Thursday, July 17, 2014

SEMA Singida wapongezwa kwa kuelimisha tabia nchi.

Mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi,akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya kuongeza uwajibikaji katika kuhimili mabadiliko ya tabia nchi wilayani humo.Kulia ni meneja wa shirika la SEMA, Ivo Manyaku.Kushoto ni mwenyekiti wa kijiji cha Kinyagigi.
Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la SEMA,Ivo Manyanku, akitoa taarifa yake kwenye hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya kuongeza uwajibikaji katika kuhimili mabadiliko ya tabia nchi wilaya ya Singida.Vifaa hivyo ni pamoja na vipeperushi,vikaragozi na mabango yenye gharama ya zaidi ya shilingi 22 milioni. Kushoto aliyekaa ni mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kunyagigi wilaya ya Singida,waliohudhuria uzinguzi wa ugawaji wa vifaa vya kuongeza uwajibikaji katika kuhimili mabadiliko ya tabia nchi.
Baadhi ya wanakikundi cha uhamasishaji cha Youth Culture Group cha mjini Singida, wakitoa burudani kwenye ufunguzi wa ugawaji wa vifaa vya kuongeza uwajibikaji katika kuhimili mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika kwenye kijiji cha Kinyagigi.
Kikaragosi kimojawapo ambavyo
vimebebeshwa bango lenye ujumbe wa mbinu bora za kukabiliana na mabadiliko ya batia nchi kilichopo kwenye kijiji cha Kinyagigi wilaya ya Singida.

SERIKALI  wilaya ya Singida, imelipongeza shirika lisilo la kiserikali la mpango endelevu wa uboreshaji mazingira (SEMA), kwa hatua yake ya kuanza kuelimisha wakulima mbinu bora za kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Pongezi hizo zimetolewa na mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya kuongeza uwajibikaji katika kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi.

Alisema mabadiliko ya tabia ya nchi ni tatizo linaloikabili dunia kutokana na ongezeko  la gesi joto angani, ambalo husababishwa na mizunguko mbalimbali ya shughuli za kibinadamu.

“Ukataji miti hovyo na uharibifu wa misitu unaofanywa hapa duniani, hususan kutokana na shughuli za upanuzi wa mashamba, mabadiliko  ya matumizi ya ardhi na uchomaji moto misitu, pia huchangia mabadiliko ya tabia ya nchi”,alisema.


Akifafanua zaidi, Mlozi alisema mabadiliko hayo ya tabia ya nchi, yana madhara mbali mbali, ikiwemo kuongezeka kwa joto duniani, kina cha maji baharini, ukame, mafuriko na kubadilka kwa mifumo ya ikolojia.

Alisema wilaya ya Singida, ni miongoni mwa wilaya nchini  ambazo zimeathirika na mabadiliko ya tabia ya nchi, madhara hayo ni pamoja na kupungua kwa mvua, mifugo na mazingira kuharibika kutokana na mabadiliko hayo.

“Kadri ya upatikanaji wa mvua na maji unavyopungua, uzalishaji wa mazao na ubora wa mifugo, nao unapunga.  Hali hii inasababisha uhaba wa chakula, kushuka kwa uchumi wa wilaya na kuchangia migogoro maeneo mbali mbali kujitokeza.

Alisema ili kuendana na mabadiliko hayo, mwanadamu anatakiwa kujiandaa kwa kuhakikisha kuwa anaanza kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji, kwa kufuata njia bora ikiwemo kilimo cha umwagiliaji na ufugaji wa mifugo michache.


Kwa wakati huo huo,mkuu huyo wa wilaya,ametoa shukrani za pekee kwa mashirika ya Forum CC, SEMA, kwa kutekeleza mradi huu ambao unachangia katika kuhamasisha wananchi kubadilika na kuanza kuendesha kilimo chenye manufaa, huku wakipambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

No comments:

Post a Comment