Thursday, November 6, 2014

Viongozi wa dini, wanasiasa waombwa kusaidia kufanikisha chanjo ya Surua na Rubella.

Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi, akifungua kikao cha uhabarisho wa chanjo mpya ya Surua na Rubella wilayani humo. Dc Mlozi pamoja na mambo mengine, ameagiza viongozi wa madhehebu ya dini na wale wa kisiasa, kushiriki kikamilifu zoezi hilo la kitaifa linalotarajiwa kuanza Okt. 18 hadi 24 mwaka huu. Jumla ya watoto 103,879 wilayani humo, wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo. Kulia ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Mwendahasara Maganga.
Mratibu wa chanjo halmashauri ya wilaya ya Singida, Emmanuel  Mawi, akitoa mada yake ya uhabarisho juu ya chanjo mpya ya Surua na Rubella inayotarajiwa kuanza kutolewa kuanzia Okt. 18 hadi 24 mwaka huu nchini kote.

Mkuu wa wilaya ya Singida, Queen Mlozi akifuatilia mada juu ya uhabarisho wa chanjo mpya ya Surua na Rubella wakati kikao cha uhabarisho huo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo. Wa pili kushoto ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Mwendahasara Maganga.
Baadhi ya wanakamati wa uraghabishi na uhamasishaji wa masuala ya chanjo mpya ya surua na rubella wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa kwenye kikao cha uhabarisho.

SERIKALI  ya wilaya ya Singida, imewahimiza viongozi wa madhehebu ya dini na wa kisiasa kutoa ushirikiano wa karibu wakati wa kampeni ya kitaifa ya chanjo mpya ya Surua na Rubella inayotarajiwa kuanza Oktoba 18-24 mwaka huu nchini kote.

Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya hiyo Queen Mlozi, wakati akifungua semina ya uhabarisho juu ya chanjo hiyo, iiyohudhuriwa na kamati ya uraghabishi na uhamasishaji wa jamii wilayani humo.

Alisema Viongozi wa madhehebu ya dini na wale wa kisiasa, endapo watashiriki kikamilifu, lengo la kuchanja watoto 103,879, wilayani humo,litafikiwa kwa asilimia mia moja.

Mlozi alisema zoezi hili ni tofauti na mazoezi yaliyopita, walengwa wa safari hii ni kuanzia umri wa miezi tisa hadi chini ya miaka 15.  Watapatiwa chanjo mpya ya MR (Meales and Rubella).


Kwa upande wake Mratibu wa chanjo halmashauri ya wilaya ya Singida, Emanuel Mawi, alisema zoezi hilo litaambatana na utoaji dawa za vitamini A kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi 59.

Alitaja dawa zingine zitakazo tolea kuwa ni za minyoo (Mebendazole) kwa watoto wa umri wa miezi 12 hadi 59, dawa ya minyoo (Albendazole) kwa watoto wenye umri wa miaka 5 na kuendelea na dawa ya mabusha na matende.

Akisisaitiza, alisema “Kwa kuwa baadhi ya walengwa wanapatikana shuleni, idaya ya afya na idara ya elimu wilaya kwa pamoja zimeshiriki katika mafunzo, ya namna zoezi litakavyokuwa na kuandaa mikakati  ya kuhakikisha kuwa walengwa wote wanafikiwa”.

Kuhusu ugonjwa wa Rubella, Mawi alisema ugonjwa huo unaofanana sana na ugonjwa wa surua,huwapata zaidi watoto walio na umri wa chini ya miaka 15.


“Mtoto anapopatwa na ugonjwa huu, huweza kumsababishia matatizo mengi ikiwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu, upofu, utosikia, utindio wa ubongo, pia endapo mama mjamzito atakuwa na vimelea vya ugonjwa huu, anakuwa na uwezekano mkubwa wa kuzaa mtoto mfu, ama mwenye ulemamvu”, alisema Mawi.


No comments:

Post a Comment