Tuesday, October 7, 2014

Subirini kupiga kura, sio kuandamana waambiwa Singida.

Baadhi ya magari ya jeshi la polisi mkoa wa Singida, yakiwa yamebeba askari kwa ajili ya kuzuia maandamano ya wanachama wa CHADEMA ya kupiga kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba. Hadi tunakwenda mtamboni,wanachama hao pamoja na mabango yao walishitukia nguvu ya polisi na kufuta maandamano hayo.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) manispaa ya Singida,wakiwa nje ya ofisi ya CHADEMA mkoa Singida mjini kwa kusudio la kufanya maandamo ya amani kwa ajili ya kutoa ujumbe kuwa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea hivi sasa ni batili. Maandamano hayo hayakufanikiwa kwa kile kilichodaiwa kuwa yakuwa na kibali halali. Ilidaiwa zaidi ya wanachama 200 wangeshiriki maandamano hayo kuanzia ofisi ya CHADEMA mkoa hadi bomani kupitia viwanja vya Peoples.


KAMANDA wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,SACP,Geofrey Kamwela amewashauri wananchi kuacha kupoteza muda wao bure kushiriki maandamano ya kupinga Bunge Maalum la Katiba na badala yake wasubiri kipindi cha kupiga kura ndipo watoe maamuzi yao sahihi juu ya katiba wanayoitaka.

Alisema kuwa maandamano kwa sasa hayawezi kuleta tija yoyote kwa madai kwamba  pamoja na mambo mengine, kuna baadhi ya  Watanzania wako mahakamani kupinga bunge hilo.

“Huko barabarani kamwe hakutamwongezea muandamaji ugali,mbali ni kupoteza muda bure ambao ungeweza kutumika  katika kuchapa kazi halali zinazoongeza kipato kwa mhusika”, alifafanua.


Kamanda Kamwela ametoa ushauri huo wa bure wakati akitoa ufafanuzi juu ya kumhoji mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Singida, Shaban Limu kwa saa zaidi ya nne wakimtuhumu kuhamasisha wanachama wa CHADEMA waandamane bila kibali kwa lengo la kushinikiza kusimamishwa kwa shughuli za Bunge Maalum la Katiba.

Alisema bunge hilo maalum la Katiba, lipo pale kisheria kwa hali hiyo kudai kwamba maandamano yanaweza kuchangia bunge hilo kusimama au kusitisha shughuli zake  kwa vile Singida watu wameandamana ni ndoto za mchana  na ni jambo lisilowezekana.

Kuhusu mwenyekiti Limu, alisema kuwa baada ya kumhoji na kujiridhisha,walimwachia huru na bila masharti yoyote.

Kamwela ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi na viongozi wakiwemo wa kisiasa,kujenga utamaduni wa kusoma kwa kina katiba katika vipengele vyote,ili kuondoa uwezekano wa kuitafisiri vibaya.

Kwa upande wake Mwenyekiti Limu, amesema kuwa kitendo cha kukamatwa yeye akituhumiwa kuhamasisha maandamano ni uonevu kwa vile maandamano ya juzi yaliandaliwa na ofisi ya CHADEMA wilaya ya Singida.


Wakati huo huo, CHADEMA mkoa wa Singida kinaendelea kuweka mipango vizuri ili waweze kuomba tena kibali kwa ajili ya kufanya maandamano ya amani kupinga bunge hilo kwa vile linafanya shughuli zake kinyume na matakwa ya wananchi.

No comments:

Post a Comment