Thursday, January 22, 2015

Singida wafanikiwa kupunguza vifo vya uzazi.

Kaimu mganga mkuu mkoa wa Singida, Dk.Ernest Mgeta, akitoa taarifa yake kwenye uzinduzi mpango mkakati wa mkoa wa Singida wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aqua Vitae mjini Singida.Wa kwanza kushoto ni mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Vicent Kone na anayefuata ni kaimu katibu tawala mkoa wa Singida, Marando.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Vicent Kone  akizindua rasmi  mpango mkakati wa mkoa wa Singida wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aqua Vitae mjini hapa.
Baadhi ya viongozi na watendaji mkoa wa Singida waliohudhuria wadau uzinduzi mpango mkakati wa mkoa  Singida wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aqua Vitae mjini Singida.

MKOA wa Singida umefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 52 hadi 49 na vifo vya watoto wachanga wenye umri kuanzia siku ya kuzaliwa hadi siku ya 28, kutoka 182 hadi 178 kwa mwaka.

Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, wakati akizindua mpango mkakati wa mkoa wa kuongeza kasi ya kupunuza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aqua Vitae mjini Singida.

Alisema hata hivyo kwa takwimu hizo, kasi ya kupunguza vifo hivyo mkoani hapa bado ni ndogo sana katika kufikia malengo ya millennia ifikapo desemba mwaka huu.

Dk. Kone alisema Rais Kikwete mei 15 mwaka jana, alizindua mpango mkakati ulioboreshwa wa kitaifa wa kupunguza kasi ya vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi, ili kuchangia kufikia malengo ya millennia namba nne na tano.

Alisema katika uzinduzi huo,iliagizwa kuwa kila mkoa uandae mpango mkakati wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano.

Akifafanua, Dk.Kone alisema mipango hiyo iwe inayotekelezeka,inayopimika,inayozingatia mazingira mahususi na iliyo shirikishi.

“Pia kila mkoa uhakikishe unasimamia halmashauri zake zinatengneza sheria ndogo zinazoongoza utekelezaji wa mikakati hiyo katika ngazi za kata  na vijiji”,alisema.

Mkuu huyo wa mkoa, alisema ili mkoa utekeleze maagizo/maazimio hayo utaweka nguvu nyingi katika ufuatiliaji na utekelezaji utakaofanyika kwa njia mbalimbali mojawapo ni kwa kutumia kadi rafiki kwa ufuatiliaji huduma za afya ya mama na mtoto (score card).

“Teknolojia hii mpya ya kufuatilia huduma za mama na motto kwa kutumia kadi rafiki ambayo inaonesha maendeleo ya huduma kwa rangi ya kijani,njano na nyekundu.Kijani ni kiwango cha juu, njano, kiwango cha kati na nyukundu,kiwango duni”alifafanua.

Kauli mbiu ya mkakati wa mkoa wa Singida,ni “weka kipaumble,wekeza, timiza wajibu, okoa maisha”.

Kwa mujibu wa takwimu za “Tanzania Demographic and Healthy Survey (TDHS 2010, akina mama wapatao 454, hupoteza maisha kati ya vizazi hai 100,000,ikionesha mafanikio kidogo ukilinganisha na TDHS 2004/2005 ya vifo 578 kwa kila vizazi hai 100,000.

Kasi hii ni ndogo sana ukilinganisha na lengo la kitaifa la kufikia vifo 193 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo desemba mwaka huu.

Kwa upande wa vifo vya watoto takwimu zinaonyesha kuwa watoto wachanga wenye umri wa kuanzia siku ya kuzaliwa hadi siku ya 28,watoto wapatao 26 kati vizazi hai 1,000, hupoteza maisha.Hii ni sawa na watoto 42,343 kufariki dunia kwa mwaka.Nusu ya vifo hutokea ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa.

No comments:

Post a Comment