Thursday, May 7, 2015

Halmashauri ya Singida yakusanya mapato ya sh bil 11/-

Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida vijijini, Elia Digha, akitoa taarifa ya mapato na matumizi kwa kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Machi 30 mwaka huu mbele ya kikao cha kawaiada cha madiwani. Digha alisema kuwa halmashauri hiyo ilikusanya zaidi yashilingi bilioni 11.4 ikiwa ni sawa na asilimia 49 ya  lengo la kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 22.1.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida vijijini, Iddi Mnyampanda, akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha kawaida cha madiwani kilichofanyika mjini Singida. Kulia ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Singida vijijini Hajjat Farida Mwasumilwe na kushoto ni makamu mwenyekiti Elia Digha.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Singida vijijini waliohudhuria kikao cha baraza kilichofanyika leo (30/4/2015) mjini Singida.

HALMASHAURI ya wilaya ya Singida,imekusanya zaidi ya shilingi 11.4 bilioni kutoka vyanzo vyake mbalimbali vya mapato  kati ya julai mwaka jana na machi mwaka huu, sawa na asilimia 49 la lengo la kukusanya zaidi ya shilingi 22.1 bilioni.

Hayo yamesemwa na makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Elia Digha, wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya makusanyo ya mapato mbalimbali katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu mbele ya kikao cha kawaida cha madiwani.

Digha ambaye ni diwani wa(CCM)  kata ya Msange, alisema kati ya mapato hayo,mapato ya ndani wamekusanya zaidi ya shilingi 214.2 milioni kati ya lengo la kukusanya zaidi ya shilingi 733,865,000.

“Serikali kuu imetupatia zaidi ya shilingi 69.6 mlioni zikiwa ni kwa ajili ya kufidia vyanzo vya mapato vilivyofutwa kutokana na kuwa kero kwa wananchi.Pia imetupatia zaidi ya shilingi 7.4 bilioni kwa ajili ya kulipia mishahara ya umma katika kipindi hicho”,alisema.

Aidha, Makamu mwenyekiti huyo, alisema kuwa katika kipindi hicho serikali kuu vile vile imewapatia zaidi ya shilingi 612 milioni kwa matumizi yasiyo ya mishahara,wakati miradi ya maendeleo ya wananchi, wamepatiwa zaidi ya shilingi biloni tatu kati ya lengo la kupatiwa shilingi bilioni 8.4.

Digha alitaja kata tatu zilizofanya vizuri katika kukusanya mapato ya ndani na aslimia zake kwenye mabano kuwa ni Ngimu (76),Mughamo (58) na Mughunga (50),wakati zilizofanya vibaya ni Kinyeto (15),Ntonge (17) na Mrama (18).

Awali akifungua kikao hicho, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Iddi Mnyampanda, aliwataka madiwani hao kuongeza juhudi katika kukamilizia ujenzi wa maabara mapema mwezi ujao.

Aidha, alisema wakafanye mikutano ya kuhamasisha wananchi kutunza chakula kidogo watakachovuna mwaka huu,ili kukabiliana na uhaba wa chakula ambao umechangiwa na uhaba mkubwa wa mvua katika msimu huu.

“Wananchi watunze vizuri chakula, wasikitumie kukorogea pombe za kienyeji na wakati huo huo,wapunguza mifugo kwa kuiuza mapema kabla ya kuanza kukonda ili fedha waweze kununualia chakula cha kutosha”, alisema Mnyampanda.


Wakati huo huo,mwenyekiti huyo alisema wakati wo wote kuanzia sasa,watapokea walimu wapya katika shule za halmashauri hiyo,kwa hiyo madiwani wawe tayari kuwapokea na kuwaandalia mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

No comments:

Post a Comment