Thursday, November 6, 2014

Kikongwe apigwa risasi na polisi na kufariki dunia.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, SACP, Geofrey Kamwela.

KIKONGWE mmoja mkazi wa kitongoji cha Ilolo kata ya Iglansoni tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi, Joyce Maragabu (65),amefariki dunia baada ya kupigwa kwa risasi na askari polisi waliokuwa wakijihami dhidi ya kundi kubwa la wananchi waliokuwa wakitaka kuwavamia,ili wasiweze kumkamata mhalifu.

Askari hao walikuwa wakitaka kumkamata Nkida Gwisu, aliyekuwa akituhumiwa kumshambulia mtu mwingine.

Kikongwe huyo alipigwa risasi kichwani wakati akiwa anaendelea
kufua nguo zake na katika viwanja vya nyumbani kwake,na kufariki papo hapo.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, SACP, Geofrey Kamwela, alisema kuwa tukio hilo limetokea oktoba 16 mwaka huu saa sita mchana, katika kitongoji cha Ilolo kijiji na kata ya Iglansoni.

Alisema siku ya tukio, askari polisi wawili wa kituo kidogo cha polisi Ihanja, walienda  katika kitongoji hicho kwa ajili ya kutoa ulinzi kwenye mnada.

Wakati wakiendelea na majukumu yao,walipewa taarifa juu ya mtuhumiwa Nkida, kumshambulia mwanakijiji mwenzake.

Akifafanua,Kamwela alisema kwa bahati nzuri alitokea mwananchi moja ambaye alidai kumfahamu mtuhumiwa Nkida na mtu huyo alifanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa kwa urahisi.

“Baada ya kukamatwa,mtuhumiwa alianza kufanya vurugu na ndipo lilipotokea kundi kubwa la watu wakiwa na silaha mbalimbali za jadi ambazo ni mawe, mishale, fimbo na mapanga na kuanza kumshambulia askari polisi aliyekuwa akimshikilia Nkida”, alisema kamanda huyo.

Akifafanua zaidi,alisema kuwa katika hali ya kutaka kumuokoa mwenzake, askari polisi aliyekuwa na bunduki ya risasi za moto,alifyatua risasi moja hewani kwa lengo la kutawanya kundi hilo lisiendelee kumushambulia mwenzake.Hata hivyo katika purukushani hizo,ndipo risasi moja ilifyatuka na kumpiga kichwani marehemu aliyekuwa anafua nguo nyumbani kwake na kufariki papo hapo.

Kamwela alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo la mauaji ya kikongwe huyo,wananchi hao walivamia pikipiki ya polisi iliyokuwa ikitumiwa na askari hao T.PT 3242 aina ya Yamaha na kuichoma moto na kuiteketeza kabisa.

“Polisi hao walijeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao kwa kushambuliwa na silaha hizo za jadi.

Kutokana na tukio hilo,jeshi la polisi linawashikilia askari hao kwa mahojiano zaidi ili kujua chanzo cha vurugu pamoja na mauaji hayo.

Kamanda Kamwela ametoa wito kwa wananchi kuachana na vitendo vya kujichukulia sheria mikononi mwao kwa kuwa huko ni kuongeza matukio ya uvunjaji wa sheria na kupelekea madhara makubwa kutokana na kutokujua ukweli hali kuhusu tukio husika.Vitendo hivyo ni sawa na kutoa hukumu pasipo kuwa na uthibitisho wala mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment