Tuesday, October 7, 2014

Mchungaji Singida awataka walemavu wasijinyanyapae.

Mkufunzi kutoka kituo cha Breli kilichoko chini ya kanisa la Pentekoste (FPCT) Tanzania, Ibrahimu Ikomba, akitoa maelezo muda mfupi kabla ya mafunzo ya siku tatu yaliyohusu ujasiriamali yaliyohudhuriwa na walemavu wa macho 60 wa mkoa wa Singida.
Mmoja wa wanasemina ya mafunzo ya ujasiriamali kwa walemavu wasioona, Potifa Sungi akisoma risala yao muda mfupi kabla mafunzo yao ya ujasiriamali hayajafungwa rasmi na mchungaji wa kanisa na FPCT, Amosi Maghasi.
Mchungaji wa kanisa la Pentekoste (FPCT) Kibaoni mjini Singida, Amosi Maghasi akizungumza kwenye ufungaji wa mafunzo ya siku tatu yaliyohudhuriwa na walemavu wa macho 60 wa mkoa wa Singida.Mafunzo hayo yalifanyika kwenye kanisa la Pentekoste Kibaoni.

Baadhi ya walemavu 60 wa macho waliohudhuria mafunzo ya ujasiriamali na mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU. Mafunzo hayo yalifanyika kwenye kanisa la Pentekoste Kibaoni.

WALEMAVU mkoani Singida, wameshauriwa kutojinyanyapaa na badala yake wajiamini kwamba wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi halali, zitakazowapatia kipato kitakachowawezesha kuishi maisha bora wao pamoja na familia zao.

Wito huo umetolewa na Mchungaji wa kanisa la Pentekoste (FPCT) Kibaoni manispaa ya Singida, Amosi Maghasi wakati akifunga mafunzo ya ujasiriamali yaliyohudhuriwa na walemavu 60 wasioona wa mkoa wa Singida.

Alisema mbele ya Mungu ,binadamu aliye mlemavu na yule asiye na ulemavu, wote wana thamani sawa.

Mchungaji Maghasi alisema kutokana na ukweli huo, mtu mwenye ulemavu anayo fursa sawa na asiye na ulemavu katika  kujiletea maendeleo kadri ya uwezo wake utakavyomruhusu.

“Mimi naomba niwatie moyo kwamba mlemavu hakuumbwa kuwa mtu wa kuomba omba. Mkijiendeleza kielimu, mtajijengea mazingira mazuri ya kujiajiri na kuajiriwa”, alifafanua mchungaji huyo.

Katika hatua nyingine, amewaomba watenge muda kwa ajili ya kuliombea Bunge Maalum la Katiba,ili liweze kuwapatia Watanzania Katiba itakayokidhi mahitaji yao kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50 ijayo.

“Mimi siwezi kuwahimiza kujiunga na vyama vya siasa kwa sababu mimi hapa nilipo, sio mwanachama wa chama chochote cha siasa., Lakini endapo ninyi wenyewe mtavutiwa  kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa, basi huko nendeni mkawe washauri wazuri na msiwe miongoni mwa wanachama wanaochochea migogoro na vitendo vinavyoashiria uvunjivu wa amani”, alifafanua.

Wakati huo huo,mchungaji Maghasi, ametumia fursa hiyo kuwaahidi walemavu hao kuwa majengo yote ya makanisa ya Pentekoste (FPCT) mkoani Singida, yatakuwa na mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu.


Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo, Ibrahimu Ikomba alisema katika siku tatu za mafunzo, walemavu hao wamefunzo juu ya uendeshaji wa ujasiriamali wenye tija na pia mbinu za kujiepusha na maambukizi ya VVU.

No comments:

Post a Comment