Monday, July 21, 2014

Vijiji vya Mgandu, Manyoni kunufaika na Mnara wa mawasiliano wa TTCL.

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa.(Picha na Maktaba).

Shirika la TTCL,linatarajia kutumia zaidi ya shilingi 503 milioni kugharamia ujenzi wa mnara wa mawasiliano katika kata ya Mgandu jimbo la Manyoni magharibi kabla ya oktoba 31 mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa yenye kumbukumbu no.WMST/GL/DOM.vol.3/01 ya mei 16 mwaka huu,mnara huo utanufaisha vijiji vya Itagata,Kalagali,Kayui,Makale na Mitundu.

Hayo yamesemwa juzi na mbunge wa jimbo la Manyoni magharibi,John Paulo Lwanji,wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Makale ulioitishwa kwa ajili ya naibu waziri wa maji,Amos Makala,kupokea kero za maji zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Hatua hiyo ya kujengwa kwa mnara huo,ni juhudi za kipekee za
mbunge Lwanji,ambaye amesema ujenzi wa miundo mbinu hiyo ya mawasiliano,unafanyika chini ya mfuko wa huduma za mawasiliano kwa wote.

“Ujio wa mnara huu,utaondoa kero kubwa ya upatikanaji wa mawasiliano katika vijiji vyetu vya kata ya Mgandu na vijiji jirani.Pamoja na mambo mengine,utachochea kwa kiasi kikubwa juhudi za wananchi kujiletea maendeleo ya kijamii nay a kiuchumi”alisema Lwanji na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi waliohudhuria mkutano huo.


Wakati huo huo,Lwanji alisema kuwa benki ya CRDB, inatarajia kuweka mashine za kutolea fedha za ATM katika vijiji vya Itigi,Mitundu na Makale wakati wo wote kuanzia sasa.

No comments:

Post a Comment