Sunday, October 19, 2014

Lissu akerwa na uongozi wa Chadema Singida kwa kumdodesha.

Mwenyekiti CHADEMA jimbo la kanda ya kati, Tundu Lissu, akihutubia wana CHADEMA na baadhi ya wakazi wa manispaa ya Singida kwenye viwanja vya Peoples mjini Singida.Tundu pamoja na mambo mengine, amewahimiza wananchi kuikataa rasimu ya katiba mpya kwa madai kwamba imechakachuliwa.

Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Singida,wakimsikiliza mwenyekiti CHADEMA jimbo la kanda ya kati na mbunge wa jimbo la Singida mashariki, Tundu Lissu, wakati akiwahutubia.

IDADI  ndogo ya wanachama na wasio wanachama wa CHADEMA waliohudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya mwenyekiti wa jimbo la kanda ya kati, Tundu Lissu, kuzungumza nao, ilimuudhi mgeni huyo rasmi na kutangaza kwamba viongozi wa CHADEMA Manispaa ya Singida, hawana sifa ya uongozi.

Tundu akionyesha kukerwa mno na mahudhurio hayo, alisema wananchi wa mji wa Singida kwa kipindi cha miaka sita, hawajapata viongozi wanaowastahiki.

“Haya maneno yaliyosemwa na viongozi wa CHADEMA manispaa ya Singida, kwamba wananachi wa mji huu, ni waoga kuhudhuria mikutano ya CHADEMA, ni
blaa blaa tupu na hayana ukweli wo wote.  Ningejua hali ingekuwa hivi, nisingekuja”,alisema kwa masikitiko.


Alisema wananchi wa manispaa ya Singida toka CHADEMA izaliwe, hawajawahi kupata viongozi wenye uwezo bora wa kuongoza, kuhamasisha na kuwaambia ukweli wa mambo yanayoendelea.

Akifafanua zaidi, Tundu alisema wananchi wa manispaa ya Singida, sio waoga kuhudhuria mikutano ya CHADEMA.  Mahudhurio mabovu ya leo, ni matunda ya maandalizi mabovu yaliyofanywa na viongozi wasio na sifa.

Katika hatua nyingine, Tundu ambaye ni mbunge wa jimbo la Singida mashariki, alitumia muda mwingi kumsifia baba wa taifa hayati Julius Nyerere, kwa kudai kwamba alikuwa ni mtu mwenye akili nyingi na alikuwa mwadilifu na hakuwa  mwizi.


“Mwalimu Julius alikuwa na hekima kweli kweli, lakini hata hivyo alikuwa si Mungu, alikuwa binadamu kama mimi na wewe.  Alikuwa kiongozi safi huwezi kumlingansiha na watoto wake hawa (marais waliomfuata)”,alisema.

Kuhusu rasimu ya katiba mpya, Tundu alisema rasimu hiyo siyo mpya ni ile ile ya mwaka 1962, isipokuwa imejaa mapambo  mapambo, ili kuwaghilibu wanachi.

“Rasimu ya katiba ingesema rais hana haki ya kumnyang’anya mtu ardhi, rais ni binadamu aliyefanya  makosa kama binadamu wengine, akikosa ashitakiwe. Mawaziri wasitokane na wabunge au iondoe nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya. Hiyo ningesema ni rasmu bora kwa usatawi wa watanzania” na kuongeza;


“Katiba mpya itakuwa ya ovyo kuliko hii ya sasa.  Katiba mpya huko mbele itatupelekea tupigane vita na wazanzibar.Nionavyo mimi ni kwamba Wazanzibar hawataipitisha kabisa, nina hofu na huku bara, bara kumejaa ujinga mwingi, kuna uwezekano mkubwa wa kupitishwa  rasimu hii ya katiba mpya”.

No comments:

Post a Comment