Friday, January 2, 2015

Chadema Singida wapanga kumburuza mahakamani msimamizi wa uchaguzi.

Mjumbe wa kamati ya utendaji CHADEMA manispaa ya Singida, Vicent Mughwai (katikati) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya kusudio la chama hicho kumfungulia shitaka msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa manispaa ya Singida, kwa tuhuma ya kukiuka kanuni za uchaguzi huo. Vicent ndugu yake na mbunge wa jimbo la Singida mashariki na mnadhimu mkuu wa sheria CHADEMA, Tundu Lissu, ametangaza rasmi kumng’oa mbunge wa CCM jimbo la Singida mjini Mohammed Gullam Dewji, kwenye uchaguzi mkuu ujao. Kulia mjumbe wa kamati ya wilaya na katibu kata CHADEMA kata ya Unyambwa na kushoto ni mwenyekiti wa baraza la wazee wilaya CHADEMA Singida mjini.
Baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali CHADEMA manispaa ya Singida, wakiwa kwenye mkutano wa chama hicho na waandishi wa habari ambapo CHADEMA walitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongozi uliomalizika Desemba 14 mwaka huu.

Baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali waliohudhuria kikao kilichoitishwa na CHADEMA manispaa ya Singida kutangaza nia ya kumfikisha mahakamani msimamizi wa uchaguzi huo manispaa ya Singida, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya vitendo vya rushwa kwa ajili ya kukidhoofisha CHADEMA.

CHAMA  Cha Maendeleo na Demokrasia (CHEDEMA) halmashauri ya manispaa ya Singida, kinatarajia kumburuza mahakamani msimamizi wa uchaguzi wa serikali kutokana na tuhuma mbalimbali, ikiwemo ya uchakachuaji wa kura.

Hayo yamesemwa na mjumbe wa kamati ya utendaji CHEDEMA manispaa ya Singida,Vicent Mughwai,wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyohusu uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika Desemba 14 mwaka huu.

Alisema zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa manispaa ya Singida, kwa kiasi kikubwa haukufanyika kwa haki. Vitendo vya rushwa na ukiukwaji kuanzia uandikishwaji wa wapiga kura na ukiukwaji mkubwa wa kanuni za uchaguzi na wa kupata wagombea nafasi za uongozi na mchakato wa kupata viongozi na chaguzi mkuu.


Vicent alitaja baadhi ya vitendo vya ukiukwaji wa kanuni kuwa ni wasimamizi wa CHADEMA kuenguliwa kwenye nafasi ambazo walitaka kuja kuwatumikia wananchi kikamilifu, kwa lengo la  wagombea wa  CCM waweze kupita bila vikwazo vyovyote.

Mjumbe huyo alitaja vitendo vingine kuwa kada wa CCM kutumia gari kusomba watu na kuwapeleka kwenye vituo vya kupigia kura na wagombea wa CHADEMA kuzuiwa kuingia kwenye vyumba vya kuhesabia kura ili uchakachuaji uweze kufanyika kitendo ambacho ni kinyume na kanuni namba 22.

“Kutokana na ukiukwaji mkubwa wa kanuni za uchaguzi katika jimbo letu,tunaomba vyombo husika na serikali,vifanye uchunguzi wa kina na hatua kali zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika wana hatia”alisema.

Aidha, mjumbe huyo alisema CHADEMA inamwomba  Waziri wa TAMISEMI, amchukulie hatua kali msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa ambaye ni mkurugenzi wa manispaa ya Singida,kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kusimamia ipasavyo uchaguzi huo.


“Tunawasiliana na wanasheria wa chama chetu ili tuweze kuchukua hatua za kisheria kupinga matokeo yote  yaliyopatikana kutokana na ukiukwaji mkubwa wa kanuni.Lengo ni wapiga kura wetu waweze kutendewa haki”,alifafanua.

Kwa upande wa msimamizi wa uchaguzi serikali za mitaa manispaa ya Singida, Joseph Mchina, alisema CHADEMA  wanao haki ya kwenda mahakamani, ili waweze kupatiwa haki yao kama wanaamini kulikuwepo na ukiukwaji wa kanuni na vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo.


“Mahali ambapo wagombea wa CHADEMA hawakuruhusiwa kuingia kwenye vyumba vya kuhesabia kura, nafasi ilikuwa finyu lakini mawakala wao waliruhusiwa.Viongozi wa CHADEMA ambao walikuwa sio wagombea wala wasimamizi, kanuni hazitoi nafasi kwao kuingia kwenye vyumba vya kuhesabia kura,l akini wao walilazimisha waingie kitendo ambacho hakikubaliki”,alisema Mchina.

No comments:

Post a Comment