Saturday, April 25, 2015

Waganga wa tiba mbadala Singida wanaotumia nyara za Serikali kupigia ramli chonganishi watakiwa kuzisalimisha Polisi.

Katibu Mkuu wa CHAWAMAMU Mkoa wa Singida, Dk.Tano Mika Likapakapa (wa kwanza kulia)Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Lunsanga,Bw.Richard Kisiwa (katikati) na Mkuu wa Kituo kidogo cha polisi Ndago, Bw.Richard Kimolo.
Afisa kilimo wa kata ya Ndago, Bi Perpetua Pius (kushoto) na Mratibu wa Tiba Asilia kutoka Hospitali ya wilaya ya Iramba,Bi Roda Yona(kulia).

Waganga wa tiba mbadala waliovaa mavazi wanayotumia wakati wa shughuli zao.
 Maafisa watendaji wa vijiji na wenyeviti wa serikali za vijiji Mtekente.
 Waganga wa tiba mbadala wa kata ya Mtekente.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Madukani Mtekente, Bi. Mwanjaa Baraka (Mwenye ushungi wa mtandio wa kizambarau).

CHAMA cha Watafiti wa Maleria Sugu,Ukimwi na Mazingira Tanzania (CHAWAMAMU) Mkoa wa Singida kimetoa muda wa siku nne kwa waganga wa tiba mbadala wanaotumia nyara za serikali kupiga ramli chonganishi kuzisalimisha kwenye kituo cha polisi kilicho karibu kwa hiyari yao wenyewe na kwamba baada ya muda huo kumalizika kinatarajia kufanya msako wa nyumba hadi nyumba kwa kila mganga wa tiba mbadala kwa lengo la kukusanya nyara hizo za serikali.

Katibu wa CHAWAMAMU Mkoa wa Singida,Dk.Tano Mika Likapakapa alitoa agizo hilo kwenye semina elekezi inayoendelea katika tarafa ya Ndago juu ya utekelezaji wa agizo alilolitoa rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,kuhusu operesheni ya tokomeza mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) na vikongwe nchini.

Aidha Dk.Likapakapa alifafanua kwamba sambamba na msako huo wa nyumba hadi nyumba,endapo watabainika waganga wa tiba mbadala watakaokuwa wameshindwa kusalimisha nnyara hizo za serikali wanazofanyiakazi zao kwa hiyo baada ya muda huo,watalazimika kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Alisema kiongozi huyo wa waganga wa tiba mbadala kwamba kumekuwepo malalamiko mengi kutoka nchi za nje kuwa matukio ya vifo vya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe yamezidi kutokea siku hadi siku nchini huku kukiwa hakuna mikakati madhubuti ya kukabiliana na vifo hivyo.

Hata hivyo Dk.Likapakapa alivitaja baadhi ya vigezo vitakavyotumika kuwakamata waganga hao wakati wa msako huo kuwa ni pamoja na wale ambao watakutwa na ngozi za wanyama,mapembe,mafuta yasiyofahamika vizuri na nyara zozote zile za wanyama zinazotumiwa na waganga hao kwenye shughuli zao za kupiga ramli chonganishi. 

Naye Mratibu wa Tiba Asilia kutoka Hospitali ya wilaya ya Iramba,Roda Yona akiwasilisha mada yake ya usafi wa mazingira aliweka bayana kwamba katika kipindi cha miaka sita sasa tangu aliposambaza fomu kwa waganga wa tiba mbadala ili waweze kuzijaza kwa lengo la kutambulika na kupatiwa usajili,lakini mpaka sasa hakuna hata mmoja aliyejaza na kurejesha fomu hizo. 

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha maafisa watendaji wa kata na vijiji kwamba waache tabia ya kuwakwamisha waganga hao kwa kuwatoza fedha wanapokwenda kuomba msaada wa kusainiwa fomu zao kwa kile alichodai kwamba huduma hiyo hutolewa bure. 


Kwa upande wake mmoja wa waganga wa tiba mbadala waliohudhuria mafunzo hayo,Nkuba Kandila alisema kwa kipindi cha utoaji wa huduma za uganga,jeshi la polisi limekuwa likimbambikia kesi za matukio asiyohusika nayo na kumtoza faini kubwa na anapolipa hakuna stakabadhi ya serikali anayopewa.

No comments:

Post a Comment