Thursday, January 22, 2015

Sina dhambi ya kuuawa na bomu, ang’aka DED Iramba

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoa wa Singida, Halima Mpita, akizungumza na waandishi wa habari juu ya bahasha iliyokuwa na bomu lililolenga kumuawa.

MKURUGENZI mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida,Halima Mpita aliyenusurika kuawa kwa bomu lililokuwa limehifadhiwa ndani ya bahasha,amefunguka na kudai kwamba anaamini hana dhambi ambayo inaweza kusababisha apewe adhabu ya kuawa kwa bomu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,Mkurugenzi huyo alisema ajuavyo yeye ni kwamba ndani na nje ya wilaya ya Iramba  hana adui wa kiwango cha kumsukuma adui huyo aweze kutumia njia ya kijasusi ya    bomu kukatisha maisha yake hapa duniani.

Alisema ujumbe alioukuta ndani ya bahasha iliyokuwa na bomu unaosema  kwamba amedhulumu watu/mtu dili ya  shilingi 90 mililoni,ni uwongo mtupu na umepitiliza.


“Mimi kama mkurugenzi,sina mafungu ya fedha yenye fedha nyingi kiasi ya kuwa na shilingi 90 milioni.Mafungu yenye fedha yako chini ya wakuu wa idara wanaosimamia miradi mbalimbali ya maendeleo.Mimi ni mwiizinishaji tu wa malipo,sasa hilo dili la milioni 90 nitalifanyaje wakati sina fungu la fedha za kiwango hicho”,alisema Mpita.

Alisema kwa sasa bado anaendelea kutafakari juu ya  maadui/adui huyo ambaye alidhamiria kumuawa kwa bomu, kwamba amemkosea nini au lengo lake hasa ni nini.

“Kwa muono wangu ni kwamba kuna mnyororo (chain) ya watu ambao nia yao kwangu sio nzuri.Nimechunguza bahasha hiyo ilivyotengenezwa na kifaa kilichokuwa na koili na nyaya za umeme,nimebaini kuwa kazi hiyo iliwachukua/ilimchukua mhusika muda mrefu sana kuikamilisha”alisema.

Akifafanua zaidi,mkurugenzi huyo alisema desemba 29 mwaka jana,watu waliokuwa wakisafiri na gari aina ya noah kutoka Singida kwenda Igunga,walikabidhi bahasha hiyo kwa askari wa usalama barabarani wa kituo kidogo cha Misigiri.

Mpita alisema siku hiyo hiyo askari polisi hao mnamo saa 12 jioni,walimpigia simu kuhakikisha endapo amepokea bahasha hilo walilopewa  na watu waliokuwa wanasafiri kwa kutumia noah.

Alisema desemba 30 mwaka jana baada ya kukabidhiwa na karani wake bahasha hilo ambalo lilikuwa zito kiasi,aliifungua na kukuta kadi ambayo ndani yake kulikuwa na  ujumbe unaodai kuwa amedhulumu shilingi 90 milioni. Vile vile kulikuwa na kitu kidogo kizito kilichokuwa na nyaya za umeme kilichokuwa kimefungashwa kwa kutumia selotape.

“Desemba 29 mwaka jana hadi januari mosi mwaka huu,nilikuwa nimebanwa mno na shughuli za kikazi kwa hiyo,sikuwa na muda wa kusoma kwa makini ujumbe uliokuwepo ndani ya bahasha iliyozungushiwa wino mzito na kufungwa kwa unadhimu.Na  sikuweza kukangua kamzingo kadogo ambacho kilikuwa na nyaya za umeme”,alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa kamzigo au kifurushi hicho cheye nyaya za umeme,alidhani ni mali ya  dereva wake lakini kikatumwa kupitia kwake na hakikuwa na ujumbe elekezi.

“Januari mbili mwaka huu asubuhi nikiwa najiandaa kwenda ofisini,kifurushi/kamzingo nilikaweka juu ya kitanda changu kwa lengo niondoke nacho nikamkabidhi dereva wangu. Lakini ghafla wakati naendelea na maandalizi,kililipuka kwa kwenda chini na kutoboa godoro langu la spring”,alisema Mpita.

Mkurugenzi huyo alisema anamshukuru sana Mungu kwa kitendo cha kutokujaribu kukifungua na kudai kwamba kama angejaribu kukifungua kwa wakati huo alipopewa,lingemlipukia kifuani na kwa sasa asingekuwepo duniani.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, uchunguzi wa mlipuko huo uliofanyika unaonyesha kuwa halikuwa bomu la kutengenezwa kienyeji kwa kuwa mtengenezaji alitumia vitu viwili tu ambavyo ni betri (power source ) na kilipuzi (detonator) na hiyo ndioa ilipelekea madhara kutokuwa makubwa.Bomu kamili linatakiwa kutengenezwa na mali ghafli zingine tatu.

Kwa sasa jeshi la polisi mkoa wa Singida,linashikilia watuhumiwa wanne wawili wakiwa ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Iramba,kuhusiana na jaribio hilo la kutaka kumuawa Mpita kwa bomu.

No comments:

Post a Comment