Thursday, August 21, 2014

Watu watano wakiwemo watatu wa familia moja,wameuawa Mkoani Singida.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, SACP, Geofrey Kamwela.

Watu watano wakiwemo watatu wa familia moja,wameuawa katika matukio tofauti,likiwemo la wanafamilia hao kukatwa katwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za miiili yao na watu wasiofahamika.

Tukio hilo la mauaji lililowahusisha wanandoa hao lilitokea siku tano baada ya kuuawa kikatili kwa wanandoa wengine wawili,Bwana Ramadhan Lyanga (80) na Bi Aziza Ali (62) wakazi wa wilayani Iramba.

Akielezea matukio hayo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, SACP, Geofrey Kamwela alisema katika tukio la kwanza  lililotokea juni,15,mwaka huu saa 11:00  jioni katika Kijiji cha Masagi,kata ya Mtoa,Tarafa ya Shelui,wilayani Iramba ambapo watu watatu,akiwemo mjukuu waliuawa.

Kwa mujibu wa kamanda huyo wa jeshi la polisi waliouawa ni pamoja na Mombasa Makala (65),mkewe Vaileth Mandi (52) na mjukuu wao Joyce  Augustino (7) anayesoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Masagi.

Hata hivyo Bwana Kamwela alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba watu hao
waliuawa nyumbani kwao kabla ya miili yao kugundulika kutokana na kuanza kuharibika,na kwamba inaonyesha pia kuwa wakati wa utekelezaji wa mauaji hayo kulikuwepo na purukushani kubwa kati ya marehemu na wauaji kwa kuwa damu zilitapakaa sehemu kubwa ya nyumba hiyo.

Aidha msemaji huyo wa jeshi la polisi aliweka wazi pia kwamba uchunguzi unaonyesha kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo wauaji waliibeba miili ya marehemu na kuiweka katika vyumba viwili tofauti na kuwaweka kitandani ambapo mwili wa Vaileth uliwekwa kitanda kimoja na mjukuu wao.

Kamanda Kamwela hata hivyo alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana na hata hivyo uchunguzi bado unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwanasa wauaji hao.

Katika tukio la pili lililotokea juni,15,mwaka huu saa moja jioni,katika barabara ya Heka – Manyoni,Kamanda Kamwela alisema Justina Joseph (58) mkazi wa Kijiji cha Jeje,kata ya Idodyandole,wilayani Manyoni alikufa baada ya gari alilokuwa akisafiria kuacha njia na kupinduka.

Aidha Kamanda huyo alisema gari hilo lenye namba za usajili T.551 ADB aina ya Toyota land cruicer lilikuwa likiendeshwa na Mchungaji wa Kanisa la TAG Manyoni,Bwana Mosses Chichola (58).

“Mchungaji huyo pamoja na abiria wake waliokuwa wakienda Manyoni mjini walipofika kwenye eneo ambalo lina kona kali ndipo ghafla alipomwona mpanda baiskeli akiwa barabarani na wakati akijaribu kumkwepa ndipo aliposhindwa kulimudu gari lake na hivyo kupinduka”,alisisitiza Kamanda huyo.

Katika tukio la tatu lililotokea juni,17,mwaka huu saa tatu asubuhi,Kamanda Kamwela alisema Musa Hamisi (40) mkazi wa Kijiji cha Msimi,kata ya Sepuka,wilaya ya Ikungi aliuawa na kisha kutumbukizwa kwenye bwawa la kunyweshea mifugo.

No comments:

Post a Comment