Friday, January 2, 2015

Walimu Singida waidai serikali mil 314/-

Baadhi ya wajumbe wa kikao cha mkoa cha kupangia shule wanafunzi waliofaulu mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu,ili kuanza kidato cha kwanza mwakani.Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kanisa Katoliki mjini Singida.

WALIMU mkoani Singida wanaidai serikali zaidi ya sh milioni 314 yakiwa ni malimbikizo ya madeni yao mbalimbali ya siku za nyuma kwa vipindi tofauti hadi kufikia Desemba mwaka huu.

Ofisa elimu wa mkoa wa Singida, Fatma Kilimia alisema mjini hapa mwishoni mwa wiki kuwa walimu mbalimbali wa shule za msingi na sekondari mkoani Singida walikuwa wanaidai serikali jumla ya sh milioni 390.5.

Alikiambia Kikao cha Bodi ya Uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza mwakani  kuwa baada ya halmashauri husika kufanya uhakiki wa kutosha, madeni yote yaliwasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa hatua zaidi lakini hadi sasa ni sh milioni 76.4 tu zimelipwa.

Kwa mujibu wa Kilimia, walimu wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi wanaidai serikali jumla ya sh milioni
69.9, halmashauri ya Manyoni sh milioni 62.3, Mkalama (81.5m/-) na halmashauri ya wilaya ya Singida (100.4).

 .Akichangia katika agenda hiyo ambayo ilihusu “Yatokanayo” na Kikao cha Desemba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi Celestine Yunde alisema kuwa kutokulipwa walimu hao fedha zao mapema kunachangia kwa kiasi kikubwa utoaji hafifu wa taaluma kwa wanafunzi.

Hata hivyo, Katibu Tawala wa mkoa ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kikao hicho  Liana Hassan alisema kuwa suala la malimbikizo ya madai ya walimu ni la kitaifa zaidi.


“Uhakiki wa madai yao unaendelea kabla ya malipo yoyote kufanyika na baada ya hapo wote wenye madai halali watalipwa stahili zao. Ila yeyote ambaye atabainika kuwasilisha madai ya uongo akae tayari kukumbana na mkono wa sheria” alisema.

No comments:

Post a Comment