Tuesday, September 2, 2014

Afariki baada ya kutibiwa na daktari feki Singida.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela.

MKULIMA na mkazi wa kijiji cha Iyumbu tarafa ya Sepuka wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida,Jubulu Mahende,amefariki dunia muda mfupi baada ya kupewa matibabu na mtu anayedaiwa kuwa ni daktari feki.

Imedaiwa kuwa Jubulu aliyekuwa akisumbuliwa na kifua, kiuno na mgongo alizidishiwa dawa kitendo kilichopelekea hali yake kuwa mbaya zaidi.

Daktari huyo ambaye amekiri hana cheti cha aina yo yote kutoka vyuo vya afya,Prospa Simson,baada ya kubaini hali ya mteja wake inakuwa mbaya,alimpa
chupa tisa za maji,ili kuokoa maisha yake,lakini hata hivyo juhudi hizo hazikuzaa matunda.Pia alipatiwa vidonge sita ambavyo hata hivyo havijafahamika vilikuwa vinatibu maradhi gani.

Imedaiwa kuwa baada ya muda mfupi,Jubulu alipoteza maisha yake katika sebule ya nyumba ya mganga feki, Simson.

Kaimu  mganga mkuu wa wilaya ya Ikungi, Dk.Philip Kitundu alisema tukio hilo lilitokea Agosti 10 mwaka huu saa nne asubuhi kwenye vyumba maalumu vilivyotengwa na Simson kwa ajili ya kutolea huduma mbali mbali za matibabu.

“Tulipata taarifa ya tukio na agosti11mwaka  huu, tulienda kukagua duka la dawa ambalo lilisadikika lilitibu Jubulu ambaye alifia pale pale dukani”alifafanua.

Akifafanua zaidi,alisema walipolikagua duka hilo,waligundua kuwa Simon hakuwa na leseni kutoka TFDA ya kumruhusu kufanya biashara ya kuuza dawa kwa ajili ya binadamu.Pia yeye mwenyewe Simon,alikiri kuwa hakuwa na cheti  cha chuo chochote alichosomea utaalamu huo.

“Hata tulipopekuwa pekua dukani tulikuta madawa ambayo hayaruhusiwi kabisa kwenye maduka ya dawa muhimu,tulikuta madawa ya sindano,madawa ya vidonda,alikuwa anafunga vidonda,analaza,anatoa huduma za kujifungua kwa akina mama wajawazito”alisema Dk.Kitundu.

Aliongeza kwamba katika ukaguzi huo walikuta pia dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi. Tukio hilo la watu kupoteza maisha yao ni la tatu kutokea kwa watu waliopatiwa matibabu katika duka hilo isipokuwa matukio mawili yalitokea nje ya duka hilo.

 Kwa upande wake daktari huyo bandia,Dk.Prospa Simson licha ya kukiri kumpokea mgonjwa huyo akiwa na hali mbaya na kwamba baada ya kuchukua historia yake aligundua kuwa alikuwa akisumbuliwa na kifua na kwamba kabla ya kupelekwa kwake, alianza matibabau kwa waganga wa tiba asilia.

Kwa upande wake mtoto wa marehemu, Jilala Jibulu, alisema siku ya tukio asubuhi alikwenda kumsalimia baba yake na kumkuta akiwa na hali mbaya na ndipo alipoamua kumpeleka kwenye duka hilo la madawa,na muda mfupi alifariki akipatiwa matibabu.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,SACP Geofrey Kamwela,amekiri kutokea kwa tukio hilo.

Alisema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kama muuza duka hilo la madawa, ndiye alikuwa akimtibu au alienda dukani hapo kununua dawa alizoandikiwa na daktari mwingine.

No comments:

Post a Comment