Wednesday, January 28, 2015

Ataka taarifa za matumizi zisomwe kujenga imani.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida, Bravo Lyapembile, katika picha.

MKURUGENZI  mtendaji wa halmashauri ya Mkalama  mkoani singida, Bravo Lyapambile, amewaagiza maafisa watendaji Kata kutoa/kusoma taarifa za michango mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa maabara kwa wakati,ili wananchi waendelee kuamini halmashauri yao.

Amesema kwa njia hiyo wananchi watajenga imani na Halmashauri yao kwamba michango yao inatumika kwa malengo yanayokusudiwa.

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na mwakilishi wa SingidaYetuBlog ofisini kwake juu ya maendeleo ya ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara katika kila Shule  19 za sekondari za kata za halmashauri hiyo

Bravo  alisema kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wa Kata, kwamba kwa
muda mrefu hawajapewa taarifa ya michango yao na hivyo kuzua hofu kwamba baadhi ya michango imeliwa na watendaji wa Kata.

“Malalamiko haya sijayapuuza, nimeyapokea na nimeanza kuyafanyia kazi. Kwanza nimeingiza kitengo cha ukaguzi wa mahesabu ya  ndani kuanza kukagua michango ya ujenzi wa maabara mara moja”,alisema.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya kazi hiyo kukamilika wananchi watapatiwa taarifa ya ukaguzi huo, watendaji watakaobainika wametumia michango hiyo kwa matumizi yao binafsi, nitawashughulikia  ipasavyo  ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Katika hatua nyingine, Bravo amewapongeza wananchi kwa kuchangia ujenzi wa maabara na kuchangia Halmashauri hiyo mpya, kuongoza kati ya halmashauri za mkoa wa Singida kwa kufanya vizuri.

“Kwa kweli wananchi wa Halmashauri hii ya Mkalama, wanamwamko wa hali ya juu katika kuhakikisha Halmashauri yao inaenda mbio kimaendeleo, ili kuzipita halmashauri zingine zilizoanzishwa siku nyingi”alisema mkurugenzi huyo.

Aidha,Bravo  ametumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Mkuu wa Wilaya  hiyo Edward Ole Lenga  na  kamati za ujenzi kwa juhudi zao kubwa za kufanikisha ujenzi wa maabara ambapo kwa sasa  halmashauri ni ya  mfano wa kuigwa katika ujenzi huo.


Mkurugenzi huyo,alisema kwa sasa wanamalizia kazi ndogo ndogo zilizobakia ikiwemo kuweka  milango, madirisha na kupaka rangi katika maabara chache ambazo kazi haijakamilika kwa asilimia mia moja.

No comments:

Post a Comment