Tuesday, May 12, 2015

Klabu ya waandishi wa habari mkoani Singida yatakiwa kuzingatia weledi katika taaluma yao.

Kaimu mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida, Cosbert Mwinuka, akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa Singida Press Club (Singpress) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel ya Muhai iliyopo kijiji cha Nduguti.Wa pili kulia (walioketi) ni mwenyekiti wa Singpress, Seif Takaza na wa kwanza kulia ni makamu mwenyekiti wa Singpress,Damiano Mkumbo.
Baadhi ya wanachama wa Singpress,waliohudhuria mkutano mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Muhai iliyopo katika kijiji cha Nduguti wilaya ya Mkalama

WAANDISHI wa habari mkoani Singida,wameombwa kutumia taaluma yao kuitangaza wilaya mpya ya Mkalama,ili pamoja na mambo mengine,fursa za uwekezaji zilizopo wilayani humo ziweze kufahamika ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwavutia wawekezaji.

Ombi hilo limetolewa na kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo,Cosbert Mwinuka,wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka (2014) wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Singida, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Muhai kijijini Nduguti.

Alisema wilaya mpya zilizoanzishwa miaka ya karibuni,zinakabiliwa na changamoto nyingi katika kujiletea maendeleo yake’ na hivyo zinahitaji kuungwa mkono na wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji.

Aidha, Mwinuka amewataka pia watumie taaluma yao kuihamasisha na kuielimisha jamii wilayani humo,   iweze kujiendeleza kijamii na kiuchumi ili iweze kuishi maisha bora.

“Naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha kuwa mhakikishe kabla ya kutoa habari yo yote,kwanza muifanyie uchunguzi wa kina.Kwa njia hiyo mtakuwa mmeondoa uwezekano wa kupotosha jamii na mtajijiengea mazingira mazuri ya kuendelea kuaminiwa na wananchi.zingatieni maadili yenu wakati wote mnapokuwa mnatekeleza majukumu yenu”,alisisitiza Mwinuka.

Kaimu huyo mkurugenzi ambaye ni afisa kilimo,umwagiliaji na ushirika katika wilaya hiyo,alisema halmashauri ya wilaya Mkalama,milango yake ipo wazi kwa waandishi wa habari sio tu kuitangaza wilaya hiyo,bali ni pamoja na kutangaza changamoto mbalimbali zinazoikabili wilaya hiyo,ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Singida,Seif Takaza, amewataka wanachama wa klabu hiyo kujiepusha na tabia ya kuanikana kwenye vyombo vya habari,bali wasitiriane ili kulinda amani na utulivu ndani ya klabu hiyo.

Aidha,Takaza amewataka wananchama hao wajiandae na kujikagua vizuri kama wanazo sifa za  kuomba nafasi mbalimbali za uongozi, kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment