Thursday, July 17, 2014

Wanaume washiriki afya ya uzazi, jinsia kwa kusindikiza wake zao kliniki.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Joseph Sabore (anayeangalia kamera) akizungumza na maafisa wa shirika lisilo la kiserikali la Health Actions Promotion Association (HAPA), YMC na WaterAid Tanzania, ambao wako katika halmashauri hiyo kufanya tathimini ya mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia. Mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi 1.6 bilioni, unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na unatarajiwa kufikia ukingoni Desemba mwaka huu.


MRADI wa ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia (TMEP) unaotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Singida,umeanza kuzaa matunda yanayotarajiwa baada ya asilimia 89 ya wanaume kubadilika na kuanza kusindikiza wake zao kliniki na vituo vya afya.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Muuguzi Mkuu wa Halmashauri hiyo,Bertha Herman wakati akitoa taarifa yake ya ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia, kwa maafisa wa shirika lisilo la kiserikali la Health Actions Promotion Association (HAPA),YMC na WaterAid Tanzania,ambao wanafanya tathimini ya mradi huo wa miaka mitatu unaotarajiwa kumalizika desemba mwaka huu.

Amesema katika miaka ya nyuma ambayo ilikuwa imetawaliwa na mfumo kandamizi (mfumo dume),ilikuwa mwiko kwa mwanaume kumsindikiza mke wake kliniki au kumsaidia kazi za nyumbani ikiwemo ya kufua nguo za watoto,kuandaa chakula na kusafisha mazingira ya kaya yao.

Amesema mfumo huo kwa kiasi kikubwa ulipunguza mawasiliano baina ya mke na mume na ulijenga utamaduni wa kuwa mwanaume ana haki ya kumpa kipigo kikali mke pindi anapoona inafaa.

“Baada ya kuanzishwa kwa mradi huu miaka mitatu iliyopita,mambo yanaendelea kubadilika kwa kasi kubwa.Kwa sasa si rahisi kusikia mwanaume
amempiga mke wake.

“Wanaume wametambua kuwa wana wajibu wa kusindikiza wake zao kliniki kwa faida kwamba wanaweza kujua mapema kama kuna tatizo.Pia wanaume wengi sasa wanawapeleka watoto wao wachanga kliniki,kuwaogesha na kufua nguo zao.Kwa ujumla mradi huu umeboresha mno ndoa za wanafamilia wengi”,alifafanua.

Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Mtamaa Manispaa ya Singida,Mohammed Alute amesema elimu waliyoipata kupitia mradi wa TMEP, imesaidia mno wanandoa kushirikiana katika kutekeleza majukumu yote ya kifamilia ambayo hapo zamani,aliachiwa mwanamke peke na kuchangia kudhoofisha afya za akina mama.

“Kwa upande wangu na kwa kweli kwa wanaume wengi waliopata elimu inayotolewa na mradi wa TMEP,hatuoni kinyaa kupika chakula,kwenda kiliniki au kufua nguo za familia.Kumbe mwanamke akisaidiwa kazi za nyumbani,hachakai wale hazeeki upesi na kwa ujumla ushiriki huu,unaongeza mapenzi zaidi baina ya wana ndoa”,amesema Alute.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Joseph Sabore amesema mradi wa TMEP,umeleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa halmashauri hiyo ambapo sasa wanandoa wanaweza kukaa pamoja na kupanga utaratibu wa uzazi wa mpango kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Amesema wamejiandaa vema ili kuendeleza mradi huo wakati TMEP itakapoacha kusimamia utekelezaji wa mradi huo.Elimu na uhamasishaji utaendelezwa kwa jamii na katika shule za msingi,sekondari na vyuo.

Mradi huo unaotarajiwa kumalizika desemba mwaka huu,unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi 1.6 bilioni.

No comments:

Post a Comment