alivitaja kuwa ni kitanda cha kujifungulia, tray ya kubebea dawa,vifaa vya uzalishaji,mizani ya watu wakubwa,mizani ya watoto na stendi ya dripu.

Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Iramba, Dk.Antony Mburu, alisema kuwa utafiti unaonyesha kuwa kijiji cha Mlandala chenye wanawake 168,ni wanawake chini ya kumi (10),ndio wanajifungulia kwenye zahanati ya kijiji hicho.

“Hii ni hatari,inaonyesha akina mama wengi wajawazito wanajifungulia nje ya vituo vya afya,jambo ambalo ni hatari kwao na watoto wao.Sasa HAPA imewapatia vifaa bora vya kujifungulia,nina imani kwamba akina mama wajawazito,sasa watakimbilia kujifungulia hapa kwa usalama wao na watoto wao”,alisema Dk.Mburu.

Wakati huo huo,muuguzi wa zahanati hiyo Sekela Michael, pamoja na kulishukuru shirika la HAPA,alisema zahanati hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo tatizo la umeme.


Sekela alitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa usafiri katika kijiji hicho ambacho kipo umbali wa zaidi ya kilomita 100 kutoka ilipo hospitali ya wilaya.

No comments:

Post a Comment