Wednesday, January 28, 2015

Singida yafanikiwa kupanda miti Mil 10

Afisa misitu sekretarieti mkoa wa Singida,Charles Kidua akisoma taarifa yake ya maendeleo ya upandaji miti mkoani Singida katika siku ya upandaji miti iliyofanyika (15/1/2015) kimkoa katika kijiji cha Nkinto wilaya ya Mkalama.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone (kushoto) akimwelekeza mwanafunzi wa shule ya msingi Nkinto wilaya ya Mkalama namna bora ya upandaji miti.Dk.Kone alishiriki upandaji miti katika siku ya upandaji miti kimkoa iliyofanyika katika kijiji cha Nkinto.

Mkuu wa wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida, Edward Ole Lenga, akipanda mti katika uzinduzi wa upandaji miti kimkoa uliofanyika katika kijiji cha Nkinto wilayani Mkalama.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Bravo Lyapembile, akishiriki upandaji miti katika siku ya upandaji miti kimkoa iliyofanyika katika kijiji cha Nkinto. 

MKOA  wa Singida umefanikiwa kupanda miti ya aina mbalimbali ipatayo 10,347, 870 sawa na asilimia 37 ya lengo la mkoa kupanda miti 27,500,000 kati ya mwaka 2010 na mwaka jana

Hata hivyo kwa mujibu wa wataalamu, asilimia 50 ya miti hiyo imekufa kutokanana uhaba wa mvua, kuliwa na mchwa, uharibifu wa binadamu na mifugo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dr. Parseko Kone, wakati akizungumza kwenye siku ya upandaji miti kimkoa ilifanyika katika kijiji cha Nkinto halmashauri ya wilaya ya Mkalama.

Alisema kutokana na mkoa kukabiliwa na tatizo la mvua haba, jitihada za kupanda miti huwa hazifikii malengo yanayokusudiwa.


“Hata hivyo hilo halitukatishi tamaa. Napenda kutoa wito kwamba tupande miti inayovumilia ukame, kutumia njia mbalimbali kwa vile pingili (cuttings) za mininga mikuyu na jamii zingine zote zinazokubali hali ya hewa ya mkoa wetu.

Aidha,mkuu huyo wa mkoa  alitaja baadhi ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mkoa katika kupambana na hali ya kuenea kwa jangwa, ambazo ni kuanzisha kampeni mbalimbali za upandaji miti ikiwemo kampeni ya msitu ni mali na msitu ni mazingira.

“Pia kampeni ya uhamasishaji wa kila kaya kupanda miti isiyopungua 10 na taasisi zenye matumizi maalumu ya miti, tunaziagiza kuanzisha mashamba yao ya miti,ili ziweze kujitosheleza kwa nishati hiyo”,alisema.


Katika hatua nyingine Dr. Kone ametoa wito juu ya umuhimu wa wananchi kuhakikisha wanahifadhi uoto wa asili uliopo kwa faida ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

“Kwa kuwa miti mingi tunayopanda inakufa ni vyema watu binafsi na vijiji watenge maeneo ya hifadhi za misitu ya uoto wa asili kwani hutoa kwa haraka”,alisema.

Kwa mujibu wa Dr. Kone, hadi sasa kuna vijiji 230 mkoa wa Singida  vyenye misitu ya asili ya ukubwa wa hekta zipatazo 520, 325.48.


Amesema misitu hiyo ya asili itumike kwa shughuli za ufugaji nyuki kibiashara, ili kumkomboa mwananchi kiuchumi.

No comments:

Post a Comment