Sunday, October 19, 2014

Matere wabamiza timu inayokusanya michango ya maabara.

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, SACP,Geofrey Kamwela.

TIMU ya ukusanyaji michango kwa ajili ya ujenzi wa maabara kata ya Mwangeza wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida,imeshambuliwa na kujeruhiwa vibaya na baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Matere kijiji cha Dominiki.

Timu hiyo iliyokuwa inaongozwa na afisa mtendaji kata ya Mwangeza,Halfa Mrisho,imekubana na dhahama hiyo ikiwa kazini, oktoba mosi mwaka huu majira ya mchana huko katika kitongoji cha Matere kijiji cha Dominiki.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa Singida Blog, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama, James Mkwega, ametaja wengine waliojeruhiwa kuwa ni Mtendaji wa kijiji cha Dominiki, Juma Saidi, Afisa mifugo Joseph Doto, Mratibu elimu kata Saidi Nyika na Askari mgambo, Koyo Maduhu.

Alisema watendaji hao baada ya kujeruhiwa vibaya kwa silaha za jadi, walikimbizwa katika hospitali ya misheni ya Hydomu mkoa wa Manyara ambako wanaendelea na matibabu.

Akifafanua, alisema siku ya tukio watendaji hao wakiwa kazini kukusanya michango ya maabara, walivamiwa na watu ambao kuna kila dalili kwamba
waliandaliwa kwa ajili ya kuwadhuru.

“Pamoja na kupigwa vibaya ,pia walinyang’anywa fedha walizokuwa wamezikusanya, stakabadhi za kukusanyia michango na vile vile pikipiki zao ziliharibiwa vibaya”, alisema mwenyekiti huyo kwa masikitiko.

Mkwega alisema jeshi la polisi mkoa linamshikilia diwani wa kata ya Mwangeza kupitia tiketi ya CHADEMA, Peter Mlinga na baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Matere, kuhusiana na tuhuma ya kuwajeruhi watendaji hao.

Jeshi la polisi mkoa wa Singida, limekiri kutokea kwa tukio hilo na limedai kwamba litatoa taarifa baada ya kukamilika.

No comments:

Post a Comment