Tuesday, January 13, 2015

Breaking News…DED Iramba alipukiwa na bomu kitandani.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP.Thobias Sedoyeka, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Iramba , Halima Hanjali Peter (47) anusurika kuawa kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu la kutengenezwa kienyeji.

MKURUGENZI mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoa wa Singida,Halima Hanjalli Peter (47), amenusurika kifo kwa kitu kinachodhaniwa kuwa bomu kulipukia kitandani kwake.

Kamanda wa jweshi la polisi mkoa wa Singida, ACP  Thobias Sedoyeka, amesema tukio hilo limetokea leo  saa 1.15 asubuhi huko katika eneo la Kiomboi tarafa ya Kisiriri wilaya ya Iramba.

Alisema kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu la kutengenezwa kienyeji kililipuka na kusababisha madhara ikiwemo kutoboa godoro la spring kiasi cha nusu nchi kwenda chini na upana wa nchi mbili.Hata hivyo hakuna mtu/watu waliojeruhiwa katika mlipuko huo isipokuwa godoro na shuka.

Akifafanua,alisema kuwa Desemba 30 mwaka jana saa nne asubuhi Mkurugenzi huyo alipokea bahasha kutoka kwa sekretari wake ambapo ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na kadi ya kumpongeza na ndani yake kulikuwa na kikaratasi chenye ujumbe “poleni sana hatuwezi kufanya dili la
milioni 90 halafu mkala peke yenu sisi mkatudhulumu tukawaacha”.

Bi. Halima alipokuta ujumbe huo, aliamua kwenda na bahasha hiyo nyumbani kwake bila kujua kuna nini kingine ndani yake.

“Leo  saa 1.15 asubuhi akiwa anajiandaa kwenda kazini huku bahasha ameiweka juu ya kitanda chake akijiandaa kuondoka nayo, kitu kilichokuwa ndani ya bahasha hiyo kililipuka kwa kishindo”alifafanua zaidi.

Kamanda Sedoyeka alisema hadi sasa hakuna mtu/watu wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo na polisi kwa kushirikiana na wataalamu toka jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) na wataalamu wa milipuko,watafanya uchunguzi wa kitu hicho na kutoa majibu sahihi.Aidha,jeshi la polisi mkoa linaendelea na upelelezi ili kumpata mtu aliyetoa ile barua kwa hatua na uchunguzi zaidi.


Wakati huo huo, Sedoyeka ametoa wito kwa viongozi kuwa makini na bahasha,zawadi zinazofungaishwa ili kuepukana na madhara yanayoweza kusababishwa na milipuko inayoweka katika vitu hivyo.

No comments:

Post a Comment