Tuesday, September 16, 2014

Serikali ijenge mazingira rafiki kwa majengo yote ya kusomea ili kuwasaidia walemavu – TASI.

Katibu wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini, TASI, Ziada Msembo (kulia) akimkabidhi mwalimu wa wanafunzi walemavu wakiwakiwemo Albino shule ya msingi Ikungi mchanganyiko, Donard Bilali  vitabu vya sheria zinazowahusu walemavu.
Katibu wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) nchini, Ziada Msembo akimkabidhi losheni ya kujikinga na miale ya jua mwanafunzi mwenye ulemavu wa ngozi (Albino) wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko.
Katibu wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) nchini, Ziada Msembo (wa kwanza kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya walimu wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko.


HALMASHAURI  za wilaya, manispaa na majiji nchini zimeshauriwa kujenga/kukarabati  majengo yawe ya  mazingira rafiki kuanzia shule zote za msingi hadi vyuo, ili kuwavutia watoto wenye ulemavu mbalimbali wakiwemo vipofu kujiendeleza kielimu.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na katibu wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi (albino)  TASI nchini, Ziada Msembo, wakati akizungumza muda mfupi baada ya kutoa msaada wa vitabu vya sheria zinazowahusu walemavu  na lotion kwa albino wanafunzi wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilayani Ikungi.

Alisema sheria zilizopo, zinamtaka kila mtoto awe na ulemavu wa aina mbalimbali au asiwe na ulemavu wo wote,wanapaswa kupata elimu kadri ya uwezo wao….ni haki yao ya msingi.

Akifafanua, Zaida alisema watoto wengi wenye ulemavu mbalimbali nchini,wanashindwa kupata haki yao hiyo ya msingi kutokana na majengo mengi kuanzia shule za msingi hadi vyuo,kutokuwa rafiki kwao.

“Tunaziomba halmashauri zote nchini,kujenga/kuboresha majengo ya shule na vyuo, yawe na mazingira rafiki kwa wanafunzi wote wenye ulemavu na wasio na ulemavu,ili wanafunzi waweze kujiendeleza kielimu bila matatizo yo yote”,alifafanua zaidi katibu huyo.

Katika hatua nyingine, Ziada ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wazazi/walezi kuacha tabia ya kuwaficha majumbani watoto wao wenye ulemavu wa aiana mbalimbali,na badala yake wawapeleke shuleni,ili waweze kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.

“Viongozi mbalimbali wa ngazi mbalimbali serikalini kuanzia kitongoji,madhehebu ya dini na wanasiasa, tusaidiane katika kuwaibua watoto wenye ulemavu na kuhakikisha wanawapeleka shule waweze kupata elimu itakayowasaidia kumudu maisha yao ya kila siku na familia zao.

Kuhusu msaada wa vitabu vya kisheria, Zaida alisema vitabu hivyo vimeandikwa katika lugha rahisi ya Kiswahili kwa lengo la kuelimisha jamii ikiwemo walemavu kwa urahisi zaidi.

Pamoja na msaada wa vitabu vya sheria, pia TASI, imetoa msaada wa losheni kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (Albino) katika shule hiyo ya msingi Ikungi mchanganyiko.

No comments:

Post a Comment