Thursday, January 15, 2015

TRA mkoa wa Singida, yatoa msaada wa madawati shule ya msingi Isanzu wilaya Mkalama.

Meneja TRA mkoa wa Singida, Samson Jumbe (kushoto) akimkabidhi Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Isanzu wilaya ya Mkalama, Sadick Mbiro Abdallah, msaada wa madawati 25 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili. Katikati mwenye miwani ni Afisa elimu kwa umma (TRA),Zakaria.
Meneja wa mamlaka ya mapato (TRA) mkoa wa Singida, Samson Jumbe akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Isanzu iliyojengwa na Wajerumani mwaka 1934.Wanafunzi hao wamekalia madawati 25 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili yaliyotolewa msaada na TRA mkoa wa Singida.
Moja ya madarasa yaliyojengwa mwaka 1934 na Wajerumani ya shule ya msingi Isanzu wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida.Viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Iramba mashariki Mgana Msindai na David Holela aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ushirika wamesoma katika shule hiyo.Kwa sasa darasa hilo bado linaendelea kutumika.


Meneja wa mamlaka ya mapato (TRA) Tanzania mkoani Singida, Samsoni Jumbe,amewahimiza  viongozi/watendaji na watu wenye uwezo kiuchumi kujenga utamaduni  wa kushiriki ukarabati  majengo na miundombinu mingine ya shule/vyuo walikosomea, ili iendelee kuvutia kama ilivyokuwa wakati wa enzi zao.

Jumbe ametoa wito wakati akizungumza na uongozi wa shule ya msingi ya Isanzu Wilaya ya Mkalama, muda mfupi kabla hajakabidhi  madawati 25 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili.

Alisema uzoefu unaonyesha shule nyingi  pamoja na vyuo mbalimbali vilizojengwa miaka  mingi, vingi zimechakaa vibaya na majengo yake mengi hayafai kutumiwa na wanafunzi  na walimu.


Aidha, Jumbe alisema kuwa majengo na miundombinu mingine ya aina hiyo inafika mahali haivutii tena na yanakuwa ni hatari kwa usalama wa wanafunzi na walimu hao.

“Shule za Msingi walikopita viongozi wa ngazi  mbalimbali wakiwemo wa kitaifa na wabunge,  na wafanya biashara  wa ngazi mbalimbali, zimejengwa miaka mingi kama hii ya Isanzu iliyojengwa na Wajerumani mwaka 1934. Ni lazima zichakae kwa hiyo zinahitaji ukarabati  mkubwa ambao gharama zake kwa kawaida ni kubwa”,alifafanua meneja huyo.

Jumbe alisema viongozi waliosomea katika shule/vyuo hivyo hawana budi kushirikiana kwa karibu na uongozi wa shule /vyuo kutafuta fedha ikiwemo kwa kuandaa harambee kwa lengo la kupata fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo na miundombinu mingine na ununuzi wa madawati.


Awali mwalimu mkuu wa shule hiyo Sadick Mbiro Abdallah, alisema shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya  600, inahitaji madawati 204 yaliyopo ni 110 mapungufu ni dawati 94.

Katika hatua nyingine mwalimu Abdallah alisema shule hiyo ambayo imetoa wasomi wengi wakiwa ni akina Mgana Msindai  Mwenyekiti wa CCM  Mkoa wa Singida na  David Holela aliyewahi kuwa Naibu waziri wa ushirika, inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mwamko duni wa elimu kwa  wazazi/walezi wengi wa wanafunzi wa shule hiyo.

Akifafanua, alisema wazazi/walezi wengi wa wanafunnzi wa shule hiyo wamekuwa wakiwatisha watoto wao na kuwaagiza wahakikishe hawafaulu hasa mtihani wa Taifa wa Kumaliza elimu ya Msingi.

“Mwanafunzi anaweza kuwa na uwezo mzuri darasani kuanzia darasa la kwanza hadi la saba. Lakini utashangaa matokeo  ya mtihani wa Taifa na darasa wa darasa la saba   kwani, atafanya vibaya mno”,alifafanua.na kuongeza; “Hali hii inachangiwa na wazazi/walezi kuwaonya watoto wao kwamba wakifaulu kwenda sekondari watajisomesha wao wenyewe.


Kwa mujibu wa Mwalimu Abdallah mwaka juzi wanafunzi 15 kati ya 66 walifaulu mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana wanafunzi 10 kati ya 66 walifaulu mtihani wa Taifa wa Darasa la saba.

No comments:

Post a Comment