Tuesday, November 11, 2014

Wanafunzi waaswa kutokufaulu kidato cha nne, sio kufeli maisha.

Rais wa shirikisho la wachimba madini Tanzania na mgeni rasmi wa mahafali ya sita ya shule ya sekondari kata Mandewa,John Bina,akizungumza kwenye mahafali hayo. Kulia ni mwenyekiti wa bodi ya shule ya sekondari ya Mandewa.Bahati Shagama na kushoto ni mkuu wa  wa shule hiyo, Margreth Missanga.
Mkuu wa shule ya sekondari kata ya Mandewa manispaa ya Singida, Margreth Missanga, akitoa taarifa yake kwenye mahafali ya sita ya wahitimu wa kidato cha nne yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo. Kulia ni rais wa shirikisho la wachimba madini Tanzania (mgeni rasmi) John Bina, na Kushoto mwalimu wa shule hiyo.
Rais wa shirikisho la wachimba madini Tanzania, John Bina akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari kata ya Mandewa mjini Singida,wakati wa mahafali ya sita.

Rais wa shirikisho la wachimba madini Tanzania, John Bina (wa tatu kulia) akishiriki kutoa burudani kwenye mahafali ya sita ya wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari kata Mandewa.Wa kwanza kushoto ni mkuu wa shule ya sekondari kata ya Mandewa, Margreth Missanga na wa pili kulia ni mwandishi wa habari wa gazeti la Jambo Leo mkoa wa Singida, Hillary Shoo.
Rais wa shirikisho ya wachimba madini Tanzania, John Bina, akichangia shilingi laki tano taslimu kwa ajili ya ujenzi wa choo cha walimu wa shule ya sekondari kata ya Mandewa manispaa ya Singida.
Baadhi ya wahitimu wa kidato cha nne wakiwa kwenye mahafali yao ya sita ya kumaliza kidato cha nne.
Mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne katika shule ya sekondari kata Mandewa,akipongezwa na dada yake kwenye mahafali ya sita ya shule hiyo.

RAIS wa shirikisho la wachimba madini Tanzania, John Bina amewataka wanafunzi ambao hawatafaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka huu,wasikate tamaa kwa madai kwamba yapo mambo mengi wanaweza kufanya kwa maendeleo yao ikiwemo kujiunga na vyuo vya VETA.

Bina aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye mahafali ya sita ya wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari Mandewa mjini Singida.

Alisema kutokufaulu mtihani wa kidato cha nne,hakumaanishi kuwa mhusika amefeli kabisa katika maisha yake hapana, mhusika akijiamini, kujituma kwa bidii na kujiwekea malengo ya kujiendeleza kielimu atafika mbali kielimu.


“Ukijiamini na kujituma zaidi ipo siku utafanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne na mingine yote katika safari ya kusaka elimu bora. Pia vipo vyuo mbalimbali ikiwemo vya VETA mahali mwanafunzi ambaye hakufanya vizuri kwenye mtihani wa kidato cha nne anaweza akajiendeleza vizuri tu”, alifafanua Bina.

Katika hatua nyingine, Rais huyo aliwataka wanafunzi hao wasidanganyike na maisha ya anasa za dunia hii,kwani yatawapeleka mahali pabaya. Kumbukeni kwamba dunia ni uwanja wa fujo,kuna UKIMWI,madawa ya kulevya na makundi mabaya.

Aidha, Bina aliwataka wawe makini na kujihadhari na vitendo hivyo na watumie elimu waliyoipata kwa manufaa yao, familia, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla.

Wakati huo huo, Rais Bina, alitoa msaada wa shilingi laki tano taslimu na tripu kumi za mchanga kwa ajili ya ujenzi wa choo cha walimu. Kwa sasa walimu 33 wa shule hiyo wanajisaidia katika choo cha canteen ya shule hiyo.

Awali mkuu wa shule hiyo,Margereth Missanga, alisema jumla ya wanafunzi 64 wanahitimu mwaka huu kati ya 104 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2011.


Missanga alisema kwa mwaka jana,wanafunzi sita wa shule hiyo wakiwemo wasichana wawili na wavulana wane,walifanikiwa kuendelea na kidato cha tano.Wengine wengi walifanikiwa kujiunga na vyuo mbalimbali ikiwemo vyuo vya ualimu,polisi,utumishi wa umma,uhasibu,unesi na VETA.

No comments:

Post a Comment