Saturday, April 25, 2015

Singida yawaonya Waganga wa tiba mbadala kutofanya mapenzi na wateja wao wanaowahudimia.

Maafisa watendaji wa vijiji,kata,Wenyeviti wa vitongoji pamoja na wenyeviti wa vijiji waliohudhuria kwenye semina elekezi juu ya operesheni tokomeza mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi(albini) na vikongwe iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kituo cha walimu Ndago.
Mratibu wa Tiba Asilia kutoka Hospitali ya wilaya ya Iramba,Bi Roda Yona akitoa mada katika semina hiyo ambayo pia elekezi juu ya operesheni tokomeza mauaji ya watu wenye ulemavu (albino) na vikongwe iliyofanyika kata ya Ndago.

Katibu Mkuu wa Chama cha watafiti wa Maleria Sugu,Ukimwi na Mazingira Tanzania(CHAWAMAMU) Mkoa wa Singida,Dk.Tano Mika Likapakapa akisisitiza jambo kwenye semina elekezi Ndago.
Ni Baadhi ya waganga wa tiba mbadala na wakunga waliohudhuria kwenye semina elekezi kutoka vijiji vilivyopo katika kata ya Ndago.

Waganga wa tiba mbadala wilayani Iramba, Mkoani Singida wameshauriwa kutofanya mapenzi na wateja wao wanaoshindwa kulipa gharama za matibabu waliyowapatia na badala yake wafuate sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utoaji wa huduma zao.

Mratibu wa Tiba Asilia kutoka katika Hospitali ya wilaya ya Iramba, Roda Yona alitoa ushauri huo kwa nyakati tofauti alipokuwa akitoa mada kwenye semina elekezi kwa waganga wa tiba mbadala na wakunga iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kituo cha walimu cha Ndago.

Alifafanua mratibu huyo kuwa mteja anapokwenda kwa mganga wa tiba mbadala kwa lengo la kupatiwa tiba hatakuwa ametendewa haki na mganga husika anaposhindwa kulipa gharama za matibabu aliyopata endapo atatakiwa kufanya vitendo vya ngono na mganga aliyempatia huduma za tiba yake.

“Unapokuwa na mteja wako akaja nyumbani kwako akapata huduma kwako akakosa malipo, naomba usimtumie,kama chambo cha wewe kupata mafanikio katika shughuli zako au ukamtumia yeye kama mke wako kwa sababu ameshindwa kukulipa huruhusiwi huo ni ukiukwaji wa sheria”alisisitiza mratibu huyo.


Kwa mujibu wa Roda endapo mganga yeyote yule atachukua hatua ya kufanya vitendo vya ngono na mgonjwa wake kwa kumbadili kuwa mke wake atakuwa amechukua hatua hiyo bila ridhaa ya mteja wake kwa kuwa atakuwa amekubali kuolewa kwa kukosa fedha za kulipa gharama za matibabu.

Naye Mary Nagunwa ambaye ni mkunga aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuandaliwa semina maalumu kwa ajili ya wakunga kwa kile alichodai kwamba masuala yahusuyo wakunga ni magumu sana na hubadilika mara kwa mara.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Chama cha Watafiti wa Malaria sugu,Ukimwi na Mazingira Tanznaia  (CHAWAMAMU),Dk.Tano Mika Likapakapa aliweka bayana kwamba mganga yeyote yule anayetaka kwenda kufanya shughuli ngumu ya tiba kwa wateja wake nje ya eneo analoishi,atalazimika kuchukua barua kwa mkuu wa wilaya husika kabla ya kwenda anakotakiwa kutoa huduma hiyo.


Mwenyekiti wa kitongoji cha Songambele,Simioni Msambala alisema haoni sababu kwa waganga wa tiba mbadala kupewa muda wa siku nne ili waende kuchoma au kusalimisha nyara za serikali wanazotumia kinyume cha sheria wakati wapo katika ukumbi wa semina kutokana na kuwepo kila dalili kwamba wanatumia viungo vya watu.

No comments:

Post a Comment