Wednesday, October 8, 2014

Mwalimu achomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, SACP, Geofrey Kamwela.

WATU wawili mkoani Singida wamefariki dunia katika matukio tofauti, likiwemo la Mwalimu wa shule ya msingi Kigogo jijini Dar-es-salaam, Hawa Idd  (34) baada ya kuchomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na mdogo wake Ramadhan Iddi (24) anayedaiwa kuwa na matatizo ya akili.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, SACP, Geofrey Kamwela alisema tukio hilo limetokea Septemba 23 mwaka huu saa 9.30 alasiri huko katika hospitali ya mkoa mjini Singida.

Alisema Septemba 22 mwaka huu  saa 5.30 asubuhi  kijana Ramadhan ilidaiwa alitoka nyumbani kwao kwa mazingira ya kutatanisha na ndipo mwalimu Hawa ambaye alikuja kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya mdogo wake huyo,walianza msako wa kumtafuta katika maeneo mbalimbali mjini Singida.

“Baada ya kumtafuta katika mitaa mbalimbali hapa mjini na kumkosa, Hawa alirejea nyumbani kwao Kibaoni na kumkuta mdogo wake Ramadhan,ameisha rejea nyumbani. Haikuchukua muda wanandugu hao walianza
kulumbana kitendo kilichosababisha Ramadhan kuchomoa kisu kutoka kwenye mfuko wake wa suruali na kumchoma dada yake tumboni, kichwani na kwenye mkono wa kushoto”, alisema Kamwela.

Kamanda huyo alisema Hawa aliweza kupiga yowe na majirani walifika mara moja na kumkimbiza hospitali ya mkoa ambako alifariki dunia kesho yake alasiri wakati akiendelea na matibabu.

Katika tukio jingine, Kamwela alisema Mchiwa Jeremia (22) mkazi wa kijiji cha Ipanduka tarafa ya Konko wilaya ya Manyoni, amefariki dunia Septemba 22 mwaka huu saa moja asubuhi baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali akidaiwa kuiba shilingi 115,000.

Alisema Septemba 21 mwaka huu saa tisa alasiri Mchiwa anadaiwa kuvunja nyumba ya Lukeresha Mdashi na kuiba kiasi hicho cha fedha.

“Kwa sasa tunamshikilia Lukeresha kwa mahojioano zaidi na pindi yatakapomalizika,mtuhumiwa tunatarajia kumfikisha mahakamani”,alisema.

No comments:

Post a Comment