Friday, November 28, 2014

CHADEMA walia kuchezewa rafu Singida Kaskazini.


Mjumbe wa kamati ya utendaji CHADEMA jimbo la Singida kaskazini,Theodory Hango,(kulia anayeangalia kamera) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya CHADEMA kulaani vikali ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea nchini kote.Hango amedai CCM wameanza mchezo mbaya dhidi ya CHADEMA  ikiwa ni pamoja na kukaa kutoa fomu kwa waombaji uongozi kutoka CHADEMA,hadi waonyeshe stakabadhi za kulipa michango ya ujenzi wa maabara. Kulia ni mwenyekiti Elia Sima,mwenyekiti wa jimbo la Singida kaskazini.

CHAMA cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) jimbo la Singida kaskazini,kimeanza kulia kuchezewa mchezo mchafu na CCM kwenye mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea nchini kote.

CHADEMA kimedai kwamba baadhi ya waombaji wa nafasi mbalimbali za uongozi katika serikali za mitaa,wananyimwa fomu hadi waonyeshe stakabadhi ya kulipa michango ya ujenzi wa maabara.

Chama hicho ambacho kimejisifu kwamba kwa sasa ni mwiba mkali kwa CCM jimbo la Singida kaskazini,kimedai CCM kimeanza kutoa rushwa kwa baadhi ya waombaji wa CHADEMA,ili
wajitoe kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Baadhi ya wagombea hao kuhongwa,wameagizwa wasirejeshe fomu,wajitoe dakika za majeruhi au wakirejesha,waje wajitoe kabla ya uchaguzi kufanyika desemba 14 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari,mjumbe wa kamati ya utendaji CHADEMA jimbo la Singida kaskazini,Theodory Hango,alitaja baadhi ya vijiji vilivyoathirika na vitendo vya rushwa inayotolewa na CCM,kuwa ni Ng’ongwapoku,Sefunga,vijiji vya kata ya Marama na kata ya Kinyagigi.

“Upuuzi na uharamia huu unaoendelea ambapo viongozi wa CCM na washiriki wake wanaendeleza mikakati yao hiyo ya kishetani ya kuwarubuni kwa fedha na ahadi nyingine wagombea wetu wanaoonekana ni tishio kwao”,alisema Hango.

Aidha,mjumbe huyo alitoa tuhuma nyingine kwamba msimamizi wa uchagzui mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Singida vijijini,alibadilisha kinyemela kituo cha uandikishaji cha Mdimanyanu bila kutoa taarifa kwa umma.

“Uchafu mwingi unaofanywa na CCM dhidi ya CHADEMA,unaashiria dalili za dhahiri kwamba uchaguzi huu inawezekana usiwe huru na wa haki.Uchafu huu ukiendelea,tutaingia kwenye vurugu zitakazosababisha amani yetu kuwa shakani”,alifafanua Hango.

Hango alipoulizwa kama malalamiko yao wameyafikisha kwa maandishi kwa msimamizi wa uchaguzi,alisema kuwa walikuwa hawaja yapeleka mahali po pote kwa madai kwamba muda huo hawana kwa sababu muda wote (mchana na usiku) wako ‘site’,wanasimamia waombaji wao.

Wakati huo huo,Hango alisema CHADEMA kimejipanga vema kuigara garaza CCM katika nafasi ya ubunge kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.


“Makamanda saba wa CHADEMA,tumeonyesha nia ya dhati ya kulikomboa jimbo la Singida kaskazini kutoka kwenye mikono ya CCM kwa nafasi ya ubunge.Jimbo letu hili kwa sasa lipo nyuma kimaendeleo.Lengo letu ni kuja kulipaisha kimaendeo na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kero mbalimbali zinazowasibu wananchi wa jimbo hilo”,alisema Hango.

No comments:

Post a Comment