Tuesday, October 7, 2014

Mampando wakabidhiwa kituo na vyoo vya kisasa.

Meneja wa shirika la HAPA la mkoa wa Singida, David Mkanje, akiwa katika kutekeleza majukumu yake mbalimbali.

SHIRIKA lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya afya, maji na usafi wa mazingira (HAPA) la mkoa wa Singida, limetumia zaidi ya shilingi 15 milioni kujenga kituo cha ushauri na ujenzi wa vyoo bora katika kijiji cha Mampando kata ya Ntutu wilaya ya Ikungi.

Ujenzi wa kituo hicho cha aina yake katika wilaya ya Ikungi, umefadhiliwa na shirika la Health, Australian Tanzania (HAT) na kusimamiwa na shirika la HAPA.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi kituo hicho, Mkurugenzi wa HAPA, David Mkanje, ametoa wito kwa wakazi wa wilaya ya Ikungi, kujitokeza kwa wingi kufika katika kituo cha ushauri na ujenzi wa vyoo bora,ili kujifunza ujenzi huo ambao una faida nyingi.

Alisema kuwa  ujenzi wa vyoo bora una faida nyingi ambazo unaimarisha mazingira bora na pia
unapunguza uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

Katika hatua nyingine, Mkanje alisema mradi huo uliotekelezwa kwa kipindi cha mwaka jana ni matokeo ya uchunguzi wa awali uliofanywa na Shirika wakati wa ujenzi wa shule  ya Msingi katika kitongoji cha Mughumbu kilichopo katika kijijini cha Mampando.

Akifafanua,alisema kuwa katika uchunguzi huo, ulionesha upungufu mkubwa  wa vyoo katika kijiji cha Mampando hali iliyowalazimu kuanza mchakato wa kupata fedha kwa ajili ya  kujenga kituo cha ushauri.

Alisema lengo la mradi lilikuwa ni pamoja na kuboresha afya za jamii ya Mampando kupitia ujenzi wa vyoo bora na elimu siha, kujenga uwezo wa jamii katika kutekeleza na kuendeleza mradi kwa uhamasishaji na ujenzi wa vyoo bora na elimu siha.

Mkanje alisema pia kujenga uwezo kwa baadhi ya vijana juu ya mbinu za ujenzi wa vyoo  bora na elimu siha  ili waweze kusaidia jamii kuondokana na tatizo la kutokuwa na vyoo bora hapa katika kijiji hicho.

Kijiji cha Mampando kina kina jumla ya kaya 586 zenye jumla ya watu 3,517 kabla ya Mradi/Uhamasishaji kijiji kilikuwa na kaya zenye vyoo bora 81, kaya zenye vyoo vya muda 396 na kaya zisizo na vyoo 109.

Kijiji cha Mampando kina jumla ya vitongoji nane (8) ambavyo ni Mampando A, Mampando B, Usandawi, Mughumbu, Mughuka, Kinyampundu, Ikokola na Makinginya.

Hata hivyo alisema baada ya kufanya Uhamasishaji kijiji kimekuwa na mabadiliko ambapo kaya zenye vyoo bora ni 121, kaya zenye vyoo vya muda 389, na kaya zisizo na vyoo 76.


“Hivyo kutokana na takwimu za hapo juu ninawapongeza wananchi wa kijiji cha Mampando kwa kuielewa vizuri na kuipokea elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira na ninaamini hata wale wasio na vyoo kabisa na wale walio na vyoo vya muda wataendelea kupokea elimu kutoka kwa wahamasishaji waliopata mafunzo kutoka kwa wataalam wa Shirika la HAPA na watabadilika tu.” Alisema Mkanje.

No comments:

Post a Comment