Thursday, July 17, 2014

Kampeni ya ushawishi CHF yaanza Mkoani Singida.

Timu ya wataalamu kutoka NHIF mkoa wa Singida na ofisi ya DMO wilayani Singida, wakiendesha zoezi la upimaji wa afya kwa wananchi wa kata ya Msange wilayani Singida.
Afisa matekelezo na uratibu NHIF mkoa wa Singida, Isaya Shekifu (mwenye shati jeupe) akiendesha zoezi la upomaji wakazi wa kijiji cha Msange wilaya ya Singida vijijini.
Meneja wa NHIF mkoa wa Singida,Agnes Chaki, akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) kwa wananchi wa kata ya Ikhanonda .Kulia ni diwani wa kata ya Ikhanoda, Higa Mnyawi.

MFUKO  wa taifa  wa bima ya afya (NHIF)Mkoa wa Singida, umeanzisha kampeni ya utoaji elimu juu ya umuhimu wa kujiunga  na mfuko huo, na ule wa afya ya jamii (CHF),ili wananchi waweze kujijengea mazingira  ya kupata matibabu hata wakati hana fedha.

Katika kampeni hiyo wananchi watapata nafasi ya kupima afya.

Meneja wa NHIF mkoa wa Singida,Agness Chaki, akizungumza na waandishi wa habari alisema shughuli za upimaji wa afya ya msingi kwa wananchi wote zinafanyika kwa lengo la kuwafanya wananchi kuwa na hamasa ya kujua.


“Upo umuhimu mkubwa kujua hali ya afya yako mapema, badala ya
kusubiri mpaka kugua.Utamaduni wa kupima na kujua afya yako, pamoja na faida zake nyingi, unasaidia kudhibiti magonjwa, na hivyo kuondoa uwezekano wa kuugua ovyo ovyo”,alisema Chaki.

Meneja huyo alisema kwenye kampeni hiyo, Wananchi wanaweza kupata fursa ya kupima vipimo vya mapigo ya moyo (blood pressure),uwiano wa uzito na urefu(BMI) na kisukari.

Katika hatua nyingine,meneja huyo  amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF)ambao ada ya kiingilio ni shilingi 10,000/=tu.


Kwa ada hiyo,kaya yenye mume, mke mmoja na watoto wanne walio na umri wa chini ya miaka 18,watatibiwa kwa mwaka mzima bila kuongeza fedha zaidi.

“Kwa kujiunga na mfuko huo, wananchi watapata fursa ya kutibiwa kwenye vituo vyote vya Serikali Wilaya ya Singida na pia kupata rufaa ya kutibiwa kwenye Hospitali ya misheni ya st. Carol Mtiko”,alisema Chaki.

Kwa upande wake Afisa matekelezo na uratibu NHIF Mkoa wa Singida,Isaya Shekifu, kwa nyakati tofauti,amewaasa watumishi wa umma kutumia  fursa ya kufuata na NHIF hadi kwenye kata zao/vituo vyao vya kazi, kutoa kero zinazo wakabili wakati wa kupatiwa huduma ya matibabu.


Shekifu aliwataka watoe ushirikiano katika kujadili changamoto za mfuko huo, ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu,na kwa njia hiyo zitasaidia kuboresha huduma mbalimbali za afya.

No comments:

Post a Comment